ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 2, 2014

Mawaziri sita kuwekwa kiti moto kuhusu BRN

Mawaziri Sita watawekwa kiti moto Septemba, mwaka huu watakapokuwa wakiwasilisha utekelezaji wa mwaka mmoja wa mpango wa Matokeo Makubwa sasa (BRN) katika wizara zao.

Mpango huo ulizinduliwa Juni, mwaka jana na Rais Jakaya Kikwete, ukiwa na lengo la kufikia matokeo yanayohitajika kwenye sekta sita nchini zikiwamo Elimu ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambayo inaongozwa na Dk.Shukuru Kawambwa.

Wizara zingine ni Nishati na Madini (Prof. Sospeter Muhongo); Wizara ya Fedha (Saada Mkuya); Kilimo, Chakula na Ushirika (Christopher Chiza); Uchukuzi (Dk. Harisson Mwakyembe) na Wizara ya Maji (Prof. Jumanne Maghembe).

Meneja Uhusiano wa President Delivery Bureau (PDB), Anastazia Rugaba, aliyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa kinachoendelea katika shule nchini jijini Dar es Salaam jana.

Alisema kila Waziri ataelezea utekelezaji wa BRN kwa muda wa mwaka mmoja, hivyo kutokana na utashi wa Rais na wananchi kwa ujumla wataangalia uwajibikaji wa viongozi kwa mujibu wa viapo vyao.

“Kwa sasa PDB tupo kwenye maandalizi ya kuandaa taarifa mbalimbali, hivyo taarifa hizo zitakuwa wazi kwa kila Mtanzania kupitia vyombo vya habari,” alisema.

Rugaba alisema kuwa PDB imeanzishwa kwa lengo la kufanyakazi yake kusimamia BRN, hivyo ni wajibu wao ni kuandaa mahojiano maalumu ili wananchi wafahamu umuhimu wa BRN.

Aidha, alilipongeza Shirika lisilo la Kiserikali la Twaweza kufanya tafiti mbalimbali na kuijulisha Serikali, ukiwamo utafiti uliobainisha kuwa asilimia 16 ya wananchi wamekuwa na uelewa wa BRN.

“Serikali imedhamiria kwa dhati kuifanya nchi ifikie uchumi wa kati ifikapo 2025, huu ni msukumo kutoka nchi ya Malaysia ambao ni wazoefu kwenye mpango wa BRN,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

No comments: