ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 1, 2014

Maalim Seif: Jiografia ya Zanzibar kikwazo kupambana na mihadarati

Asema pia utajiri wa wauza unga unakwamisha mapambano kwa  kuwarubuni watendaji
Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema jiografia ya visiwa hivyo ni changamoto kubwa katika kudhibiti uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Maalim Seif alitoa kauli hiyo jana katika mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha ITV, Mikocheni Dar es Salaam.
Maalim Seif ambaye ofisi yake ndiyo inayohusika na udhibiti wa dawa hizo, alisema vita hiyo ni ngumu kutokana na uwezo mkubwa wa wafanyabiashara ambao wanaweza kuwarubuni watendaji kwa fedha nyingi na kuacha kutekeleza wajibu wao.
Alisema ili kupambana na vita  ya dawa hizo, kuna haja ya kuimarisha ushirikiano na uadilifu miongoni mwa watendaji, hasa wale wanaofanya kazi katika viwanja vya ndege, bandarini na vyombo vya ulinzi.
Aonya hujuma
Maalim Seif alionya kuwa vitendo vya hujuma dhidi ya raia na wageni vinavyotokea Zanzibar vinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wake.
Alisema Zanzibar ambayo imekuwa ikitegemea zaidi sekta ya utalii kuendesha uchumi wake na kukuza pato la taifa, imekuwa ikiguswa na matukio hayo ya hujuma ambayo yanaathiri uchumi, ustawi wa jamii na sifa ya ukarimu kwa Zanzibar.
Alisema katika kukabiliana na vitendo hivyo, Serikali inakusudia kutekeleza mpango wake wa kuweka kamera za CCTV katika maeneo muhimu ya utalii likiwamo eneo la Mji Mkongwe, ili kuwabaini kwa urahisi wanaofanya vitendo hivyo.
Majaliwa ya SUK, Katiba
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) itaendelea kuwapo hata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa vile suala hilo ni la kikatiba na limewekewa misingi maalumu.
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, Maalim Seif alisema bado Serikali ina jukumu la kuhakikisha inapatikana ili kuendeleza ustawi wa Taifa na kukidhi mahitaji ya wananchi.
Alisema Serikali imeshatumia fedha nyingi za wananchi na kwamba kushindwa kukamilisha mchakato huo kwa wakati, itakuwa ni hasara kwa Serikali na taifa kwa jumla na kusema Serikali haina budi kutafuta njia mbadala za mazungumzo, kuhakikisha kuwa mchakato huo unaendelea na unafanikiwa kwa masilahi ya Taifa.
Kuhusu zao la karafuu kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar, Maalim Seif alisema Serikali imefanikiwa kudhibiti magendo ya karafuu baada ya kuongeza bei ya zao hilo na kuwashinda wanunuzi wengine wa Afrika Mashariki ambako ilikuwa ikipelekwa. Alisema katika kuhakikisha kuwa ubora wa karafuu za Zanzibar unalindwa, Serikali kupitia Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, itaweka nembo maalumu ili kuzitofautisha na za maeneo mengine.
Mwananchi

No comments: