ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 6, 2014

Aveva ampotezea Wambura Simba

Rais Mpya wa klabu ya Simba, Evans Aveva

Rais wa klabu ya Simba, Evans Aveva, amesema kwamba hana muda wa kubishana na mtu yoyote kwasababu hali hiyo itaondoa lengo na shauku ya kuandaa timu bora kwenye ligi kuu ya Bara ili kuwapa raha mashabiki.

Kauli ya Aveva imekuja siku moja baada mgombea wa nafasi ya urais wa Simba aliyeenguliwa kwa kufanya kampeni kabla ya wakati Michael Wambura kuwatetea wanachama 69 waliosimamishwa uanachama kutokana na kuipeleka klabu yao Mahakamani.

Aidha, Wambura alipinga uanachama wake kujadiliwa na mkutano mkuu wa Simba wa mwezi ujao.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Aveva alisema Simba inaendeshwa kwa mujibu wa katiba hivyo hakuna sababu ya kuendelea kubishana na watu kupitia vyombo vya habari.

Alisema kuendelea kutoleana matamko ni kutumia vibaya muda wa kutafakari mambo muhimu yenye kuijenga klabu ambayo kwa miaka minne imeshindwa kuwapa raha wanachama na mashabiki wake kwa ujumla.

“Hii ni Simba mpya yenye kila sababu ya kufikia malengo yake. Sioni kama wapo watu wanaotaka tuendelee kubishana kwenye vyombo vya habari wakati kanuni na sheria zinajieleza wazi juu ya wanaopeleka masuala ya soka mahakamani," alisema Aveva.

“Kutokana na kupania kuvunja makundi ndani ya Simba, pia nilitoa agizo la kuandaliwa kwa mkutano mkuu utakaokuwa na nia njema ya kujadili baadhi ya wanachama wake, akiwamo Wambura, sasa inashangaza kwanini hataki.”

Aveva alisema ameshangazwa na taarifa ya kuwa Wambura hataki kujadiliwa kwenye mkutano huo kwa madai kuwa suala lake lilimalizwa na kamati ya maadili ya Shirikisho la soka (TFF) wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Simba ulifanyika Jumapili iliyopita.

Aveva alisema kimsingi mwanachama yoyote anayekataa kujadiliwa kwenye mkutano mkuu ana matatizo kwa kuwa kikao hicho ndiyo sehemu nzuri ya kujadiliana mambo yote yanayohusiana na klabu yao.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: