ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 23, 2014

Imam, mke, mume wakamatwa na mabomu saba Arusha

2
Mabomu na risasi zilizokamatwa Arusha

Jeshi la Polisi mkoani hapa linawashikilia watu 25 wakiwamo mume na mkewe na aliyewahi kuwa imam wa msikiti mmoja wa jijini hapa kwa tuhuma za kukutwa na mabomu saba ya kurushwa kwa mkono.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za jeshi hilo mkoani hapa, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Isaya Mngulu, alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa na mabomu hayo Julai 21, mwaka huu saa 2.00 usiku katika eneo la Sombetini la Manispaa ya Arusha.

Alisema mabomu hayo sita yanaonyesha yametengenezwa nchini Urusi na moja Ujerumani.

Aliwataja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni aliyewahi kuwa Imamu wa Msikiti huo wa Masjid Quba uliopo Makao Mapya Arusha, Mlinzi wa Mgahawa wa Chinese, Jafari Lema (38), Shabani Musa, Mohamed Nuru, Abdul Mohamedy (31), mfanyabiashara wa mabasi makubwa ya Khandahar , Said Temba (31), Athuman Hussein, Yusuph Ally na mke wake huyo, Sumaiya Juma (19).

Mngulu alisema wanandoa hao wanadaiwa kukutwa na baadhi ya mabomu hayo, risasi sita za short gun, mapanga mawili na bisibisi moja nyumbani kwao.

Alisema kuwa uchunguzi wa polisi umebaini kuwa watuhumiwa sita kati ya hao, wanadaiwa kuhusika katika tukio ulipuaji wa bomu katika mgahawa wa Vama Traditional uliopo Uzunguni karibu na Mahakama Kuu na Ikulu Ndogo ambako kuna makazi ya Mkuu wa Mkoa Arusha. Bomu hilo lilipuka Julai 7, mwaka huu.

Alisema wakati watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya ulipuaji wa mabomu katika mgahawa huo.

Akizungumzia kuhusu uingizwaji mabomu mkoani Arusha, Mngulu alisema kuna uwezekano mkubwa,
kutokana na kuwa jirani na nchini nyingine.

“Kikubwa kila mtu awe makini na mwenzake ili kumaliza mtandao huu na mikusanyiko yote watu wajihadhari hasa isiyo ya lazima na watuhumiwa hawa wanahusika katika matukio yote yaliyotokea

Olasiti, Arusha High Park Club na Vama, ” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, Mngulu alisema jeshi hilo linamsaka mtu aliyedai kuwa ni mlipuaji maarufu wa mabomu, Yahaya Hassan (35)maarufu kwa jina la Hela .

Kwa mujibu wa Mngulu hadi sasa watuhumiwa 33 wamefikishwa mahakamani, wakiwamo 16
wanaodaiwa kulipua kwa bomu High Park Club, 16 jijini Dar es Salaam na mmoja kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi lililopo Olasiti.
CHANZO: NIPASHE

No comments: