Advertisements

Saturday, July 12, 2014

MHE. MWIGULU NCHEMBA ALONGA UMOJA WA MATAIFA

 Naibu Waziri wa  Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.  Mwigulu Nchemba ( Mb) akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu masuala ya  Ushirikiano wa Kimaendeleo uliofanyika kwa siku mbili hapa Umoja wa Mataifa. Mhe. Naibu  Waziri  alikuwa mmoja wa wanajopo wanne walioendesha majadiliano hayo. Katika mchango wake, Naibu  Waziri pamoja na mambo mengine amesisitiza  kuwa  Ushirikiano wa Kimaendeleo bado  una mchango mkubwa katika ufanikishaji wa  suala zima la maendeleo endelevu lakini akataka   iwemo mifumo ya ufuatiliaji ambayo  itakuwa jumuishi.
 Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi ambaye alifuatana na  Mhe. Naibu Waziri katika  mkutano huo. Aliyeketi nyuma ya Balozi  Manongi, ni  Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiwano wa Kimataifa, Balozi Celestin Mush na  pembeni ya  Balozi ni msaidizi wa Naibu Waziri.
 Huu ni  Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao kwa takribani wiki mbili umekuwa ukihudhuria na kushiriki mikutano na mijadala  mbalimbali  inayohusu mwelekeo wa  ukamilishwaji wa  malengo ya maendeleo ya milenia ( MDGs), mchakato wa  maandalizi ya ajenda  na malengo mapya ya maendeleo endelevu baada ya 2015 na Ushirikiano wa Kimaendeleo. Mikutano  hiyo   imeandaliwa  na Balaza la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala  ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii  ( ECOSOC)
 Sehemu ya  washiriki waliokuwa wakifuatilia majadiliano hayo na ambapo  baada ya wanajapo kutoka mchango wao walipata fursa ya  kuuliza maswali au kuchangia maoni yao. Mkutano huu wa siku mbili kuhusu Ushirikiano wa Kimaendelea umefanyika  nchi na mwamvuli wa  ECOSOC
Hii ni sehemu nyingine ya wajumbe walioshiriki majadiliano kuhusu Ushirikiano wa Kimaendeleo  wakifuatilia majadiliano hayo 

Na Mwandishi  Maalum
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kuwa Ushirikiano wa  Kimaendeleo   bado ni eneo muhimu katika  kuchagiza kasi ya maendeleo endelevu, kupunguza umaskini na  katika kuzijengea uwezo  na mazingira  ambayo hatimaye yataziwezesha nchi zinazoendelea  kupunguza utegemezi.
Hayo yameelezwa siku ya  Ijumaa na   Naibu Waziri wa Fedha wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba ( Mb), wakati aliposhiriki akiwa mmoja wa wanajopo wanne walioongoza majadiliano kuhusu hatua muhimu za kimataifa  kuelekea 2015 ya  mifumo ya ufuatiliaji na uwajibikaji kwa ushirikiano wa  kimaendelea.

Ajenda hii ilikuwa kati ya  ajenda kadhaa, ambazo  mawaziri, wabunge, wasomi, wafafiti na wajumbe  kutoka  Taasisi  zisizo za kiserikali wamekuwa wakizijadili na kubadilishana  mawazo katika  mkutano wao wa siku mbili  kuhusu Ushirikiano wa Kimaendeleo ( DCF). Mkutano huo  ambao hufanyika kila  badaa   ya miaka  miwili umefanyika chini ya  mwamvuli wa  Baraza   la Umoja wa Mataifa linalohusika na  Masuala ya Uchumi na Maendeleo ya Jamii ( ECOSOC). 
Akitilia  mkazo kuhusu eneo hilo la ushirikiano wa kimaendeleo, Naibu Waziri amewaeleza washiriki wa majadiliano hayo kuwa uanzishwaji  upya wa ushirikiano  kwajili ya  maendeleo baada ya 2015 unatakiwa kuendelezwa kama  ulivyoainishwa katika lengo la nane la MDGs ambalo  linasisitiza kuhusu   ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo.
Akaongeza kuwa   ushirikiano huo lazima pia ujengekee katika  mazingira ya kuaminiana, kuwajibika na kuwa na mifumo ya  ufuatiliaji.
Akizungumzia kuhusu misaada ya   maendeleo   ( ODA) Naibu Waziri wa Fedha, amesema  ingawa misaada hiyo ya maendeleo bado ni muhimu hususani kwa nchi zinazoendelea lakini  mchango wake si mkubwa sana  katika  eneo la maendeleo kwa ujumla wake.
Akabainisha  pia kuwa pamoja na  nafasi yake katika ushirikiano wa kimaendeleo upatikanaji wa  ODA umekuwa hautabiliki au kupatikana kwa wakati, na kikubwa zaidi hakuna mifumo ya  kuwawajibisha watoaji wa ahadi hizo pale wanapokwenda kunyume na ahadi zao.
Na kwa sababu  hiyo akasema  ushirikiano mpya wa kimaendeleo lazima pia uimarishe pamoja na  mambo mengine uwajibikaji wa  washirika wa maendeleo na  uanzishwaji wa vyanzo vipya vya ugharimiaji wa maendeleo vitakayoziba pengo la misaada ya  maendeleo kutoka nje.
Akataja  maeneo ambayo  yanaweza  kuzalisha  mapato mapya ya ndani  kuwa ni  pamoja na  ukusanyaji wa kodi   na udhibiti wa fedha  chafu.Na kusisitiza kwamba,   ni kwa uimarishaji wa  vyanzo hivyo vya mapato, udhibiti wake, uwajibikaji pamoja na ushirikiano wa kimaendeleo ndipo mataifa yanayoendelea yataweza kupunguza utegemezi wa misaada kutoka nje.
Kuhusu eneo la ufuatiliaji na uwajibikaji,   Naibu Waziri amesema,  Tanzania  siyo tu  inafanya vema katika eneo hilo lakini pia  imejiwekea  sera, taratibu  na mifumo inayosimamia utawala bora  na uwajibikaji.
Akatoa mfano   uamuzi wa Serikali wa  kuiwasilisha Bungeni  taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa   Hesabu za Serikali kama eneo mojawapo la uwajibikaji.
Aidha akasema, kama hiyo haitoshi Tanzania,  ni kati ya nchi ambazo kwa hiari yake iliamua kujiunga na Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi ( OGP) kama sehemu ya uwajibikaji .
Katika   majadiliano hayo, Naibu  Waziri wa Fedha amesisitiza pia haja na umuhimu wa nchi  kumiliki na kuendesha mambo yake yenyewe ikiwamo miradi ya maendeleo.

No comments: