Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP),Ernest Mangu.
Matukio ya kuuawa kwa askari polisi yanazidi kuongezeka kwa kasi nchini na kuutikisa uongozi wa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) mpya, Ernest Mangu (pichani).
Mangu aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete Desemba 30, mwaka jana kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Said Mwema, uongozi wake umekumbana na majanga ya mauaji ya askari polisi yanayofanywa na majambazi katika maeneo kadhaa ya nchi.
Matukio hayo yanayoendelea kwa kasi maeneo mbalimbali ya nchi, yanazidi kulipa Jeshi la Polisi wakati mgumu katika kutekeleza jukumu lake la kulinda raia na mali zao.ya kikazi nchini China na kuelekeza atafutwe Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Issaya Mngulu.
Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE, Mngulu alitaja matukio ya kuuawa kwa polisi sita na wanne kujeruhiwa.
Alilitaja tukio la kwanza lililotokea Zanzibar kijiji cha Pongwe Machi Mosi, mwaka huu la kuuawa Koplo Mohamed Mjombo na Koplo Juma kujeruhiwa wakati wakilinda hoteli ya kitalii ya Bongo Bay, iliyopo Kusini Unguja.
Tukio la pili alisema lilitokea Aprili 29, mwaka huu wilayani Temeke, Dar es Salaam alikouawa askari Koplo Busagala wakati akipambana na majambazi yaliyovamia makazi ya watu.
Mei 2, mwaka huu wilaya ya Longido, mkoa wa Arusha, askari mmoja PC Sabato, aliuawa kwa kupigwa jiwe la kichwa akiwa anamshikilia mtuhumiwa wa kesi ya uvunjaji wa nyumba.
Mngulu alilitaja tukio lingine la Mei 27, mwaka huu la kuuawa askari wawili waliouawa mkoani Tabora, PC Shaban na PC Jumanne, ambao walishambuliwa na majambazi wakati wakielekea eneo la tukio lililokuwa limevamiwa na majambazi.
Tukio jingine ni la Mei 23, mwaka huu aliuawa askari mmoja eneo la Stakishari Ukonga, Dar es Salaam. Hata hivyo, Mngulu hakutoa maelezo kuhusiana na tukio hilo wala kutaja jina la askari aliyeuawa.
Tukio jingine ni la Juni 11, mwaka huu alipouawa askari Koplo Joseph Ngonyani, baada ya majambazi kuvamia kituo kidogo cha polisi cha Mkamba, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani na kuwajeruhi mgambo wawili. Hata hivo, kesho yake mgambo mmoja alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.
Aidha, katika tukio hilo, bunduli tano aina ya Shotgun tatu na SMG mbili kila moja ikiwa na risasi 30 ziliporwa.
Pamoja na Mngulu kusema polisi waliouawa ni wanne, taarifa zilizopo ni kwamba, tangu IGP Mangu aingie madarakani ni polisi 10, waliouawa na majambazi.
Pia Mngulu hakutaja tukio lilitokea mkoani Mtwara lililohusishwa mkuu wa upelelezi wa wilaya (OC-CD) na askari mmoja ambao waliuawa kwa risasi na mtu aliyedaiwa kuwa ni jambazi baada ya kupora fedha katika kituo cha mafuta cha Camel kilichopo katika msitu wa Kiduni.
OC-CD aliyeuawa ni wa Wilaya ya Newala, ASP F. 8106 Nurdun Kassim Sif na DC Robert F. 5339 ambao walipigwa risasi sehemu mbalimbali za miili na kufariki dunia hapo hapo.
Mngulu hakuwa tayari kueleza sababu zinazochangia majambazi kuwaua polisi, lakini alisema ni muhimu raia wakajua kuwa Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda usalama wao, hivyo wanatakiwa kuonyesha ushirikiano.
Badala yake alisema wanajipanga kutoa mafunzo kwa askari kuhusu namna ya kukabiliana na matukio kama hayo ikiwa ni pamoja na mbinu za kisasa za kukabiliana na majambazi.
Aidha, Mngulu, alisema hivi karibuni kumeshamiri matukio ya wananchi kuchukua sheria mikononi badala ya kusubiri jeshi la polisi kufanya kazi yake.
“Nawaomba wananchi waache kujichukulia sheria mkononi wanapoona tukio limetokea waliripoti katika kituo cha polisi ili sheria ichukue mkondo wake,” alisema Mngulu.
Aliongeza kuwa, vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mikononi vinakatisha tamaa askari.
Baadhi ya wananchi wakizungumzia vitendo vya kuuawa kwa askari wamesema hali hiyo inaleta hofu kwenye jamii kwa kuwa hao ndiyo wamepewa jukumu la ulinzi wa raia na mali zao.
Hamisi Omary, mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam, alisema inahitajika elimu kwa raia juu ya kazi za Jeshi la Polisi kwani hali ikiendelea hivi polisi watakuwa hawafiki maeneo ya matukio kuhofia usalama wao.
Naye Dani Noha, mkazi wa Mwananyamala, Dar es Salaam, alisema matukio ya raia kuwashambulia polisi wakati mwingine yanatokana na baadhi ya askari wasiokuwa waaminifu kuhusika na matukio ya kihalifu kwenye maeneo mbalimbali na ndiyo maana imefikia wakati wananchi hawaamini tena.
Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema vitendo vya askari polisi kuuawa na raia ni jambo la hatari kwa taifa na kwamba Jeshi Polisi linatakiwa kujiimarisha kwa ulinzi wao kwanza.
Mkurugenzi wa LHRC, Dk. Hellen-Kijo Bisimba, alisema kituo hicho kinalaani vitendo hivyo na kwamba kimeanza kuvitolea taarifa kwenye ripoti yake ya mwaka jana.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi linatakiwa kupata mafunzo maalum ya kujilinda zaidi na vitendo hivyo kabla ya kulinda raia kwani vitendo vya kushambulia askari ni hatari.
“Polisi kupigwa na kuuawa inaonyesha wazi kuwa kuna shida mahali, polisi kama walinzi wanahitajika kuwa walinzi zaidi na maisha yao kabla ya wale wanaowalinda,” alisema Bisimba.
Alisema hali hii inaonyesha wazi kuwa ulinzi uko matatani na kwamba katika tukio lililotokea hivi karibuni la polisi kuuawa lilionyesha wazi kuwa polisi haikujiimarisha.
“Vitendo kama hivi tunavilaani, ni tatizo kwa nchi na tunalaani mauaji ya raia yeyote katika taifa letu, hivyo polisi na raia tunapaswa kujiimarisha,” alisema Bisimba.
Imeandikwa na Kamili Mmbando, Elizabeth Zaya na Mary Geofrey.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment