Advertisements

Thursday, July 24, 2014

SHERIA: Watu sita wapandishwa kizimbani kwa ugaidi

WATUHUMIWA WA UGAIDI: Watuhumiwa wa mabomu jijini Arusha wakirudishwa mahabusu baada ya kusomewa mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha jana kwa madai ya kujihusisha na ugaidi. Picha na Filbert Rweyemamu

Arusha/Dar. Watuhumiwa sita wa matukio ya ugaidi katika Jiji la Arusha jana walipandishwa kizimbani wakiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kujibu tuhuma za kufanya matendo ya kigaidi.
Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani saa 7:20 mchana, wakisindikizwa na magari matatu ya polisi wenye silaha  na gari la mbele likipiga king’ora.
Waendesha mashtaka wa Serikali, Augustino Komba na Felix Kwatukia, kwa kupokezana walimweleza Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Rose Ngoka kuwa watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka manne tofauti ya kujihusisha na matukio ya ugaidi katika Jiji la Arusha kati ya Februari na Julai mwaka huu.
Komba aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni, Shaaban Mmasa (26), mlinzi wa Mgahawa wa Vama, Athuman Mmasa (38) ambaye ni mlinzi pia, mkazi wa eneo la Unga Ltd, Mohamed Salehe (30) mkazi wa Unga Ltd na Jafari Lema (38) ambaye ni mwalimu.
Watuhumiwa wengine ni Abdul Humud (30) ambaye ni wakala wa mabasi, mkazi wa Murieti na wa sita ni Said Temba (42), mfanyabiashara  mkazi wa eneo la Sinoni eneo la Unga Ltd Arusha.
Komba alisema katika shtaka la kwanza, washtakiwa wa kwanza hadi wa nne wanatuhumiwa  kula njama za kufanya matukio ya ugaidi kinyume na Kifungu cha 24 (2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi namba 21 ya mwaka 2002.
Katika shtaka hili washtakiwa wanatuhumiwa kufanya matukio ya kigaidi kati ya Februari na Julai katika Mgahawa wa Vama.
Katika kosa la pili, washtakiwa wote sita, wanatuhumiwa kutenda makosa ya kigaidi kinyume na Kifungu cha 4(2)(c)(i), vifungu vya 3(a),(b),(c) na (e) na 27(a),(c) na (d) vya Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002 kwa kupanga njama ya kufanya uhalifu katika Mgahawa wa Vama eneo la Uzunguni na kuwasababishia madhara watu wanane.
Katika kosa la tatu, mtuhumiwa wa pili, Athuman Mmasa na wa nne, Jafari Lema, wanatuhumiwa kumiliki mabomu kinyume cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi namba 21 ya mwaka 2002, Kifungu cha 20(c) ambapo wanatuhumiwa kuwa kati ya Julai 5 na 7 mwaka huu walikuwa na bomu la F1 ambalo walimpatia Mohamed.
Katika shtaka la nne, Lema, Mohamed na Temba wanatuhumiwa kuwa kati ya Aprili 2013 na Julai mwaka huu kuwawezesha watu kifedha kufanya ugaidi katika Mgahawa wa Vama uliopo eneo la Mianzini. Baada ya watuhumiwa hao kusomewa mashtaka, Hakimu Ngoka alisema hawapaswi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu Ngoka aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 6, mwaka huu kwa kuwa upelelezi haujakamilika na watuhumiwa walirudishwa mahabusu.
Kesi ugaidi Dar
Wakati huohuo; upande wa mashtaka katika kesi ya ugaidi inayowakabili washtakiwa 16 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam umeiomba mahakama muda zaidi wa kukamilisha upelelezi.
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Alhamisi iliyopita na kusomewa mashtaka ya kula njama kutenda makosa ya kuwaingiza watu nchini kushiriki katika vitendo ya ugaidi pamoja na kusaidia na kuwezesha kufanyika vitendo hivyo.
Baada ya kumaliza kuwasomea mashtaka hayo, Jamhuri iliyowakilishwa na jopo la mawakili wanne, iliomba kesi hiyo itajwe jana ikidai kuwa itakuwa na maombi maalumu.
Hata hivyo, kesi hiyo ilipotajwa jana, hakuna maombi maalumu yaliyotolewa na badala yake, Wakili wa Serikali, Peter Njike aliieleza tu mahakama kuwa upelelezi haujakamilika na kuomba muda zaidi wa kukamilisha upelelezi.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

mfumo kristo at work

Anonymous said...

Wacha ushenzi wewe anonymous hapo juu 2:38pm,Wakati robo za binaadamu wasiokuwa na hatia zinapotea kwa ajili ya wajinga hawa ni vigumu kuamini kwa walichokifanya bado wanaweza wakapata sympathizes wajinga kama wewe kwa kuaanza kuiingiza udini.