Mgonjwa akiwa hoi hospitalini bila huduma.
UOZO MAHOSPITALINI...
OFM YAIFUNGIA KAZI PALESTINA.
Katika habari hiyo, mapaparazi wa Oparesheni Fichua Maovu
‘OFM’ walitinga Hospitali ya Wilaya ya Kinondoni, Dar, Palestina iliyopo Sinza
na kufanya ‘upelelezi’ kuhusu kuwepo kwa madai kwamba, huduma za sehemu hiyo ya
afya si nzuri.
OFM walifanya kazi mambo yakajulikana na kuanikwa hadharani
ambapo ilitegemewa kuwa, hali ya huduma ingebadilika.
Hata hivyo, juzi kati, wana-OFM watatu walitinga hospitalini
hapo wakifuatilia majibu ya vipimo vya ndugu wa mmoja wao na kukutana na
kisanga kipya kabisa.
Kisanga hicho ambacho kilirekodiwa hatua kwa hatua na
mapaparazi wetu kilimhusu mgonjwa mmoja (jina tunalo) akiteseka na nduguye wa
kike (naye jina tunalo) kupita vyumba vya madaktari kwa lengo la kupata tiba.
....na ndugu zake wakitafuta tiba bila mafanikio.
Mgonjwa huyo
aliyekuwa kwenye kiti cha matairi cha wagonjwa (wheel chair) alionekana kuwa
hoi kwa vile alikuwa hawezi kutembea wala kujieleza sawasawa.
Mawasiliano yote ya OFM na mgonjwa huyo yalifanywa kupitia
ndugu yake ambaye alisema alikatisha shughuli zake za siku hiyo kwa ajili ya
kumpeleka mgonjwa hospitalini hapo.
Malalamiko ya ndugu huyo yalikuwa haya:
“Mimi nashangaa hii hospitali haina chumba cha wagonjwa wa
dharura (emergence), tangu nimefika napata usumbufu wa kufuata taratibu zote
kama wagonjwa wa kawaida.
“Mtu anaumwa hoi kama hivi, badala wampeleke chumba cha dharura, wao wamenipa
kiti chao eti tufuate taratibu. Sasa mtu akizidiwa akifa je?” alilalama ndugu
huyo.
Ndugu huyo alisema kuwa, baada ya kuzurura kwa karibu saa
nzima na mgonjwa wake, daktari mmoja alitokea na kuonesha kutofautiana na
wauguzi ambapo aliwauliza kisa cha kumwacha mgonjwa huyo kwenye baiskeli badala
ya kumpeleka kwa daktari.
“Ilibidi yule dokta, tena Mungu ambariki sana, akamwandikia
nimpeleke kupima malaria, lakini kule nako ilibidi nikae kwenye foleni kwa muda
mrefu.
“Lakini daktari wa maabara naye alimlaumu daktari
aliyemshauri mgonjwa huyo afike hapo akisema ilipaswa mgonjwa wangu apewe
chumba cha mapumziko na kupatiwa huduma akiwa hukohuko badala ya kumsumbua
kwenye foleni zisizo na ulazima,” alisema ndugu huyo.
Alizidi kudai kwamba vipimo vilionesha kwamba mgonjwa hakuwa
na kitu alichoumwa mwilini hivyo aliandikiwa dawa za kupunguza maumivu
(panadol) na kutakiwa kwenda kuzinunua dirishani.
“Lakini pale dirisha la dawa napo nikakutana na tatizo
jingine, mhusika alisoma kadi na kudai shilingi 200 kwa ajili ya malipo ya
panadol.
“Nilitoa noti ya shilingi 5,000, akaikataa akisema eti
hapokei, anapokea shilingi 200 kamili na kama sina nikanunue dawa hiyo nje ya
hospitali,” alisema ndugu huyo huku akisikitika.
Hatua kwa hatua ya matukio hayo, OFM ilikuwa ikipiga picha
kwa kamera ya kisasa kwa ajili ya ushahidi na kumbukumbu.CHANZO GLOBAL PUBLISHERS
No comments:
Post a Comment