Advertisements

Friday, August 22, 2014

Dk Kigoda awaita Wachina zaidi nchini

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amewaomba wawekezaji wa Kichina kuwekeza zaidi nchini ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo.
Dk Kigoda aliyekuwa akifungua maonyesho ya siku nne ya bidhaa za China jana, alibainisha kuwa iwapo wawekezaji hao wakiongeza kasi ya uwekezaji watapunguza tatizo la ajira, kuongeza teknolojia na kuwapa uzoefu wafanyabiashara wazawa.
“Nawaomba wawekezaji hawa waje kwa wingi na kushirikiana na wazawa ili waongeze thamani ya bidhaa zetu ili zikiuzwa nje ya nchi ziweze kushindana kimataifa,”alisema Dk Kigoda.
Waziri huyo aliwasisitizia wawekezaji wa Kichina waliokuja katika maonyesho hayo yanayomalizika Jumapili kuwekeza zaidi katika sekta za madini, mafuta na gesi na nyingine zitakazochochea ukuaji wa uchumi.
Uhusiano baina ya nchi hizi mbili umezidi kukua huku kukiwa hakuna uwiano wa kibiashara ambapo China imeingiza bidhaa za takriban Dola 3.7 bilioni(Sh6.1 trilioni) za Marekani wakati Tanzania imeuza bidhaa zake China zenye thamani ya Sh907.5 bilioni.
Dk Kigoda alisema kuwa Tanzania ilipewa fursa ya kuuza bidhaa China kwa masharti nafuu ya ushuru na forodha lakini wafanyabishara wemeshindwa kutumia vizuri fursa hiyo.
“Tumepewa upendeleo wa nafuu ya kodi na ushuru kwa karibu bidhaa za aina 4,000 lakini tumeshindwa kutumia vizuri. Viwanda vya Tanzania vijitahidi kuongeza ubora wa bidhaa zao ili waweze kutumia soko hilo vizuri,” aliongeza.
Aliwataka wafanyabiashara wa ndani kutumia nafasi ya maonyesho hayo ili kubadilishana mawazo na uzoefu wa kibiashara ili waweze kuzalisha bidhaa zinazoweza kushindana kimataifa.
Balozi wa China nchini, Li Yuoqing alisema kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania kibiashara kwa kuhakikisha bidhaa za Tanzania nazo zinafahamika China kupitia fursa za maonyesho.
“Tanzania ni nchi kubwa yenye amani na rasilimali za kutosha hivyo nina imani kwa ushirikiano na wafanyabiashara wetu, Watanzania wengi watajifunza mengi,” alisema Youqing.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Haya ndiyo mambo ya kuibiwa live