ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 13, 2014

Tendwa awapa siri wapinzani

Na Fidelis Butahe na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Dar es Salaam. Tangu mwaka 1995 vyama vya upinzani nchini vimekuwa vikisimamisha wagombea katika Uchaguzi Mkuu na kuambulia patupu mbele ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini sasa vimepewa somo la kushinda katika uchaguzi huo na aliyekuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.
Tendwa (pichani) ambaye alistaafu nafasi hiyo Agosti mwaka jana alisema siri ya ushindi huo ni kubadilishwa kwa Sheria ya Vyama vya Siasa, ili kuruhusu vyama hivyo kuungana na kusimamisha mgombea mmoja, kama ilivyo katika nchi za Kenya, Lesotho na Jamhuri ya Kidemokrasi Kongo (DRC).
Msajili huyo aliyetumikia nafasi hiyo kwa miaka 13, aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake, Dar es Salaam.
Anasema wakati anaondoka katika wadhifa wa Msajili aliacha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ya vyama vya siasa ofisini kwake, ambao unapendekeza vyama vya siasa vinaweza kuungana wakati wa uchaguzi kusimamisha mgombea wa urais kama ilivyo kwa nchi ya Kenya.
“Mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hiyo niliyaacha ofisini na yanatakiwa kwenda katika sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Kamati za Makatibu Wakuu, Baraza la Mawaziri ambalo inaweza kutoa maelezo kwenye kamati yake ndogo ambayo inashughulikia Masuala ya kisheria,” alisema Tendwa.
Alisema kama mapendekezo hayo yakipitishwa na kuwa sheria, basi hiyo itakuwa njia nyeupe kwa wapinzani kuingia Ikulu kama wataungana. Msajili huyo msataafu alisema hivi sasa jambo hilo linatakiwa kupigiwa debe na ofisi ya Mjasili wa Vyama vya Siasa, ili lifanyiwe marekebisho.
Tendwa anasema katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010, wapinzani wangeweza kushinda kama wangeunganisha nguvu kwa kusimamisha mgombea mmoja wa urais, huku akitolea mfano jinsi CCM kilivyoporomoka katika kura za urais kutoka asilimia 80 hadi 60.
“Mwaka 2010 niliwaambia CCM ila walinitukana. Niliwaeleza wataporomoka kutoka asilimia 82.5 za mwaka 2005 hadi asilimia 60 na wasipoangalia 59. Mwaka 2010 kama wapinzani wangekazana na kuungana ni wazi kuwa wangeshinda ” alisema Tendwa na kuongeza;
“Nadhani nilijadiliwa ndani ya vikao wakati huo Katibu Mkuu wa CCM akiwa Yusuph Makamba. Niliona wazi kuwa walikuwa hawaendi vizuri, kwani walibweteka na kulewa na ushindi wa kishindo wa mwaka 2005. Ila kwa sasa CCM wanakuja vizuri.”
Aina ya muungano
Tendwa alisema ili vyama hivyo viweze kuungana Sheria ya Vyama vya Siasa inatakiwa kurekebishwa ili kuviwezesha kusimamisha mgombea mmoja.

Alisema kwa mujibu wa sheria iliyopo sasa, vyama vya siasa vinaweza kumuunga mkono mgombea wa chama fulani, lakini haviwezi kuwa na umoja utakaopewa jina, kisha kusimamisha mgombea mmoja huku kila chama kikibaki na utambulisho wake.
Tendwa alisema kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulianzishwa na vyama vya upinzani, hivi sasa hawawezi kuutumia kusimamisha mgombea mmoja katika Uchaguzi Mkuu.
“Huu muungano wa Ukawa siyo wa kisheria. Hawawezi kuweka mgombea mmoja wa urais na kumuita mgombea wa Ukawa, kwani sheria haisemi hivyo,” alisema na kuongeza;
Alisema huko nyuma jambo hilo la kuunganisha vyama lilipopendekezwa wadau waliliunga mkono bila kufahamu kuwa muungano uliopendekezwa siyo ule unaoweza kuvifanya vyama vya siasa kusimamisha mgombea mmoja na kuwa na jina moja.
“Yalikuwa ni mapendekezo ya kuunganisha vyama (merge) na siyo muungano wa vyama (alliance) ambao vyama vinaweza kuungana na kujiita jina moja, kisha kusimamisha mgombea mmoja kwa jina hilo, ila kila chama kinabaki na utambulisho wake,” alisema.

Mfano wa muungano huo
Tendwa alisema Kenya vyama viliungana na kuzaliwa umoja uliopewa jina la Jubilee na kusimamisha mgombea mmoja, Uhuru Kenyatta aliibuka mshindi kupitia umoja huo.
Tendwa alisema katika nchi hiyo vyama vingine viliungana na kuzaliwa umoja uliopewa jina la Cord, lakini ulishindwa katika Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo na Umoja wa Jubilee kutokana na kukosa uongozi imara na demokrasia zaidi.
Pia alitolea mfano wa Lesotho, kwamba ina watu milioni 1.3, lakini kuna vyama vya siasa 29 ambavyo viliungana na kuzaliwa umoja wa miungano minne vya vyama hivyo.
Alisema Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) hadi mwaka juzi kulikuwa na vyama vya siasa 428 na kwamba viliungana na kuzaliwa miungano minne ya vyama hivyo katika Uchaguzi Mkuu waliogombea urais walikuwa watu wanane tu.
Angalizo
Alisema utaratibu huo ukianzishwa ni lazima upatikane ufumbuzi kuhusu ruzuku:, “Lazima tujue ruzuku itakwenda vipi, inakwenda katika umoja au chama kupitia mbunge. Kenya wanachofanya ni asilimia fulani kwenda katika umoja na inayobaki inaingia kwenye chama kupitia mbunge.”
Tatizo la vyama vya upinzani
Tendwa alisema tatizo kubwa linalovikabili vyama vya upinzani ni ubinafsi, kukosa utulivu wa kisiasa jambo ambalo linazua migogoro kila uchwao.
“Mfano Chama cha Wananchi (CUF) umeibuka mgogoro na baadhi ya wanachama wakajiengua na kuanzisha chama kingine cha Alliance for Democratic Change (ADC). Baadaye walioanzisha chama hicho walizozana na mmoja wa viongozi wake akaenda katika chama kingine cha Alliance for Change and Transparency (ACT),” alisema.

No comments: