Zanzibar: Jeshi la Polisi Zanzibar limesema bomu la kurushwa lililolipuka juzi katika eneo la Darajani na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wengine saba ni la kivita lililotengenezwa kiwandani.
Bomu hilo lilirushwa na kulipuka muda mfupi baada ya watu kuhudhuria mawaidha msikitini yaliyokuwa yakitolewa na Sheikh Kassim Mafuta Kassim(38) kutoka Tanga ambaye kutokana na tukio hilo, amesitisha ziara yake Zanzibar kwa sababu za kiusalama.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alisema jana kwamba uchunguzi wa awali umebaini bomu hilo hutumika kwa shughuli za kivita na kwamba hiyo ni mara ya pili kwa bomu kama hilo kutumika katika matukio tofauti Zanzibar.
“Mabaki tuliyoyapata yametusaidia kutambua bomu lililotumika ni Hand Grenade na hutumika kwa shughuli za kivita,” alisema na kuongeza kuwa wataalamu wanne wa kuchunguza mabomu waliwasili juzi kutoka Makao Makuu Polisi Dar es Salaam na kuungana na wenzao wa Zanzibar kuongeza nguvu za uchunguzi.
“Uchunguzi wa kitabibu uliofanywa katika mwili wa marehemu Mohamed Khatib Mkombalaguha umebaini kuwa kifo chake kimesababishwa na vipande vya vyuma vilivyotoboa moyo wake baada ya bomu kulipuka,” alisema.
Hata hivyo, Kamanda Mkadam alisema hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo na uchunguzi unaendelea ili kuwabaini wahusika na kupitia mikanda ya video na kusikiliza mawaidha yaliyokuwa yakitolewa na Sheikh Kassim ili kuwasaidia kubaini chanzo.
Akizungumzia ziara ya Sheikh huyo, Kamanda Mkadam alisema alifika Zanzibar Jumatatu iliyopita kwa mwaliko wa Masjid Farouq wa Kibandamaiti kupitia kwa Sheikh Omar Abuulukman na tayari alikwishatoa mawaidha katika misikiti mitano ya Zanzibar.
Kamanda Mkadam alisema Sheikh Kassim ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo, amelazimika kusitisha ziara zake za kutoa mawaidha kwa sababu za kiusalama na tayari ameshaondoka Zanzibar.
Hadi jana, majeruhi wanne walikuwa wameruhusiwa akiwamo Sheikh Ahmed Haidar Jabir na mwanawe Khalid Ahmed Haidar pamoja na mwanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari Vikokotoni, Suleiman Ali Juma.
Msemaji wa familia ya Sheikh Ahmed, Sheikh Kassim Haidar alisema ndugu yake pamoja na mtoto wake wameruhusiwa jana na wanaendelea vizuri.
“Madaktari wamefanikiwa kutoa vipande sita vya vyuma vya bomu katika miguu ya Sheikh Ahmed na mwanaye katika sehemu za miguuni na mkononi,” alisema.
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mungulu aliwasili visiwani humo kwa ajili ya tukio hilo jana lakini hakuna taarifa rasmi iliyotolewa.
JK atoa amri kwa polisi
Rais Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki wale wote waliohusika katika tukio hilo lisilo la kistaarabu.
Katika salamu zake za pole alizomtumia Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Rais Kikwete alisema kitendo hicho ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara na Visiwani.
“Ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na wala hakikubaliki katika dunia ya sasa,” alisema Rais.
Rais alielezea kusikitishwa na watu hao kufanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya kidini na ambako panastahili amani, uvumilivu na unyenyekevu zaidi kwa kuwa ni wakati binadamu anapofanya mawasiliano na Muumba wake.
Mwananchi
1 comment:
Kumbe kuna mabomu yasiyokuwa ya kivita?
Post a Comment