ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 20, 2014

Azam robo fainali Kagame leo

kocha wa Azam,Joseph Omog
Wawakilishi wa Tanzania Bara katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) timu ya Azam ya Dar es Salaam wanatarajia kushuka dimbani leo kuikabili El Merreikh kutoka Ethiopia katika mechi ya hatua ya robo fainali itakayofanyika kwenye Uwanja wa Nyamirambo jijini hapa.

Mechi hiyo ya robo fainali ya tatu ya mashindano ya mwaka huu itafanyika kuanzia saa 9:00 alasiri kwa saa za hapa sawa na saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Akizungumza na NIPASHE jana baada ya mazoezi ya asubuhi kwenye Uwanja wa Mumena, kocha wa Azam, Joseph Omog, alisema kuwa kikosi chake kiko tayari kwa ajili ya mechi hiyo ya kuwania kucheza nusu fainali.

Omog alisema kuwa wachezaji wake wataongeza umakini katika mechi hiyo na asingependa wafike hatua ya matuta.


Mcameroon alisema kwamba anawafahamu vizuri El Merreikh na anawaheshimu kutokana na soka la ushindani wanalocheza.

"Maandalizi yameenda vizuri, tuko tayari kwa mchezo, kikubwa ni kuongeza umakini katika mechi ili tufike nusu fainali, tunawaheshimu El Merreikh na naifahamu kwa muda wa miaka miwili sasa nimekuwa nikiifuatilia," alisema Omog ambaye kikosi chake kinaishi hoteli moja na wapinzani hao.

Aliongeza kuwa wachezaji wake wote wa kikosi cha kwanza wako katika hali nzuri isipokuwa beki Waziri Salum ambaye atakosa mechi zote zilizobakia kutokana na kushindwa kupona maumivu ya kifundo cha mguu.

Omog alikataa kuweka wazi mbinu atakazotumia katika mechi ya leo huku pia akisema jana jioni ndiyo alitarajia kupanga kikosi kitakachoanza.Naye nahodha wa timu hiyo, John Bocco, alisema kwamba wachezaji wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanashinda mechi ya leo.

Bocco alisema kuwa kila mmoja anafahamu umuhimu wa mechi hiyo na deni walilonalo ni kuhakikisha wanawafurahisha Watanzania.

"Ni mechi ngumu lakini kwa ujumla tuko tayari kupambana ili tuweze kushinda, tunamuomba Mungu atusaidie kutimiza ndoto zetu, ni wazi kwamba si mechi rahisi," Bocco aliongeza.

Mechi nyingine ya robo fainali itakayofanyika leo ni kati ya KCCA ya Kampala, Uganda dhidi ya Atlabara ya Sudan Kusini.

Timu zitakazoshinda katika mechi hizo za leo, zitakutana katika mechi ya nusu fainali ya pili itakayochezwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Amahoro jijini hapa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: