ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 1, 2014

Ngasa arejea leo akisononeka

Mshambuliaji wa Yanga na timu ya Taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngasa

Mshambuliaji wa Yanga na timu ya Taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngasa, anatarajiwa kurejea nchini leo akitokea Afrika Kusini huku akisema kwamba ameumia kukosa kusajiliwa na klabu ya Free State Stars baada ya kufuzu majaribio.

Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu kutoka Johannesburg, Ngasa, alisema kwamba anarejea nchini kuitumikia Yanga kwa uaminifu lakini hajakata tamaa ya kutimiza ndoto zake za kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania.

Ngasa alisema kwamba kwa sasa ana maamuzi tofauti na anaamini kuwa bado ana nafasi ya kupata timu nje ya nchi atakapomaliza mkataba wake na Yanga mwakani.

"Imeniuma lakini sina jinsi, narudi Jumanne (leo)," Ngasa alisema kwa kifupi.Hata hivyo, alisema bado hajajua ni lini ataondoka nchini kuelekea Botswana kujiunga na kikosi cha Stars ambacho kimeweka kambi jijini Gaborone kujiandaa na mechi yake dhidi ya Msumbiji itakayofanyika Julai 20 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Ngasa alisema kuwa Free State ilikuwa tayari kutoa Dola za Marekani 80,000 (sawa na Sh. Milioni 130 za Tanzania) lakini Yanga ilikataa na kuwaeleza viongozi wa klabu hiyo mpya wanahitaji kiasi cha Dola za Marekani 150,000 ili wamruhusu nyota huyo wa zamani wa Kagera Sugar, Azam na Simba kuichezea timu hiyo.

Nyota huyo amebakiza mkataba wa mwaka mmoja wa kuitumikia Yanga iliyomsajili akitokea Simba alikochezea kwa mkopo na endapo angefanikiwa kutua Free State angekutana na kocha wa zamani wa timu hiyo ya Jangwani, Mbelgiji Tom Saintfiet.

Desemba 2012 Ngasa alikaribia kusajiliwa na El Mereikh ya Sudan lakini mshambuliaji huyo alikataa ofa aliyopewa na kurejea nchini akitokea Kampala, Uganda alipokuwa na kikosi cha Bara (Kilimanjaro Stars) na kujiunga na Yanga.

 
SOURCE: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Wakati umefika watu inabidi kukubali ukweli kuwa Ngassa ni msanii tu na wala si mchezaji wa kiukweli. Hii ni timu ya tatu sasa kujaribishia na kila timu anakataliwa kwa kuwa na kiwango kidogo na si cha kimataifa. Hakuna kocha mwenye akili timamu akampanga Ngassa, yule ni mchawi tu na uchawi gauna tija ndani ya soka. Mi nimefurahi hajapata namba kwani analihaibisha taifa kwa uzoba wake. Karne ya na ni mwaka 2014 yeye anafikiri kuroga ndiyo dili.

Anonymous said...

waongea pumba wewe wahapo juu