ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 12, 2014

TUWAEPUSHE VIJANA WETU NA UHAFIDHINA-NAIBU WAZIRI SILIMA

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon,  akifunguza majadiliano  kuhusu mazingira yanayochangia kuendenea kwa vitendo vya  kigaidi.  majadiliano hayo yamefanyika siku ya  Jumatano yakitangulia mkutano wa nne utakafanya tathmini kuhusu Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kudhibidi Ugaidi.  Katika salamu zake, Katibu Mkuu amesema hakuna sababu iwayo yoyote ile  inayoweza kuhalalisha ugaidi.  Kulia kwake ni Rais wa Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa Bw, John Ashe .
 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe.  Pereira Silima ( Mb) akichangia majadiliano hayo. Naibu  Waziri anaongoza ujumbe wa Tanzania.  Katika  mchango wake amesema kuna kila sababu ya  kuhakikisha kuwa vijana hasa wale wasiokuwa na  ajira hawashawishiki kujiunga na uhafidhina na kwamba kutoka na changamoto mbalimbali zikiwamo za ukubwa wa mipaka baina ya nchi na nchi, tishio la ugaidi na uhafidhina kwa nchi za Afrika Mashariki ni kubwa.

 Wajumbe walioshiriki majadiliano kuhusu masuala ya ugaidi na changamoto zake wakimsikiliza Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Silima
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huu  ukiongozwa na Naibu Waziri Silima walioketi  nyuma ni  Bw.  Abdalla Khamis  Afisa katika Uwakilishi wa Kudumu na    Bw. David Hiza. Kamishna Msaidizi wa  Jeshi la Polisi na  Mratibu  Kituo cha Kitaifa cha  Kuratibu Mapambano dhidi ya Ugaidi.

Na Mwandishi Maalum, New York

Wakati matukio ya kigaidi yakiendelea kuripotiwa karibu kutoka kila kona ya dunia. Tanzania imesema ipo haja ya msingi ya kitaifa na kimataifa ya kuwaepusha vijana hasa wale wasiokuwa na ajira kurubuniwa na kuwa wahafidhina.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Pereira Silima (Mb) ameyasema hayo siku ya Jumatano hapa Umoja wa Mataifa, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, lilipokutana kujadiliana kuhusu mazingira yanayochangia kusambaa kwa ugaidi.

Katika majadiliano hayo ambayo yalifunguliwa na Katibu Mkuu Ban Ki Moon, Naibu Waziri amesema. “ katika nchi nyingi za Afrika, ongezeko la idadi kubwa ya vijana wasio kuwa na ajira kunatoa mwanya mkubwa kwao kurubuniwa na makundi yenye itikadi kali”.

Akasema vijana wanaweza kuepushwa na uhafidhina ikiwa serikali zitawawesha kwa kuwapatia nyenzo na ujuzi mbalimbali. Na katika hili ushirikiano na wadau mbalimbali utahitajika.

Naibu Waziri Silima akasisitiza matukio ya kihafidhina yanazidi kuwa changamoto kubwa katika eneo la Afrika Mashariki. Na kwamba lengo kubwa la uhafidhina huo ni kuwaanda vijana wenye itikadi kali ikiwa ni pamoja kutumika kujilipua kwa kujitoa muhanga huku wengine wakijiunga na kwenda kupigana kwenye makundi ya kigaidi.

Akizungumzia mazingira yanayosababisha kuenea kwa matendo ya kigaidi Naibu Waziri, ameyataja baadhi ya mazingira hayo kuwa ni ukubwa wa mipaka baina ya nchi na nchi, biashara haramu ya binadamu na madawa ya kulevya, uingizaji holela wa silaha na matumizi mabaya ya mitandao.

Akizungumzia namna gani Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejiandaa kukabiliana na vitendo vya kigaidi. Naibu Waziri amesema , pamoja na mikakati mingine,Tanzania ni mwanachama wa taasisi nane za kimataifa na kimoja cha kikanda zinayohusika na masuala ya ugaidi na pia imepitisha kanuni za kudhibiti ufuaji wa fedha chafu.

Juhudi nyigine zinazofanyika ni pamoja na kufungua kituo cha kitaifa cha kuratibu mapambano dhidi ya ugaidi, kuandaa na kuratibu mipango mbalimbali inayofungua fursa za ajira, kujiajiri na ujasiliamali, uwezeshwaji wa wanawake na uboreshaji wa vyuo vya ufundi stadi.

Vile vile Naibu Waziri Silima, amesema kuanzishwa kwa Polisi Jamii kumesaidia sana katika kukabiliana na uhalifu wa aina mbalimbali. Na kuwa uwepo wa polisi jamii unawahusisha makundi mbalimbali ya jamii wakiwamo viongozi wa madhehebu ya dini.

Awali akifungua majadiliano hayo, ambayo ni sehemu ya mkutano wa nne ambapo nchi wanachama watakutana kwa siku….. kufanya mapitio ya Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ugaidi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon amesema, hakuna sababu yoyote ile inayoweza kuhalalisha vitendo vya kigaidi.

Lakini akasema ugaidi unakua na kuota mizizi pale ambapo kuna migogoro isiyokwisha, ukiukaji wa haki za binadamu, kukosekana kwa taasisi imara za kiserikali, ubaguzi na matarajio hafifu ya usalama na uimara wa maisha.

Akasisitiza kwa kusema changamoto kubwa inayoikabili jumuiya ya kimataifa ni katika kuhakikisha kwamba magaidi hawapati ardhi ya kupandikiza chuki na kutovumiliana. Huku akisisitiza umuhimu wa wathirika wa matukio ya kigaidi kupewa misaada ya hali na mali.

No comments: