Advertisements

Monday, July 28, 2014

Je,unajua jinsi ya kuyafanya maisha yako yawe na shangwe ?

Siku hizi katika kila mji ninakokwenda, nastaajabu kuona nguzo za mabomba zinazochomoza kwenye mapaa ya nyumba na juu yake kumetundikwa vitu vya maumbo mbalimbali.
Ninapojaribu kurudisha kumbukumbu zangu nyuma nagundua kuwa mabadiliko haya yametokea takriban miaka ishirini iliyopita.
Kabla ya hapo, hapakuwa na vitu hivi kwenye mapaa. Kuna mtu mmoja kutoka shamba alimuuliza mtu mmoja, hizo nguzo za mabomba zilizowekwa kwenye mapaa karibuni katika kila nyumba huku mjini zina kazi gani?
Yule mtu akamjibu kuwa zile ni antena za televisheni. Bado yule mtu akaonyesha mashaka kama anaelewa maana ya televisheni. Akamwambia, televisheni ni redio kubwa ambayo badala ya kutoa maneno na muziki tu, yenyewe hutoa pia na picha kama unavyoona kwenye sinema. Yule mtu aliyeuliza swali akamalizia kwa kusema; “kumbe televisheni imeleta sinema nyumbani.
Kama alivyosema mtu kutoka shamba televisheni zimeleta sinema nyumbani, siku hizi watu hawaendi tena katika kumbi za sinema. Nyingi zimefungwa na kutumika kwa shughuli nyingine. Radio, televisheni na video zimeleta shangwe nyumbani. Nakumbuka wakati wa Fainali za Kombe la Dunia la Soka katika kila nyumba kulikuwa na shangwe zilizopambwa kwa shamrashamra na vifijo. Televisheni ikisaidiana na video imekuwa kivutio kinachowafurahisha watu wote katika familia.
Tangu zama za kale, binadamu amekuwa akipenda kuyafanya maisha yake kuwa ya shangwe. Baada ya kumudu kutengeneza zana kufanyia kazi alitengeneza pia ala za muziki alizozitumia kuleta shangwe katika maisha yake.
Katika maisha ya leo, radio, televisheni, video na sinema huleta shangwe, lakini pia kuna vitu vingine vingi vinavyoleta shangwe kwenye maisha ya binadamu. Vitu hivyo ni kama vile michezo, ngoma, muziki, tamthilia na vinginevyo. Licha ya vitu hivi tulivyovitaja, bado binadamu ana wajibu wa kutafuta furaha katika maisha yake.
Ataweza kufanya hivyo kwa kujaribu kufanya mambo mapya, kukutana na watu wapya, kufanya miradi mipya, hata kuwa na mawazo mapya. Furaha itachangamsha mwili na akili na kumfanya ayashangilie maisha yake, kujenga haiba, kuwa na afya nzuri na wakati wote kujisikia kijana.
Hatua ya kwanza kabisa ambayo binadamu anapaswa kuichukua ili kuifungulia milango ya shangwe ni kuepuka hali ile ambayo mimi ningependa kuiita ngumbaru.
Hii ni tabia ya kukataa kubadilika kwa kuendelea kuwa na tabia ya kufuata taratibu na kufanya mambo vile vile siku zote bila mabadiliko au maendeleo yoyote. Kwa utaratibu huu wa maisha, mtu huweza kujikuta amekuwa mtumwa wa tabia na mwenendo wa kufanya mambo.
Kuna watu ambao hudai kuwa kuacha tabia za asili siyo sahihi. Lakini ni vyema kukumbuka kuwa kuna baadhi ya taratibu za mazoea, ambazo pengine zinaweza kutumika katika mambo yanayopaswa kufanywa kila siku. Lakini hazitakuwa na maana kama mtu atakuwa akizifuata kwa sababu hajawahi kufikiria njia bora zaidi za kutekeleza mambo yake. Kubadili tabia ni kuongeza upeo wa shangwe.
Kuna watu waliozoea tabia fulani ambazo hawataki kuziacha,hivyo kuwanyima fursa ya kupanua upeo wa furaha yao.
Mathalan, watu hao wana tabia walizozizoea kama vile kutazama aina fulani tu ya vipindi katika televisheni, aina ya nguo wanazovaa wanapokwenda kazini, jinsi wanavyoandalia wageni wanapowatembelea nyumbani, mpangilio wa aina moja tu wa kazi za nyumbani na mambo mengine mengi ya aina hii. Watu wengine wameganda katika tabia fulani kwa mazoea tu, bila kuwa na sababu za msingi.
Kwa mfano, kuna rafiki yangu mmoja aliyekuwa amezoea kusoma gazeti la zamani lililokuwa likiitwa Mfanyakazi bila kubadilisha. Liliposimama kuchapwa na yeye akaacha kusoma magazeti. Vile vile nakumbuka babu yangu alipokuwa akitoka kazini alipopumzika alikuwa akicheza bao.
Nilimwona akicheza bao tangu nilipopata akili hadi alipofariki. Hadi leo kuna watu wengi wasiotaka kubadilisha tabia zao. Ni vyema wajiulize kwa dhati kwamba kwa nini waendelee kuzing’ang’ania na kwa nini wasingefikiria kuzibadili ili kuziboresha. Au kuziacha na kuchukua tabia nyingine. Kama unataka kuleta shangwe katika maisha yako jaribu taratibu kuanza majaribio ya kufanya vitendo vitakavyokutoa katika utumwa wa mazoea.
Kwa mfano hebu jaribu kusoma magazeti mengine badala ya lile moja ulilolizoea. Wewe na familia yako fanyeni shughuli nyingine wakati wa sikukuu badala ya zile mlizozizoea madhali hamfanyi madhambi au kuvunja sheria
Vitendo tofauti na vile ulivyovizoea huenda vikaleta mabadiliko kidogo, lakini itakuwa hatua muhimu katika kuyafanya maisha yako yakawa na shangwe.
Tafuta fursa ya kukutana na watu tofauti na kujipatia marafiki kwa kujiunga na vikundi kama vile vya kuweka na kukopa vilivyo maarufu sana kama Pride, Saccos, Vicoba na jumuiya nyingine za faraja za kusaidiana katika maafa.
Vilevile kwa wale wacha Mungu kuna vikundi vya kidini vya aina nyingi. Kubali mialiko ya shughuli za jamii na kuwa msitari wa mbele katika kushauri jumuiya au vikundi utakavyojiunga navyo kufanya ziara za mara kwa mara.
Kutafuta mbinu za kuleta shangwe maishani
Ili kuyafanya maisha yako yasiwe ya kuchusha tafuta njia mpya za kufanya mambo ambayo umekuwa ukiyafanya katika namna fulani. Kwa mfano kama umezoea kuwaalika wageni kwenye karamu ya sikukuu nyumbani jaribu kuwaandalia ufukweni au shambani kwako. Licha ya kualika wageni hata wewe na familia yako mnaweza kufanya hivyo.
Unaweza kujitoa katika hali ya ungumbaru kwa kuzibadili hisia na fikra zako kwamba kuna mambo ambayo huwezi kuyafanya. Ukifungua moyo wako na fikira zako zikawa tayari kuthubutu, kuna mambo mengi mapya unayoweza kuyatenda na yatakayoleta shangwe katika maisha yako.
Kwa mfano, unaweza kujifunza mambo mbalimbali mapya kama vile kushona nguo zako na za familia yako, unaweza kujifunza namna ya kupiga picha ukawa unapiga picha za matukio mbalimbali ya familia na kutunza albamu ya historia ya familia yako.
Najua kadri ninavyotoa mifano mingi huenda unaingiwa na wasiwasi kama unaweza kujifunza kufanya walau jambo moja. Lakini kumbuka tulivyojifunza katika makala zangu zilizopita.
Kuhusu tabia ya kuweza na kutoweza. Zungumza na nafsi yako na uiambie kuwa unaweza. Akili yako itamtuma yule asikari wa “ninaweza” na kumweka kando yule askari wa “siwezi”. Ukimtii askari huyo wa akili yako kwa dhati na ukajituma, hapana shaka utaweza.
Tumia fursa ya kujifunza
Njia nyingine ya kujitoa katika maisha ya ngumbaru ni kutafuta ujuzi na uzoefu kutoka kwa watu wengine.
Kwa mfano, unapomwona fundi anafanya kazi fulani unayohisi unaweza kuifanya ili kuleta shangwe katika maisha yako, jitahidi kujifunza kutoka kwake. Uliza maswali mengi yatakayokuongezea maarifa na stadi, hebu tafakari kisa kifuatacho.
Kuna bwana mmoja aliyekuwa akipenda mapambo ya karatasi yanayotumiwa sherehe nyingi hasa za kuzaliwa kwa watoto.
Akaingiwa na ari ya kujua namna ya kuyatengeneza. Katika jitihada zake akabahatika kukutana na mchina aliyewahi kufanya kazi katika kiwanda cha mapambo hayo huko China. Y
ule mchina akamwagizia makaratasi na vifaa vidogo kutoka China na kumfundisha yeye na familia yake namna ya kutengeneza mapambo hayo. Walipojua ikawa ndiyo kazi ya familia kila siku za mapumziko. Wakaipenda na kuifurahia sana shughuli hiyo. Wakawa wanatengeneza mapambo mazuri kama yale yanayotoka nje. Wakawa wakiyauza na kuongeza kipato cha familia.
Shughuli hii ikawaletea mambo matatu makuu; kwanza, iliwatoa katika hali ya kufanya vile vitu walivyozoea na kufanya shughuli mpya. Jambo la pili, kazi hiyo iliwapatia wanafamilia shughuli kadhaa za kufanya ambazo ziliwaletea shangwe katika kaya. Jambo la mwisho ni kwamba wakati wanafamilia wanafurahia ujuzi na stadi mpya, wamekuwa wakijiongezea kipato cha familia.
Hitimisho
Natumaini utagundua kuwa kusoma makala hii ni moja ya matukio ya kusisimua katika maisha yako. Hapana shaka itakuwa imeimarisha haiba yako kwa kuifanya akili yako kuwa macho na makini katika kujipatia maarifa na stadi zitakazofanya maisha yako yawe ya furaha na shangwe.
Sasa kwa kutumia akili yako na kurekebisha tabia yako utaweza kuingiza shangwe katika maisha yako na kuyafanya yasiwe butu kwa kuendeleza mienendo ambayo haishii kutazama hali ya leo tu bali hata miaka mingi baadaye.
Mwananchi

No comments: