Serikali ya Tanzania imetoa
vyeti vya uraia wa Tanzania kwa
raia wa Somalia zaidi ya elfu moja na
mia tano,ambao kiasili walitokea nchini Tanzania zaidi ya karne tatu
zilizopita.Raia hao ambao asili yao wanasema kuwa ni kutoka kabila la wazigua kutoka mkoani Tanga,walizaliwa na kukulia nchini Somalia huku ikiaminika kuwa wao walitokea nchini Tanzania enzi za biashara ya Utumwa kwa zaidi ya ambapo wamekuwa wakitambulika kama Wasomali wabantu.
Mwandishi wa BBC Erick David Nampesya ambaye alihudhuria halfa hiyo anasema kuwa hatua hiyo ya serikali ya Tanzania inahitimisha miaka zaidi ya ishirini ambayo raia hao wapya wa Tanzania wamekuwa wakiishi kama wakimbizi katika nchi inayoaminika kuwa ndiyo asili yao ambayo mababu zao walichukuliwa na kupelekwa ughaibuni enzi za biashara ya utumwa zaidi ya karne tatu zilizopita.
Baadhi na Raia hao wapya niliozungumza nao wameishukuru sana serikali ya Tanzania.
Raia hao wapya wa Tanzania wamepewa uraia ikiwa ni kwa mujibu wa sheria za Tanzania baada ya serikali ya Tanzania kuwafanyia usajili na kuridhika kuwa hapakuwa na sababu za kuwanyima uraia huku pia kukiwa na kundi jingine la wasomali wabantu 150 ambao bado wanasita kuomba uraia wa Tanzania.
Naye waziri wa mambo ya ndani nchini Tanzania Bwana Mathias Chikawe baada ya kuwakabidhi vyeti vya uraia raia hao aliwataka kujisikia kuwa huru.
Hata hivyo aliwataka kuheshimu sheria za nchi na kutowaruhusu maadui wa nchi kuvuruga amani kwenye kijiji hicho cha Chogo,huku akiwataka kujilinda na matendo ya kigaidi na kutoruhusu kushawishiwa na maadui wanaoweza kutumia njia mbali mbali kama mihadhara ya kidini au kisiasa.
Kwa upande wake mwakilishi wa shirika la umoja wa mataifa nchini Tanzania Bi Joyce Mends Cole anasema jukumu lao kwa raia hao sasa limekamilika baada ya kupata uraia,huku shirika hilo likiwa limewajengea zahanati katika kijiji cha Chogo,shule na kuimarisha mradi wa maji ya kunywa.
Wengi wanatumia Kiswahili ambacho ni lugha ya asili ya Tanzania lakini pia raia hao wanazungumza kwa ufasaha lugha ya kizigua na sasa wakiwa wameongezea lugha ya kisomali waliyojifunza ughaibuni nchini Somalia.
Inaaminika kuwa nchini Somalia bado kuna Watanzania wengi asilia wanaoishi nchini humo ambao hawana namna wanayoweza kuja nchini Tanzania ingawa wana hamu ya kufanya hivyo.
BBC
No comments:
Post a Comment