KILA kukicha kunaibuka mambo mapya. Katika ulimwengu wa mapenzi kila siku lazima uwe mwanafunzi ili uweze kuboresha uhusiano wako. Ukiacha ubongo wako uingize vitu vipya ni rahisi kubadilika na kuwa wa kisasa zaidi.
Somo la leo linashangaza kidogo lakini ni vizuri kama tukijifunza. Tumezoea kusikia kuwa uongo ni kitu kibaya katika maisha ya mwanadamu – ni kweli. Uongo si mzuri lakini katika uhusiano na mapenzi, wakati mwingine unanafasi na unaboresha sana uhusiano.
Kwa kawaida uongo unakatazwa kuanzia kwenye mafundisho ya dini na hata katika jamii. Mtu muongo si mwaminifu. Hakubaliki.
Hata mwanasiasa ambaye ni muongo, wapigakura wake hawamchagui tena atakaporudi mara ya pili; kwa nini? Kwa sababu aliwaongopea.
Hiyo ni kweli kabisa, lakini hapa katika Let’s Talk About Love nataka kukupa kitu kipya kabisa ambacho hujawahi kukipata mahali popote; uongo mtamu!
Ndiyo! Kuna uongo mzuri tena wenye faida na utakaokusaidia kukuza upendo wako kwa mwenzi wako. Ni suala la kukubali kujifunza tu. Karibu darasani tujifunze...
UDANGANYIFU
Rafiki zangu, sitaki kueleweka vibaya katika hili lakini kama nilivyosema mwanzo, uongo si kitu kizuri kwenye jamii. Mtu anayedanganya hakubaliki. Kwa tafsiri ya haraka, mwongo si mwaminifu.
Haaminiki kwa sababu ni rahisi kutunga mambo ambayo hayapo na akayatengenezea mazingira yakaonekana ni ya kweli. Huyu hafai hata kidogo. Lakini rafiki zangu, katika uhusiano upo uongo ambao unakubalika kama nilivyosema.
Nasema unakubalika maana una lengo la kutengeneza uhusiano, kuufanya uendelee kuwa na nguvu na si kuupoteza.
Huo ndiyo uongo unaokubalika. Kabla sijaenda mbele zaidi hebu twende tukaone kwanza tofauti ya uongo mzuri na mbaya halafu tutaendelea na darasa letu.
UONGO MZURI
Haikubaliki hata mara moja kumdanganya mpenzi wako kuhusu taarifa zako muhimu. Nasema hivyo kwa sababu utakuta mwingine anafanya kazi mahali fulani, lakini kwa sababu ya kutaka ukubwa anadanganya kwamba anafanya kwenye taasisi fulani kubwa.
Huo ni ulimbukeni ambao hauna maana. Mweleze mwenzi wako ukweli, ukifanya hivyo atakuwa anajua yupo na mpenzi wa namna gani. Una sababu gani ya kumdanganya mwezi wako?
Wapo wanaodanganya wanatoka katika familia zenye uwezo mkubwa kifedha, huku wengine wakijipachika majina ya koo maarufu ili waheshimiwe na wapenzi wao, huo ni utumwa, mbaya zaidi kuna siku ukweli unajulikana halafu unabaki na aibu zako.
Ndugu zangu, katika maisha ya kila siku ni vyema ukawa mkweli kwa watu muhimu wanaokuzunguka hasa mtu ambaye unatarajia awe mwezi wa maisha yako. Utaficha mpaka lini wakati kuna siku atagundua ukweli? Kuwa mkweli.
UONGO MZURI
Naam! Upo uongo ambao unakubalika rafiki zangu. Unajua kuna baadhi ya mambo ukiyasema kwa usahihi kama yalivyo yanaweza kuleta athari kwenye uhusiano, ndiyo maana nimesema kwamba upo uongo unaokubalika.
Inawezekana umefanya kitu ambacho hakimpendezi mpenzi wako, ama kwa kujua au kutokujua, lakini baada ya kuhisi labda amegundua na kukuuliza, unakataa. Ukikubali kwa kitu ambacho hakipendi inaweza kusababisha penzi kuvunjika.
Unabaki kuwa uongo mzuri kwa sababu kwanza una lengo la kulinda penzi, lakini pia hauna madhara kwa mpenzi wako. Huo ndiyo uongo mzuri ninaouzungumzia hapa.
Kwa nini nasema wakati mwingine uongo unahitajika kwenye mapenzi? Kuna mambo zaidi ya kujadili kuhusu kipengele hiki, lakini kutokana na nafasi yangu kuwa ndogo, naomba niishie hapa kwa leo.
GPL
No comments:
Post a Comment