
Sumaye aliyasema hayo wakati akihutubia mkutano mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, uliofanyika jana jijini Arusha. Ujumbe wake ulijikita katika uwapo wa umoja, amani na utulivu.
Pamoja na mambo mengine, Sumaye alitumia hafla hiyo kumpongeza, Askofu Mteule, Mchungaji Solomon Massangwa, kwa kuchaguliwa kuiongoza dayosisi hiyo kujaza nafasi iliyoachwa wazi kutokana na kifo cha Askofu Thomas Laiser.
Akizungumzia vurugu zinazohusiana na masuala ya siasa, Sumaye alisema uvunjifu wa amani unatokea pale upande mmoja unapohisi kudhulumiwa au kuonewa katika maamuzi ya kisiasa hasa nyakati za kampeni, upigaji kura na wizi wa kura.
“Wakati mwingine hali hii hutokea kwa upande moja kukataa kushindwa hata kama wameshindwa kwa halali.
Jambo hili la kisiasa limeleta fujo nyingi hasa katika nchi nyingi za Kiafrika na kusababisha umwagaji wa damu,” alisema.
“Ni lazima shughuli zetu za siasa zifuate sheria na taratibu zilizowekwa kwa uwazi bila kutiliwa shaka na upande wowote. Haki ni lazima isimamiwe kikamilifu nyakati zote za kampeni hadi upigaji wa kura, kuhesabu kura na hata kutangaza matokeo,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, Tanzania inahitaji kuendeleza umoja miongoni mwa raia wake, ili kuimarisha utulivu na kuvunja migawanyiko nchini.
Kwa mujibu wa Sumaye, nchi zenye uvunjivu wa amani kiasi cha kuwapo vita vya wenyewe kwa wenyewe, zimefikia hali hiyo kutokana na kuwapo kundi linaloamini kudhulumiwa haki zao na wakati mwingine ni kutokana na chuki iliyojengeka kati yao.
UDINI
Sumaye alisema chuki zinazoelekezwa kwenye imani za kidini zinapaswa kukemewa kutokana kuwa na madhara yanayoiathiri jamii nzima.
Alisema hivi sasa kuna chokochoko zenye sura ya imani zinazochangia kufifisha upendo na uzalendo, hivyo kuathiri umoja uliopo.
“Tukiwa wamoja hili halina nafasi kwa sababu hakuna dini inayofundisha chuki kwa binadamu mwenzake,” alisema.
Alisema viongozi wa dini wanapaswa kuwasimamia waumini wao, ili nchi isije ikakumbwa na balaa la vurugu za kidini, jambo ambalo ni la hatari na lisilopaswa kutokea.
TOFAUTI ZA KIPATO
Sumaye alikemea pia kushamiri kwa tofauti kubwa ya kipato baina ya makundi tofauti, hasa kati ya matajiri wachache na wenye madaraka kwa upande mmoja na maskini walio wengi kwa upande wa pili.
Alisema tofauti hizo zinasababishwa na mfumo mbaya wa uchumi na ubinafsi uliokithiri ama usiojali binadamu wengine.
“Hali hii ni ya hatari kwa amani na utulivu kwa sababu walio wengi hawatavumilia kuwaona wachache wakiishi katika anasa za kutisha wakati wao hawamudu hata mahitaji ya lazima kama vile chakula, matibabu na maji,” alisema.
Alisema hali kama hiyo imesababisha vurugu katika nchi nyingi na kuathiri amani na utulivu na kwamba hata hapa nchini, kuna tofauti kubwa ya kipato kwa makundi hayo hivyo inahitajika kudhibitiwa kwa haraka.
Sumaye alisema kutokana na hali hiyo, ipo haja ya kuwekeza na kutekeleza mipango inayochochea uzalendo wa kuipenda nchi na watu wake.
Waziri Mkuu mstaafu huyo, alisema kukosekana kwa umoja ni miongoni mwa sababu zilizofifisha maendeleo katika nchi nyingi za Bara la Afrika.
VIONGOZI WA DINI
Alisema viongozi wa dini wana kazi kubwa katika wakati huu kuliko ilivyokuwa zaidi ya muongo uliopita.
Alisema ukosefu wa maadili umekuwa chanzo cha kuibuka kwa matatizo kadhaa ya kijamii na kuhoji, “Je, katika upungufu huu wa maadili, viongozi wa kiroho mna nafasi ipi ya kudhibiti mambo haya?”
Sumaye alisema viongozi wa serikali, dini na asasi nyingine za kijamii wana jukumu la kuuongoza umma, badala ya kuliacha (jukumu hilo) kwa kikundi kimoja.
AMANI KWA MAKANISA
Alisema umoja unatakiwa kuwapo hata kwenye madhehebu ya dini, ambako waumini wanatakiwa kumheshimu na kumtii kiongozi anayechaguliwa.
“Kama hamtakuwa na umoja maana yake hapatakuwa na upendo baina yenu, amani na utulivu vitaathirika na hatimaye maendeleo ya kimwili na ya kiroho yatakuwa ni ndoto za alinacha,” alisema.
Aliongeza: “Siku hizi hutokezea hata katika chaguzi za nafasi za uongozi makanisani watu kujitenga na viongozi waliochaguliwa eti kwa sababu tu huyo aliyechaguliwa hakuwa chaguo lake, hali ambayo huwafanya viongozi kuongoza kwa shida sana.”
CHANZO: NIPASHE
2 comments:
Alivyo kuwa waziri mkuu, hakuwahi kusema kama CCM walimwibia kura Mrema....leo hii anayasema kwasababu anajua siri za viongozi wetu.
Kila binadamu anahaki yakuwa na dreams na huyu mzee anaonyesha njozi zake.
Post a Comment