ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 2, 2014

CCM, Ukawa ngoma nzito

Kikao chagonga mwamba kufikia muafaka
Mazungumzo ya kufikia muafaka wa kushawishi Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kurudi Bungeni ili kuendelea na mchakato wa kujadili Rasimu ya Katiba Mpya, yameendelea kuwa magumu baada ya kikao hicho kutofikia muafaka hadi jana.

Kikao hicho ambacho kinafanyika katika hoteli ya Sea Cliff jijini Dar es Salaam, kilianza asubuhi jana lakini hadi jioni mazungumzo hayo yalikuwa yakiendelea.

Waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia katika hoteli hiyo ambayo mazungumzo hayo yalikuwa yakiendelea na badala yake walikuwa wakisubiri nje kuvizia wajumbe wa mkutano kuwaeleza kinachoendelea.

Hata hivyo, ilipofika wakati wa chakula cha mchana, Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, ambaye ndiye Mwenyekiti wa kikao hicho, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wamekubaliana kwenye kikao hicho kuwa yeye ndiye atakuwa msemaji wa yatakayojiri kwenye kikao hicho.

Licha ya kusubiri kwa muda mrefu, wajumbe wa pande zote mbili za Ukawa na CCM, walionekana kutoka nje ya kikao na kukaa katika makundi wakiendelea na majadiliano.

Kwa upande wa Ukawa wakiwa na wajumbe zaidi ya 10 walioonekana ni Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba, Dk. Wilbroad Slaa, John Mnyika, James Mbatia, Halima Mdee na Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Nyambambe Mosena.

Kwa upande wa kundi la CCM kulikuwa na wajumbe 11 ambao walioonekana ni Katibu Mkuu wa CCM, Abdulraham Kinana, Mussa Zungu, Hawa Ghasia, Nape Nnauye na January Makamba.

Hata hivyo, wajumbe wa kundi la Ukawa , walionekana kuendelea na mvutano wa kutoelewana licha ya kutoka nje kwenye makundi.

Saa 12.27 jioni, wajumbe hao walionekana kutoka nje ya kikao hicho wakiwa wamegawanyika katika makundi mawili. Aidha, saa 12.31 jioni, kundi la wajumbe kutoka CCM lilionekana kumaliza majadiliano yao na kurudi ukumbini.

Habari kutoka kwenye kikao hicho zinasema kuwa kikao hicho kitaendelea kufanyika mpaka muafaka utakapopatikana.

“Hata kama bunge maalumu la katiba litaendelea kufanyika mjini Dodoma, kikao chetu cha hapa kitaendelea kufanyika hadi tuone mwisho wake,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Hoteli hiyo ilionekana kuzingirwa na kikosi cha wana usalama ambacho kilikuwa kikifuatilia mwenendo mzima wa kikao hicho.
Wakati tunaenda mitamboni, Profesa Lipumba alitoka nje na kuwaambia waandishi wa habari kuwa leo watatoa taarifa ya kinachoendelea kuhusu mkutano wa jana.
CHANZO: NIPASHE

No comments: