Tuesday, August 12, 2014

Dk. Magufuli: Foleni Dar itakuwa ndoto

Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katikati akiwa na Balozi wa Japan Nchini Masaki Okada kulia wakipita juu ya Daraja la Lugalo mara baada ya kulikagua katika ziara ya Ukaguzi wa Barabara ya Mwenge Tegeta jijini Dar es salaam leo.

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, amesema katika kipindi cha miaka mitatu ijayo tatizo la msongamano wa magari katika barabara za jiji la Dar es Salaam litakuwa ndoto.

Alisema hayo jana wakati wa ziara ya kukagua miradi ya barabara inayojengwa katika jiji hilo.

Alisema serikali imetenga zaidi ya Sh. Trilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa barabara za jiji la Dar es Salaam, ikiwamo ujenzi wa ‘Fly Over’ katika makutano ya barabara za Ubungo, Tazara na Kamata.

Waziri Magufuli alisema Oktoba, mwaka huu, ujenzi wa ‘Fly Over’ katika eneo la Tazara wenye urefu wa kilomita 1.2 utakaoghalimu zaidi ya Sh. bilioni 100 utaanza kujengwa.

“Ninawahakikishia wakazi wa Dar es Salaam na vitongoji vyake, katika miaka mitatu ijayo tatizo la foleni katika jiji hili litakwisha, Ubungo ujenzi utaanza Novemba, mwaka huu,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema katika eneo la Ubungo kutajengwa mapishano ya barabara utakaogharimu kati ya Sh. bilioni 46 hadi 50, ujenzi utakaochukua miaka miwili na nusu hadi kukamilika kwake. Dk. Magufuli alisema barabara ya Tegeta-Mwenge iliyogharimu Sh. bilioni 89 imeshakamilika kujengwa, huku Sh. bilioni mbili zikiwa zimetengwa kwa ajili ya kuweka taa na muda wowote Rais Jakaya Kikwete ataifungua.

Alisema mwishoni mwa mwezi huu, serikali itapokea kivuko cha meli kutoka nchini Denmark kitakachofanya kazi Dar es Salaam hadi Bagamoyo, lengo likiwa ni kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada, alisema, Japan itakuwa bega kwa bega kuisaidia Tanzania katika masuala ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa barabara.

Meneja Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT), Barakaeli Mmari, alimweleza Waziri Magufuli kuwa kuna wizi wa vifaa katika mradi wa BRT unaochelewesha kukamilika kwa wakati.

Alisema hadi sasa milingoti ya taa saba, alama za barabarani 25, mifuniko ya maji machafu 12 imeshaibiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alisema kutokana na wizi huo, kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa itafanya kazi ya kuwabaini wahusika wa uhalifu huo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake