Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge anayetarajiwa kusoma maoni ya kamati yake leo Bungeni.
Dodoma. Siri ya mvutano uliodumu kwa takriban wiki mbili baina ya Serikali na Kamati ya Bajeti, utawekwa hadharani leo wakati Bunge litakapoanza kujadili Bajeti Kuu.
Mjadala huo utaanza kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge kusoma maoni ya kamati yake na kufuatiwa na Waziri Kivuli wa Fedha, James Mbatia ambaye atasoma maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu bajeti hiyo.
Mbatia pia ni mjumbe katika kamati inayoongozwa na Chenge, hivyo hoja zao huenda zitashabihiana katika baadhi ya maoni na mapendekezo, kubwa ikiwa ni hoja ya kutozingatiwa kwa baadhi ya ushauri kuhusu vyanzo vipya vya mapato.
Kadhalika, hoja kuhusu mzigo wa madeni unaoikabili Serikali, kutokuwapo kwa miradi ya vipaumbele, kutotengwa kwa fedha za kutosha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuyumba kwa bajeti inayoishia Juni 30 mwaka huu, zinatarajiwa kutawala mjadala huo.
Kuanza kwa mjadala huo ndani ya Bunge ni mwendelezo wa kile kilichokuwa kikijadiliwa kwa takriban kwa wiki mbili baina ya Serikali na Kamati ya Bajeti.
Awali kulitokea mabishano makali kutokana na kutotengwa katika bajeti fedha za kulipa madeni ya makandarasi wa ujenzi wa barabara ambayo hivi sasa yanafikia Sh800 bilioni, pamoja na kutokuwapo kwa makadirio ya fedha za kugharimia mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
“Tumewauliza kwamba hizo fedha zitatoka wapi, kwa kuwa katika mafungu ya wizara hizo (Ujenzi na Nishati na Madini) hazikutengwa na hata kwenye bajeti kuu hazipo, sasa zitalipwaje, lakini hawatujibu,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya kikao hicho na kuongeza:
“Tumekuwa na wasiwasi kwamba huenda fedha wanachukua kwenye makusanyo ya kodi na kusababisha kushindwa kutekeleza mahitaji mengine kwenye bajeti. Ndiyo hivyo si mnaona fedha hazikutoka kabisa mwaka huu wa fedha?”
Taarifa Hazina iliyotolewa mbele ya Kamati ya Bajeti inaonyesha kuwa kati ya Oktoba mwaka jana na Machi mwaka huu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), lilipewa Sh578 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa mafuta, ikiwa ni wastani wa Sh96.33 bilioni kwa mwezi.
Akisoma bajeti ya Serikali ya 2014/15, Alhamisi iliyopita, Waziri wa Fedha, Saada Nkuya Salum alitaja gharama kubwa za uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme wa dharura na madeni makubwa ya makandarasi, wazabuni na watumishi kuwa ni baadhi ya changamoto katika utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
Hata hivyo, alisema: “Kuhusu madai ya makandarasi na wazabuni, Serikali inakamilisha utaratibu wa kuyasimamia na kulipa madai yaliyohakikiwa kupitia Hazina kwa kushirikiana na wizara na taasisi zinazohusika.”
Suala lingine ambalo lilionekana kuitisha Kamati ya Bajeti ni ukuaji wa kasi wa deni la taifa ambalo limefikia Sh30.563 trilioni, ambalo kwa mtizamo wa wajumbe wengi ni sawa na asilimia 57.7 ya pato la taifa.
Hata hivyo, Mkuya katika hotuba yake alisema: “Deni la taifa bado ni himilivu” kwa sababu fedha zinazokopwa zimekuwa zikiwekezwa kwenye miradi ya kukuza uchumi ili kuwezesha madeni husika kulipwa yanapoiva.
Kwa nyakati tofauti, Chenge na Mbatia walipoulizwa maoni yao kuhusu masuala hayo, walisema watatoa misimamo yao watakapowasilisha taarifa zao leo bungeni.
Uhamishaji wa fedha
Mwandishi wetu amefanikiwa kuona bango kitita linaloonyesha jinsi Serikali ilivyoafikiana na Kamati ya Bajeti kukata asilimia nane ya fedha za matumizi mengineyo katika kila wizara kuwezesha kupatikana kwa Sh225.281 bilioni ambao zimeelekezwa katika maeneo kadhaa muhimu na yaliyokuwa na uhitaji wa lazima.
Mchanganuo wa fedha hizo uliopo kwenye bango kitita unaonyesha kuwa kati ya fedha hizo, Sh163.701 bilioni zitaelekezwa katika matumizi ya kawaida, wakati Sh61.58 bilioni zimeelekezwa katika shughuli za maendeleo.
Makubaliano hayo yaliyofikiwa kati ya Hazina na Kamati ya Bajeti yanaelezwa kuliumiza vichwa Baraza la Mawaziri ambalo lililazimika kukutana kwa siku tatu tangu Ijumaa kufanya mapitio ya bajeti na marekebisho yaliyopendekezwa.
Habari zinasema baadhi ya wajumbe wa baraza hilo walitoa mapendekezo ya kuwekwa kando kwa mabadiliko hayo ili bajeti ibaki ilivyo, lakini hoja zao zilikosa mashiko kutokana na unyeti wa maeneo husika. Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue jana alikiri kwamba Baraza la Mawaziri lilikuwa na vikao vyake mjini Dodoma, lakini akasema lilikuwa na ajenda nyingine tofauti na bajeti.
“Nadhani taarifa uliyonayo siyo sahihi, kwa kawaida Baraza la Mawaziri hukutana kabla ya Waziri wa Fedha kusoma bajeti bungeni, kwa hiyo hilo lilifanyika, lakini baada ya hapo baraza lilikutana kwa mambo mengine,” alisema Sefue.
Kwa upande mwingine, mwafaka wa pande hizo pia ulizua manung’uniko miongoni mwa wenyeviti wa Kamati za Bunge. Hali hiyo ilitokana na mapendekezo ya kamati zao kutozingatiwa na hata kutoonekana kabisa kwenye bango kitita ambalo hata kwa sekta ambazo hazikuongezewa fedha zilipata ufafanuzi kutoka kwa wataalamu wa Hazina.
Habari za uhakika zinasema kutokana na hali hiyo, walitishia kupinga bajeti, lakini waliridhishwa na hatua ya kuitaka Kamati ya Bajeti na Serikali wakaandae taarifa nyingine itakayojibu hoja zote, uamuzi ambao ulifikiwa wakati wa kikao cha Kamati ya Uongozi, ambacho pia kilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waliopewa fedha
Imebainika kuwa kati ya Sh225.281 bilioni zilizopelekwa kwenye maeneo yanye mahitaji, Sh211.3 bilioni zimetokana na makato ya asilimia nane kwenye fedha za matumizi ya kawaida ya wizara zote, Sh11 bilioni kutoka kwenye fungu la safari za Rais na Sh2 bilioni ni kutoka kwenye Mfuko Maalumu wa Hazina.
Wizara na taasisi ambazo zimenufaika kwa fedha hizo na fedha zao kwenye mabano ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania - Ngome (Sh43.2 bilioni), Wizara ya Uchukuzi (Sh14 bilioni), Jeshi la Kujenga Taifa - JKT (Sh8 bilioni), Wizara ya Kilimo (Sh20.13 bilioni), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Sh12.58 bilioni), Wizara ya Afya (Sh55 bilioni), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Sh4 bilioni), Idara ya Uhamiaji (Sh838 milioni), Wizara ya Habari (Sh6 bilioni), Mambo ya Nje (Sh12 bilioni), Umwagiliaji (Sh13 bilioni), Tamisemi (Sh5.5 bilioni), Hazina (Sh3 bilioni), Zimamoto (Sh898 milioni), Magereza Sh5.785 bilioni, Katiba na Sheria (Sh600 milioni), Polisi Sh20.3 bilioni.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment