ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 2, 2014

Ndulu: BoT haiwezi kuzuia mabilioni kutoroshwa


“Pia masuala ya fedha hayafanywi na BoT moja kwa moja, benki zilizopo nchini ndizo zinashughulikia haya mambo, sisi ni wasimamizi tu, ndiyo maana hata wewe ukitaka kutuma fedha zako nje huji BoT, unakwenda kwenye benki yoyote na unapewa taratibu ukizifuata unatuma fedha zako.” Profesa Benno Ndulu

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT), imesema haiwezi kuzuia utoroshaji wa mabilioni ya fedha ambayo hufichwa nje ya nchi na baadhi ya watu wakiwamo waliowahi kuwa watumishi wa umma.
Gavana wa benki hiyo, Profesa Benno Ndulu amesema utoroshaji wa fedha hufanywa kwa mbinu ambazo ziko nje ya mfumo rasmi wa sekta ya fedha, hivyo siyo rahisi kwa BoT kuwadhibiti wahusika.
Kauli ya Profesa Ndulu imekuja wakati Tanzania ikitajwa kuwa moja ya nchi ambazo baadhi ya vigogo wake wameficha fedha nje ya nchi, hususan Uswisi na BoT ikielezwa kuwa moja ya taasisi zinazopaswa kufahamu Watanzania wenye fedha nje ya nchi.
Balozi wa Uswisi nchini, Olive Chave katika mahojiano na gazeti hili siku chache zilizopita alisema: “Siyo tu kwamba Serikali ya Uswisi ndiyo inajua kila kitu kuhusu fedha hizo, Benki Kuu ya Tanzania ndiyo inayoidhinisha fedha kwenda kwenye akaunti zilizopo nje ya nchi.
“Kwa mfano, kuna kampuni ya Kitanzania inayofanya biashara ya mitambo kutoka Uswisi, hapa sisi hatuwezi kujua kama pesa hizi ni haramu au la, maana kitendo cha fedha kuwa Uswisi siyo kigezo pekee kwamba ni haramu.”
Balozi Chove alisema fedha hasa za kununua bidhaa zimekuwa zikiidhinishwa na benki kwa malipo halali, kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamefungua akaunti katika benki za nchi hiyo.
Hata hivyo, hakuwa tayari kutaja kampuni zinazonunua bidhaa zake Uswisi, lakini akasema watu kama hao hawawezi kufanya biashara kubwa bila sekta ya benki kuwa na taarifa. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa baadhi ya Watanzania walioficha fedha nje ya nchi, hutumia kampuni walizozianzisha huko (off shore companies) ambazo huzitumia kutorosha fedha kwa kukwepa kodi.
Ripoti ya Mei, mwaka huu ya Taasisi ya Global Financial Integrity, inaonyesha kuwapo ukwepaji mkubwa wa kodi nchini ambao umekuwa ukiikosesha Tanzania Sh409 bilioni kila mwaka, huku Uswisi na Singapore zikitajwa kuwa nchi za maficho ya fedha hizo.
Profesa Ndulu alisema BoT haiwezi kuzuia uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwani inabanwa na Ibara ya 8 ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambayo inazuia malipo ya fedha kwa shughuli za biashara za kawaida.
“Sisi (Tanzania) ni signatory (tumesaini) wa Ibara ya Nane ya Kanuni za IMF ambayo inakataza kuzuia malipo yoyote ya current account (akaunti ya amana), kwa hiyo mtu akitaka kununua bidhaa na nyaraka zipo, siyo kazi ya BoT kumzuia.
Sehemu ya pili ya Kanuni ya 8 ya IMF inazielekeza nchi zilizosaini makubaliano hayo kutoweka kizuizi chochote kwenye malipo ya amana. “Bila idhini ya shirika (IMF), hakuna mwanachama (nchi) atakayeruhusiwa kuweka vikwazo dhidi ya malipo ya amana yanayotakiwa kufanywa katika mfumo wa biashara ya kimataifa.”
Profesa Ndulu alisema malipo yanayohusu akaunti za mitaji (capital account) ndiyo yanayohitaji idhini ya BoT hasa yanapozidi Dola za Marekani 10,000, lakini hata katika eneo hilo ni vigumu kudhibiti watu wenye nia mbaya.
“Mtu au kampuni ikiwa inaagiza bidhaa kama mafuta hawezi kutumia Sh1 milioni, yanaweza kuwa ni mafuta ya Dola 5 milioni, hapo sisi (BoT) tunalazimika kutoa kibali. Hata hivyo, haisaidii sana maana utoroshaji wa fedha una njia nyingi kama mlivyosikia kwenye ile Ripoti ya Global Financial Intergrity,” alisema.
Utoroshaji fedha
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwapo na udanganyifu mwingi katika uagizaji wa mafuta unaofanywa na baadhi ya kampuni za uchimbaji wa madini na uagizaji wa bidhaa zilizowekeza chini ya mpango wa kanda maalumu za kiuchumi (Export Processing Zones – EPZ), kwa kampuni husika kuongeza thamani za bidhaa zinazoagizwa kinyume na uhalisia.
“Wachumi wetu wamebaini asilimia 67 ya udanganyifu unaofanywa katika nyaraka za mauzo na uagizaji wa bidhaa, unazihusisha Uswisi na Singapore, lakini ukichunguza zaidi unabaini kwamba udanganyifu kwenye nyaraka za kuagiza mafuta kwa zaidi ya asilimia 25 zilihusu uagizaji wa mafuta kutoka Uswisi pekee,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo nakuongeza:
“Kwa kufanya hivyo, kampuni nyingi zimeweza kupunguza kiwango cha mapato yake yanayotozwa kodi (kwa kuongeza gharama za mafuta kama sehemu ya matumizi ya kibiashara), hivyo kukwepa kodi nyingine kama vile ya kampuni (corporate tax) nchini Tanzania.”
Taarifa za 2011 kutoka Uswisi zilizoonyesha kuwapo kwa Sh327.9 bilioni zilizofichwa kwenye benki za nchi hiyo, lakini ripoti mpya ya 2012 inaonyesha kuwa fedha hizo zimepungua hadi Sh291.96 bilioni.
Tayari Tanzania imeomba msaada kwa Taasisi ya International Centre for Asset Recovery – ICAR ya Uswisi kuchunguza kesi tano zinazohusu watu na taasisi zinazotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo.
Mwananchi

No comments: