ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 2, 2014

Sendeka:Muhongo tuonane NEC

Asema ni mbumbumbu wa kanuni
Mbunge wa Simanjiro (CCM),Christopher Sendeka
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Sendeka, amejibu mapigo kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo, kutokana na kauli yake kwamba ni mchochezi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM|), akisema waziri huyo kwanza ni mbumbumbu wa kanuni za Bunge na pia za chama tawala katika kutoa malalamiko dhidi ya kiongozi.

Akiwa njiani kuelekea jimboni kwake mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kushiriki ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, Sendeka alisema kinachosikitisha zaidi ni Muhongo kuwashambulia watu badala ya kujibu hoja kuhusu ‘ufisadi’ wa fedha za IPTL kwenye akaunti ya Escrow.

Pia alisema kuwa Muhongo anadhani kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda, ni wakala wa CCM kwa maana hiyo anaweza kuwasilisha kwake malalamiko yake kwa ajili ya chama.

Sendeka alikuwa akijibu kauli ya Waziri Muhongo aliyoitoa bungeni Ijumaa iliyopita majira ya jioni wakati akihitimisha bungeni hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 na kujibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia hotuba yake hiyo.


Prof. Muhongo alisema Mbunge Sendeka, ni mchochezi mkubwa kutokana na kauli zake ambazo amekuwa akizitoa kupitia santuri (CD).
Alisema Sendeka amekuwa akitumia kituo cha televisheni cha ITV kufanya uchochezi huo na kukabidhi santuri hiyo mezani kwa Spika Anne Makinda, kama ushahidi.

Hata hivyo, Prof. Muhongo hakufafanua uchochezi huo wa Sendeka.

“Msheshimiwa Spika, Sendeka ni mchochezi mkubwa … natoa CD aliyokuwa akiitumia kupitia ITV. CCM itampima kuona kama wanataka mwanachama wa namna hii,” alisema.

Alisema alidhani Sendeka ni mtu `geneous’ (mwenye uwezo mkubwa wa kiakili) anayewasumbua sana na hivyo kulazimika kufuatilia matokea yake ya kuhitimu kidato cha nne Baraza la Mitihani la Taifa.

“Nilifuatilia matokeo yake ya kidato cha nne ya Mei…(lakini kabla hajamaliza, Spika wa Bunge, Makinda, alimkatisha na kumtaka apeleke kielelezo hicho mezani kwake.

Sendeka alisema kama Prof. Muhongo anataka kumshitaki kwenye chama, basi anapaswa kufuata taratibu za chama na siyo kumfanya Spika awe wakala wa CCM, kwa kuwa chama kina taratibu zake tofauti na Bunge.

Alisema atafurahi kama Waziri Muhongo atalipeleka suala hilo kwenye chama kwani atamsubiri White House Dodoma kupambana naye kwa hoja.

“Nafikiri nitatangulia White House kumsubiri na mashitaka yake,” alisema Sendeka akimaanisha ukumbi ambako vikao vya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM hufanyika mjini Dodoma.

Aidha, Sendeka alisema iwapo Waziri Muhongo anamuona yeye (Sendeka), ni mchochezi, aende akaripoti polisi ili achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria kwa kuwa uchochezi ni kosa la jinai.

Alisisitiza kwamba hoja yake kuhusu sakata la akaunti ya Escrow, bado ni ya msingi kutokana na fedha kuchotwa bila utaratibu.

"Anachopaswa Muhongo kukifanya, ni kujibu hoja kwa hoja na siyo kumshambulia mtu," alisema Sendeka.

Aliongeza kuwa kimsingi Prof. Muhongo bado hajajibu hoja yake na ndiyo maana msimamo wake bado anataka sakata la akaunti ya Escrow lifanyiwe uchunguzi.

Katika maelezo yake, Prof. Muhongo, alisema akaunti ya fedha hizo ilikuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa wanahisa wa IPTL na kuilazimisha Tanesco kuwasilisha malipo ya umeme iliyokuwa ikiuziwa katika akaunti hiyo, ingawa pia kulikuwa na hoja ya malipo hayo kutokuwa sawa.

“Huyu bwana anajua kuwa wizara yake inasimamia Tanesco, fedha zimechotwa bila utaratibu. Tanesco walikuwa na madai yao, sasa zimeondoka huku wakijifanya hawajui lolote. Haiwezekani Muhongo aendelee tu kutukana watu huku akijua amefanya madudu pale wizarani,” alisema Sendeka.

Mbali na kumshambulia Mbunge Sendeka, Prof. Muhongo pia aliwaponda wabunge waliowasilisha bungeni ushahidi dhidi ya IPTL akisema kwamba ana wasiwasi na elimu yao na hivyo kuna haja ya vyeti vyao vya kuhitimu shule vikaguliwe.

Wabunge waliowasilisha ushahidi dhidi ya IPTL ni John Mnyika (Chadema-Ubungo), David Kafulila (NCCR-Kigoma Kusini) na Sendeka.

Alisema yeye (Waziri) anazo documents (nyaraka) za kujaza kigari chenye uwezo wa kubeba mzigo wa tani moja na kwamba ushahidi uliotolewa na baadhi ya wabunge hao ni batili na haujitoshelezi na ni vema utupwe kwenye kapu la kuhifadhia takataka (dustbin).
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: