ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 4, 2014

Karume atinga polisi kumwona Mansour

Aliyewahi kuwa Waziri wa SMZ, Mansour Yusuph Himid ambaye alikamatwa na silaha mbili za moto na risasi 412, nyumbani kwake Chukwani hivi karibuni. Picha ya Maktaba.

Zanzibar. Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume jana alifika Kituo cha Polisi Madema kumjulia hali shemeji yake, aliyewahi kuwa Waziri wa SMZ, Mansour Yusuph Himid ambaye alikamatwa na silaha mbili za moto na risasi 412, nyumbani kwake Chukwani hivi karibuni.
Karume alifika katika kituo hicho ambacho ni Makao Makuu ya Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi saa 5.30 asubuhi na kumjulia hali Himid ambaye amewekwa mahabusu akisubiri uchunguzi wa polisi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Habari za uhakika kutoka ndani ya polisi zinadai kuwa Rais Karume alizungumza na shemeji yake kwa muda usiopungua dakika tano na kumtaka kuwa mstahimilivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na utaratibu wake.
Viongozi wengine waliofika katika kituo hicho ambacho kimeimarishwa ulinzi tangu alipofikishwa juzi, ni pamoja na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka CUF; Hija Hassan Hija (Kiwani), Saleh Nassor Juma (Wawi), Hassan Hamad Omar (Kojani ) na Naibu Waziri wa Maji, Nishati, Makazi na Ardhi, Haji Mwadini Makame ambao walimpa mkono wa pole 6.30 mchana.
“Mansour anastahili pongezi na siyo kupewa pole, inashangaza mambo ya ulinzi na usalama ni ya Muungano kwa nini upande mmoja uruhusiwe kumiliki silaha na upande mwingine uzuiwe, ndiyo maana tunasema Zanzibar haitendewi haki,” alisema Hija muda mfupi baada ya kutoka kituoni.
Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi linapaswa kuendelea na operesheni ya kuwasaka viongozi wengine wanaomiliki silaha na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa vile tukio hilo limewafunza mambo mengi na kutaka haki itendeke.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai Zanzibar, Salum Msangi alisema polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na matokeo yake ndiyo yatakayoamua wapi pa kufunguliwa mashtaka kati ya Zanzibar au Tanzania Bara.
“Kwa mujibu wa sheria za Zanzibar, hairuhusiwi raia yeyote kumiliki bastola,” alisema.
Himid alipekuliwa nyumbani kwake juzi baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa za kiintelejensia kuwa anamiliki silaha za moto.
Taarifa kutoka katika eneo la tukio zinaeleza kuwa kazi ya upekuzi wa nyumba mbili zilizopo katika eneo moja ilifanywa kwa kutumia mashine maalumu.
Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...


mungu atampa kila la kheri laki babumju wajue huo ndio mwisho wao.

Insha Allah itakuwa kheri tu.Ni hawa hawa ndio walio mdhalilisha maalim Seif na leo wanampigia saluti.Jengine ni kwamba kesi za aina hii zinaendeshwa kwa amri ya wanasiasa uchwara wanaojificha nyuma ya pazia.Visingizio vinavyotolewa mahakamani ni upelelezi haujakamilika, mtuhumiwa akibaki uraiani anaweza kuharibu upelezi au pia anaweza kutoweka.

Nia na lengo ni kumkomoa hasa baada ya kujiunga na chama cha CUF na dhana ya kwamba huenda akagombea katika jimbo la kiembe samaki aliloliongoza.

Kuungoa mti uliopandwa miaka hamsini iliyopita kunataka mbinu kubwa lakini kwa umoja wetu tutaungoa.

Anonymous said...

kunamambo katika mikutano alivokuwa akihutubia Mansour. huwa akisema hapa si pahala pake na wala si wakati wake kwa kuyasema .Ana siri kubwa anataka kuitowa na ndiomaana wakamfanyia ujanja wa kumkamata