ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 3, 2014

Wabunge:Waziri anajipendelea bajeti ya maji jimboni kwake


Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, akisikiliza michango ya wabunge waliochangia bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2014/15 bungeni mjini Dodoma jana.

Baadhi ya wabunge wamemshambulia Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, kwamba amekuwa akipendelea Jimbo lake la Mwanga lililopo mkoani Kilimanjaro kwa kulitengea kiasi kikubwa cha fedha za miradi ya maji huku majimbo yenye ukame mkubwa yakipewa fedha kidogo.

Wabunge hao walitoa shutuma hizo wakati wakichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji Singida kwa mwaka wa fedha wa 2014/15. Hotuba ya wizara hiyo iliwasilishwa bungeni mjini Dodoma na Waziri Profesa Maghembe Jumamosi iliyopita.

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, alisema Mkoa wa Singida ni mmoja kati ya mikoa yenye ukame mkubwa na isiyo na vyanzo vya uhakika vya maji.


Lissu alisema katika Jimbo lake lililopo Wilaya ya Ikugi mkoani Singida lenye kata 12, lina miradi miwili tu ya maji, jambo ambalo alieleza kuwa si sahihi.

Alisema kumekuwapo na utaratibu wa ugawaji wa fedha za miradi ya maji katika majimbo, wilaya ama mikoa isiyo ya haki kutokana na upendeleo mkubwa sana.

Kwa mujibu wa Mbunge huyo, mikoa yenye mahitaji makubwa ya maji, imekuwa ikitengewa fedha kidogo kwa kulinganisha na mikoa yenye unafuu wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.

Aliitaja baadhi ya mikoa yenye ukame na ambayo kimsingi ilipaswa kutengewa fedha nyingi za miradi ya maji kuwa ni pamoja na Singida, Dodoma, Shinyanga na Simiyu. Hata hivyo, alisema licha ya mikoa hiyo kuongoza kwa ukame, lakini kila mwaka imekuwa ikitengewa bajeti ndogo ya miradi ya maji.

Kwa mfano, alisema mkoa wa Singida umetengewa Sh. bilioni 3.304 kwa mwaka wa fedha wa 2014/15, Simiyu Sh. bilioni 2.864, Shinyanga Sh. bilioni 3.296 na Dodoma Sh. bilioni 7.236.

Aidha, Lissu aliitaja baadhi ya mikoa yenye unafuu wa upatikanaji wa maji kuwa ni Tanga ambayo kwa mwaka huu wa fedha imetengewa Sh. bilioni 10.791, Mbeya Sh. bilioni 9.293, Mtwara Sh. bilioni 7.571 na Kilimanjaro Sh. bilioni 6.322.

Alisema Wilaya ya Mwanga ambayo ni Jimbo la Waziri Profesa Maghembe, limetengewa Sh. bilioni 1.4 huku Wilaya ya Makete ambayo awali Naibu wake Waziri, alikuwa ni Mbunge wa Jimbo hilo, Mahenge limetengewa baejeti ya Sh. bilioni 1.9 kwa mwaka huu wa fedha wa 2014/15.

"Mikoa yenye mifumo ya upatikanaji wa maji kwa urahisi, inatengewa bajeti kubwa ya fedha na mikoa yenye tatizo kubwa la maji, inatengewa bajeti ya fedha kidogo...huu ni upendeleo wazi na haufai. Tutamtaka Waziri atakapokuwa anatoa majumuisho ya hotuba yake, aeleze sababu za kufanya hivyo,” alisema Lissu.

Aliongeza kuwa hiyo inaonyesha jinsi mawaziri na naibu mawaziri wanavyotumia fursa za madaraka yao kujipendelea katika majimbo yao.

David Silinde (Chadema-Mbozi Mashariki), alisema anashangazwa na namna Jimbo la Mwanga ambalo mbunge wake ni Waziri wa Maji lenye wakazi wasiozidi 130,000, kutengewa Sh. bilioni 1.4 kwa ajili ya miradi ya maji mwaka wa fedha wa 2013/14 na Sh. bilioni 1.7 kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 huku Jimbo lake la Mbozi Mashariki lenye watu zaidi ya 350,000, likitengewa Sh. milioni 400 mwaka wa fedha wa 2013/14 na Sh. milioni 900 kwa mwaka wa fedha wa 2014/15.

Silinde alisema ni aibu kwa serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya miradi kwa maeneo yenye watu wachache na kutenga fedha kidogo katika maeneo yenye watu wengi.

Mathalan, alisema Tunduma inayoliingizia Taifa mapato mengi, imetengewa Sh. milioni 26 tu za miradi ya maji kwa mwaka mzima.

"Hii ni aibu na si haki inabidi serikali ibadilike kwa kupanga fedha kulingana na mahitaji halisi ya eneo husika," alisema Silinde.

Aliongeza: Jimbo la Mwanga ni dogo lakini linatengewa fedha nyingi...ni aibu na huo ni ubinafsi na ndiyo maana mlibeba viwanja vingi (akimaanisha viwanja vya mpira wa miguu vinavyomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema baadhi ya viwanja hivyo vilivyochukuliwa na CCM baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza nchini ni Kirumba cha jijini Mwanza na Ali Hassan Mwinyi kilichoko mjini Tabora.

Aidha, mbunge huyo alisema kauli ya Waziri Maghembe katika hotuba yake ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2014/15 kwamba kwa sasa asilimia 57 ya Watanzania wanapata maji safi, si ya kweli.

Mbunge wa Kasulu Vijijini (NCCR-Mageuzi), Zaituni Buyogera, alilalamikia mchezo mchafu wa kumuondoa jimboni kwake katika uchaguzi mkuu mwakani, unaofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM kwa kukwamisha miradi ya maji .

Aliliambia Bunge kuwa kuna hila za kuhakikisha miradi iliyo kwenye majimbo ya wapinzani inakwama ili kwenye uchaguzi 2015 wasirudi bungeni.

Alisema Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kasulu ni Diwani anayetoka jimboni kwake, lakini anashindwa kusimamia na kumaliza kazi za kata zinazoshughulikia miradi ya maji na kulalamika kuwa miradi yote ya Kasulu Vijijini haijakamilika.

Alisema Mwenyekiti wa CCM wa Kasulu anatoka kwenye jimbo la Kasulu pia, lakini naye anashindwa kuchochea maendeleo yakiwamo ya maji kwenye jimbo hilo hivyo anakuwa na shaka ya madai ya wananchi waliyotoa kuwa miradi inakwamishwa ili wapinzani washindwe mwakani kwenye uchaguzi.

WACHINA WAKAUSHA MAJI
Wafanyabiashara wa China wameendelea kutuhumiwa kuwa chanzo cha upungufu wa maji nchini kutokana na kushiriki kwenye biashara ya kukata miti na kununua magogo. Mbunge Riziki Lulida Viti Maalumu (CCM), alisema Wachina wanahusika na kununua magogo hayo yaliyosafirishwa kwa wingi kwenda nchi za Asia hasa taifa hilo.

Alisema ukataji miti umekausha maji nchini na sasa unatishia Tanzania kuwa jangwa.

Aliliambia Bunge kuwa hang’ati meno wala kupepesa macho magogo yamekatwa na kupelekwa China na sasa yanaifanya Tanzania kuwa jangwa.

Alimtaka Profesa Maghembe kuwasiliana na Balozi wa China kumueleza kuhusu ukataji magogo na kuharibu mazingira nchini akionya kuwa Wachina wanaipa Tanzania Shilingi mbili na kuchukua rasilimali za mamilioni.

Alisema wanahusishwa na kuharibu misitu na kusababisha kukosekana maji, wanamaliza misitu na kufukuza wanyama akionya kuwa China inatishia hatima ya utalii nchini.

KITENGO CHA MABWAWA CHA WIZARA
Rosemary Kirigini, (CCM) Viti Maalumu, aliitaka Wizara ya Maji kukishughulikia kitengo cha mabwawa kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
Alisema kimeshindwa kusimamia mabwawa ambayo hayakamiliki na yale yaliyokamilika utandazaji wa mabomba na miundombinu haujamalizika.

Kirigini ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Meatu, alisema bwawa la Mwanjolo lililoko wilayani humo lililokuwa likamilike mwaka 2009 hadi sasa halijamalizika licha ya kuelezwa kuwa limekamilika kwa zaidi ya asilimia 80.

Alisema Mei 16 mwaka huu alitembelea bwawa la Mwanjolo na Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla, na kugundua kuwa hakuna bwawa lililojengwa mbali na kufyeka fyeka uwanja.

Lakini jana Makalla analiambia Bunge kuwa serikali imetenga Sh . milioni 400 kwa kazi iliyokuwa inatarajiwa kukamilika kwa miezi minne tangu 2008 hadi sasa.

Alihoji kuwa iwapo kazi ya kujengwa bwawa ilikuwa zaidi ya Sh. bilioni 1.2 tayari mkandarasi amelipwa zaidi ya Sh. milioni 900 malipo yalifanyikaje kwa mjenzi ambaye hadi leo ajulikani halipo? Malipo yalitolewaje?

MIRADI YA WB
Wabunge waliiponda miradi ya maji ya Benki ya Dunia kwa kuwa ya kitapeli na isiyokamilika.

Mbunge wa Singida Kusini (CCM), Mohamed Missanga, alisema Benki ya Dunia ni aibu japo licha ya jina kubwa, lakini yanayaofanyika ni fedheha akitaja kuwa tangu 2007 jimboni kwake ni vijiji vitatu pekee vilivyonufaika.

Mbunge huyo alitaka kuanzishwa Mfuko wa Maji kama ilivyo kwa ule wa barabara, wakala wa umeme vijijini (Rea) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCUF) ambao umefikisha mawasiliano vijijini.

KULINDA MIUNDOMBINU YA MAJI
Wabunge walizungumzia suala la walinzi wa vyanzo vya maji kushindwa kupata huduma hiyo.Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM) Sylvester Koka alisema licha ya wananchi hao wa Kibaha kuwa wenyeji wa mto Ruvu na miundombinu ya DAWASA hawana maji.

Alitaka miradi na miundombinu wanayoilinda iwanufaishe wananchi wanaolinda chanzo cha maji iwe Ruvu ama Ziwa Victoria.
WAJAWAZITO KUBEBA MAJI

Suala la wajawazito kubeba maji kwenda kujifungua hospitalini limezungumzwa na wanawake kuelezea jinsi wagonjwa hasa wazazi na wanavyoteseka kwenda na maji hospitalini ili kujifungua

Josephine Chagulla, Viti Maalum (CCM), alisema siyo sawa ukiwaambia waende na maji na kuitaka serikali iliangalie suala hilo ili hospitali za wilaya , vituo vya afya na zahanati viwe na maji ya kutosha. Imeandikwa na Godfrey Mushi na Gaudensia Mngumi, Dodoma
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: