ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, July 27, 2014

Ukawa yazidi kutikisa

  Sitta asema Bunge la Katiba litaendelea
  Jukata yataka liahirishwe hadi 2016
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umegeuka kuwa kimbilio la makundi ya kijamii, ukitakiwa kurejea kwenye vikao vya Bunge Maalum la Katiba, ili kufanikisha mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Wakati rai hiyo ikitolewa na makundi tofauti, Kamati ya Mashauriano ya Bunge hilo, iliyoteuliwa na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, imemaliza vikao vyake huku wajumbe kutoka Ukawa wakiendelea kususia.

Kamati hiyo, imetoa tamko ambapo pamoja na mambo mengine, inasema miongoni mwa sababu za kukua kwa mgogoro uliopo sasa ni kutambuliwa kwa Ukawa kama kundi rasmi ndani ya Bunge hilo.

Hata hivyo, kamati hiyo imependekeza Bunge Maalum la Katiba liendelee na vikao vyake Agosti 5, mwaka huu mjini Dodoma na kuwasihi wana Ukawa kurejea.

SITTA: BUNGE LITAENDELEA
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta, yapo mambo mengi ya kikatiba yanayohitaji kuendelea kwa Bunge hilo na kuyataja kuwa ni haki za usawa wa kijinsia katika nafasi za uongozi.

Mengine ni kuikarabati tume ya uchaguzi, kurekebisha kikatiba masuala ya Muungano, haki za wakulima, wafugaji, ukomo wa vipindi vya uongozi, wasanii na makundi mengineo.

Taarifa hiyo iliyosomwa na Katibu wa Bunge la Katiba, Yahaya Khamis Hamad kwa niaba ya Sitta, ilisema baada ya wajumbe wa kamati ya mashauriano kutoka vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi kususia kikao cha juzi, zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wote waliohudhuria wameazimia bunge hilo liendelee.

UPUNGUFU
Pia, kamati hiyo imesema, pamoja na Ukawa kutambuliwa kama kundi rasmi, mjadala unayaweka kando makundi yanayostahili kwa mujibu wa sheria, yaani wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kundi la wajumbe 201.

Alitaja upungufu mwingine kuwa ni sheria ya mabadiliko ya katiba na kanuni za Bunge hilo kutokuwa na vipengele vinavyozuia utoro, ukosefu wa nidhamu na matendo mengine yanayolenga kuvuruga mchakato huo.

Sitta, alisema hatua ya Ukawa kuendelea kususia Bunge hilo na kupuuza wito wa jamii kupitia makundi mbalimbali pamoja na madhehebu ya dini, inatilia shaka dhamira halisi ya viongozi wake.

Pia alisema kupuuzia juhudi zote za usuluhishi kunazua mashaka kuhusu lengo lao (Ukawa), kwamba pengine ajenga ya viongozi hao ni nyingine na sio upatikanaji wa Katiba Mpya.

“Kamati inarejea kwamba sisi wajumbe 629 tumekabidhiwa jukumu adhimu na la kihistoria kwa niaba ya Watanzania, jukumu ambalo hutokea baada ya miongo kadhaa ya uhai wa Taifa lolote, tutakuwa hatuwatendei haki Watanzania ikiwa hatutafikia maridhiano yaliyotuwezesha kukamilisha kazi tuliyopewa,” alisema.

KANUNI ZIPITIWE UPYA
Aidha, kamati hiyo imesema katika awamu ya pili, Bunge hilo liangalie umuhimu wa kupitia upya baadhi ya kanuni zake, ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kwamba kazi ya kujadili na kupitisha katiba inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 63 zilizosalia.

Kamati ya mashauriano yenye wajumbe 30 iliyokuwa ikiongozwa na Sitta, moja ya kazi iliyopewa ni kushauriana matatizo yaliyotokea Dodoma na kusababisha baadhi ya wajumbe Aprili 16, mwaka huu kutoka nje ya bunge hadi matakwa yao yatakaporidhiwa .

Pia kamati hiyo ilikuwa na kazi ya kutathmini njia za kupata maelewano ya makundi yote ili ungwe ya pili ya mkutano wa bunge uendelee salama na kukamilika kazi waliyokabidhiwa na wananchi.

VIONGOZI WA DINI `WAIPIGIA MAGOTI’
Jana, viongozi wa dini waliwasihi wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, kuacha tofauti zao ili washiriki na kufanikisha mchakato wa kutunga Katiba mpya.

Wakizungumza katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana, kwenye maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ambapo Rais Jakaya Kikwete, alikuwa mgeni rasmi, viongozi wa dini waliwataka wajumbe hao kujali uzalendo na mshikamano wa taifa. Mwakilishi kutoka Baraza la Kikristo (CCT), Steven Mang’ana, aliwataka wabunge wanaojiandaa kushiriki Bunge Maalum la Katiba kuweka mbele uzalendo na mshikamano.

“Wakati taifa lipo katika mchakato wa kutafuta Katiba Mpya, tunawaomba wabunge wawe na maslahi mapana pamoja na kuondoa mkanganyiko wa tofauti za kisasa ili tupate Katiba bora kwa maslahi ya wananchi,” alisema Mchungaji Mang’ana.

Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Wakatoliki (TEC), Padre Raberatus Kadio, pamoja na kuhimiza wajumbe hao kurejea bungeni wakiwa `kitu kimoja’, alikemea vitendo vya uchu wa madaraka na kujilimbikiza mali vinavyofanywa na viongozi.

Alisema Taifa linatakiwa kuendelezwa na misingi yake, ikiwamo watu kuishi kwa amani, umoja na maridhiano. Mwakilishi wa Baraza Kuu la Waislamu nchini (Bakwata) Sheikh Ally Muhidini Kinyogoli, aliwaomba Watanzania kuishi kwa mshikamano na amani.

JUKATA: BUNGE LISITISHWE
Wakati hali ikiwa hivyo kwa viongozi wa dini, Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), limependekeza kusitishwa kwa mchakato wa kuandika Katiba Mpya hadi mwaka 2016, ili kupisha Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Aidha, limependekeza mkutano wa Bunge Maalum la Katiba unaotarajia kuanza Agosti 5, mwaka huu, kukaa kwa siku 14 badala ya siku 60, ili lijadili, kuridhia na kupendekeza ratiba mpya ya mchakato ujao.

Kaimu Mwenyekiti wa Jukata, Hebron Mwakagenda, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana kuwa, sababu za mchakato huo kusitishwa ni kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, muda na vifaa.

Alisema Bunge hilo halipaswi kuendelea kutokana na kupanda kwa joto la kisiasa nchini, ikiwamo Taifa kukabiliwa na michakato sita kwa kipindi cha miezi 15.
Aliitaja michakato hiyo kuwa ni uandikishaji wa vitambulisho vya Taifa, uchaguzi wa serikali za mitaa na uandikishaji upya wa wapiga kura katika mfumo wa kieletroniki (BVR).

Mingine ni uhakiki wa daftari la wapiga kura, upigaji kura ya maoni kuamua hatma ya Katiba Mpya na Uchaguzi Mkuu.

Pia, Jukata imependekeza kuwa mchakato mpya wa kuandika Katiba Mpya unastahili kuendelea mwaka 2016, likiwa na sura na wajumbe wapya, wawili kutoka katika kila wilaya kwa kuzingatia jinsia, watakaoteuliwa na tume huru ya uchaguzi.

Wilayani Temeke, wajumbe wa Ukawa wametakiwa kutumia busara ili kuokoa mchakato wa kupata Katiba Mpya.

Akizunguma katika futari iliyoandaliwa na Meya wa Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam jana, Sheikh wa Wilaya ya Temeke, Mohamad Kingo, alisema Ukawa, watafakari kwa kina na kuchukua uamuzi wenye maslahi kwa umma.

Ukawa, wamesusia kushiriki shughuli za Bunge hilo kwa madai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ‘kimechakachua’ rasimu halisi iliyopaswa kujadiliwa, ikitokana na maoni ya wananchi.

Sheikh Kingo, alisema makundi yote yanatakiwa kuacha pembeni tofauti zao za kimsimamo, badala yake wakae kwa pamoja kuangalia njia ambazo zitapelekea nchi kupata Katiba bora yenye manufaa kwa Watanzania.

SHEREHE ZA MASHUJAA
Kabla ya viongozi wa kidini kutoa nasaha zao kwenye Siku ya Mashujaa, Rais Kikwete, aliingia kwenye viwanja hivyo saa 3:00 asubuhi na kupigiwa wimbo wa Taifa.

Pia, ilipigwa mizinga miwili kama ishara ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha kwa ajili ya kuipigania nchi, na baadaye viongozi mbalimbali waliweka silaha za jadi na mashada ya maua kwenye mnara wa kumbukumbu.

Rais Kikwete, alianza kwa kuweka mkuki na ngao na kufuatiwa na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Devis Mwamunyange ambaye aliweka silaha ya jadi aina ya sime.

Kiongozi aliyefuatia alikuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi aliweka upinde na mshale; na kiongozi wa mabalozi nchini aliweka shada la maua na Mwenyekiti wa Chama cha Askari Wastaafu, Ezekiel Chacha aliweka shoka kwa niaba ya wastaafu wenzake.

Habari hii imeandikwa na romana mallya, Moshi Lusonzo na Christina Mwakangale
CHANZO: NIPASHE

No comments: