ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 13, 2014

Kashfa zamwelemea Mkurugenzi Muhimbili

Mkurugenzi Mtendaji Dk.Marina Njelekela

Kashfa za ufujaji na matumizi mabaya ya fedha zinazomhusu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuibuliwa, wakati tanuru la kuchomea taka likiwa halijapatiwa ufumbuzi.

Licha ya hospitali hiyo kuwa taabani kifedha, kukosa vitendea kazi na wataalamu, Mkurugenzi Mtendaji Dk.Marina Njelekela, anatuhumiwa kufuja fedha kwa kujilipa posho nyingi kinyume cha sheria.

Vyanzo vya kuaminika ndani ya hospitali hiyo, vimeiambia NIPASHE Jumapili kuwa, licha ya Njelekela, kununua gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 kwa Sh. milioni 207, fedha zilizolipwa kwa kampuni ya Toyota Tanzania kupitia hundi namba 117781 ya PV P3-13-001697 ya Mei mwaka huu.

“Tangu Mkurugenzi huyu ameingia Muhimbili, amekuwa akikiuka kanuni za fedha, baada ya kuona watu wanamshtukia anamtumia katibu muhtasi wake kuchukua fedha za posho za safari anazozipanga mwenyewe akijua kuwa hazina tija,” kilidokeza chanzo kimoja.

Baadhi ya fedha zilizodaiwa kuchukuliwa na mkurugenzi huyo ni kupitia hundi yenye namba 97543 (PV-13-000100) ambayo Njelekela alijilipa Dola 5,355 (sawa na Sh. milioni 8.8) na 3,780 (Sh. milioni 6.2) kwa wakati mmoja.

Chanzo hicho kilieeleza kuwa, wakati mkurugenzi huyo akidaiwa kufanya safari zisizo na tija, hospitali ina deni la zaidi ya Sh. bilioni 12 linayojumuisha madeni ya wazabuni na stahiki za wafanyakazi hasa madaktari na wauguzi.

Aidha vyanzo vimeeleza kuwa baadhi ya safari alizofanya zilistahili kufanywa na madaktari na si mkurugenzi.

“Huu ni ufisadi na ubinafsi, mfano mwaka huu amekwenda kwenye mkutano wa kimataifa wa taasisi ya watoto akalipwa Dola za kutosha, je yeye ni daktari wa watoto, basi hata angekuwa mjumbe wa chama cha madaktari wa watoto tusingelalalamika lakini hayuko kote,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Hakuishia hapo alikwenda mkutano wa kimataifa wa chama cha madaktari wa figo na ini, akavuta dola za kutosha tena , hivi yeye ni daktari wa figo na ini? Huku ni kuchukua majukumu ya wengine na kuacha kazi ya ukurugenzi…”kililalamika.

Tangu aingie Muhimbili amefanya safari zaidi ya 34 kwa mujibu wa vyanzo vya habari ndani ya Idara ya Fedha ya hospitali hiyo ambavyo vilihoji imeleta matunda gani? Wapashaji wetu wakizungumzia zaidi ubadhirifu walisema Dk.Njelekela amekuwa akijilipa posho za kujikimu ambazo wengine wakisafiri wananyimwa.

“Februari 17, mwaka huu kupitia hundi Na. 97523 alijilipa Dola 2100 (sawa na Shilingi milioni 3.5) fedha za safari iliyoanza Februari 28 hadi Machi 3 mwaka huu ,” kilieleza chanzo hicho.

Pia kilibainisha kuwa wafanyakazi hawajalipwa fedha za nauli kutoka Agosti mwaka jana hadi sasa na wanadai Sh. milioni 247.3

Chanzo kingine kilisema watumishi wa Muhimbili kwa miaka miwili hawajalipwa posho za wafanyakazi zikiwamo mapato ya Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF), yanayotokana na kutoa huduma kwa wateja wa mfuko huo.

“Wakati deni hilo kubwa na madai ya wafanyakazi yakikwama kulipwa hospitali ina changamoto lukuki huwezi kuamini haina mita za kupima kiwango cha oksejeni anayopewa mgonjwa anayepumua kwa mashine (oxygen gauge) ambazo ni muhimu kwa wodi ya watoto wanaolazwa kila mara kwa kushindwa kupumua.

Chanzo kingine kilisema wagonjwa hujinunulia dripu na glovu na hakuna mashuka wala vyandarua vya kutosha mawodini.

Gazeti hili liliwasiliana na Dk Njelekela ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma hizo lakini alijibu kwa jeuri kuwa anayetakiwa kuzungumzia madai hayo ni Afisa Uhusiano wa hospitali na sisi yeye.

Hata hivyo, mwandishi alipomwambia kuwa tayari amewasiliana na ofisa huyo na kujibiwa kuwa yupo Nairobi, Kenya na asingeweza kushughulikia habari hizo, Mkurugenzi Njelekela alisisitiza aendelee kuulizwa afisa uhusiano.

Awali gazeti hili, lilipowasiliana na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Hospitalini hapo, Aminiel Aligaesha, ambaye alikuwa ametumiwa maswali ya tuhuma hizo , alisema kuwa yupo nje ya nchi hivyo si busara kuyajibu.

Wiki iliyopita tulichapisha taarifa kuhusu kuharibika kwa tanuru la kuchomea taka na kusababisha mabaki ya miili ya binadamu , dawa na vifaa tiba kuchomwa kwenye shimo la taka.

Pamoja na uongozi kuahidi kuwa unashughulikia tatizo hilo ili wiki hii tanuru hilo liweze kuanza kazi, lakini hadi jana NIPASHE ilifuatilia suala hilo iliambiwa bado linashughulikiwa.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

2 comments:

Anonymous said...

YALE YALE YA AKINA BALALI NA BoT,MKAPA ALIJUA WIZI MKUBWA WA MALI YA UMMA NA AKASHINDWA KUWAJIBISHA SABABU NA YEYE NI MWIZI. HATA HUYO NAYE HAKUNA WA KUMWAJIBISHA SABABU WOTE NI WEZI. KWA TAARIFA YAKO KILA KIONGOZI SASA HIVI ANAKULA KWA LALA SALAMA. JK ANAKULA HIVYO,MAWAZIRI NAO PIA, SEMBUSE HUYO MKURUGENZI

Anonymous said...

Pathetic!