Advertisements

Thursday, August 21, 2014

KAULI NDIYO SILAHA PENZINI

KARIBUNI kwa mara nyingine katika safu yetu maridhawa ya All About Love. Kwa mtu 

anayejali, lazima atakuwa akipata vitu vinavyoweza kumsaidia katika maisha yake ya kimapenzi anayoishi.Tunajua changamoto nyingi zilizopo katika mambo yetu haya ya uhusiano.

Mapenzi, pamoja na utamu wake, lakini hakuna kitu hatari kama hiki katika maisha kinachoweza kukuharibia ndani ya muda mchache kuliko unavyofikiri.

Watu wanamwagiana maji ya moto, tindikali, kuchomwa visu na hata kuuana kwa sababu ya mapenzi. Na usije ukadhani wanaofanyiana hivi ni wale waliochepuka, hapana, wakati mwingine mume anamfanyia hivyo mke wake au mke anamfanyia mume wake.

Na kinachosababisha litokee hivi, siyo mara zote linahusiana na mapenzi moja kwa moja, ni kitu kingine kabisa. Maana tumezoea mume au mke kumfanyia mwenzake unyama kwa sababu labda alimfumania na mtu mwingine.


Hii inatokana na jinsi tusivyo huru kimawazo katika kukabiliana na changamoto zinazokuja mbele yetu. Kuna kitu kimoja ambacho wanandoa wengi na walio katika uhusiano wanashindwa kukielewa kuwa ni cha msingi sana katika maisha yao ya kimapenzi.

Kauli
Kauli ni jambo linaloonekana dogo, lakini lina madhara makubwa sana, siyo tu katika mapenzi, bali hata katika maisha ya kawaida tunayoishi uswahilini. Ndiyo maana unaweza kuwa umeshasikia mara nyingi sana habari kuwa mtu kachomwa kisu kwa deni la shilingi mia moja au hata elfu moja.

Unajiuliza mara nyingi ni vipi umuue mwenzako kwa deni dogo kiasi hiki, lakini kumbe nyuma ya pazia ni kauli. Badala ya mdaiwa kutoa majibu mazuri, anajibu ovyo, mtu anapandisha hasira, ibilisi anafanya kazi.

Katika mapenzi, kauli au kwa maana nyingine lugha ni silaha kubwa sana inayoweza kuyalinda au kuyaharibu. Siku zote ni lazima uwe mtu mwenye kuzichunguza sana kauli zako kabla ya kuzitoa kwa mwenza wako.

Katika nyakati mbaya za uhusiano wenu, kauli ndicho kitu pekee kitakachoweza kuboresha palipoharibika au kuharibu kabisa. Unaweza kuzungumza na kutuma ujumbe ukafika bila kutoa mapovu.

Unapotaka kukabiliana na mwenza wako, ili uende sawa ni lazima kwanza upunguze hasira, ujiweke katika nafasi ambayo unaweza ukazungumza na mwenzako akakuelewa. Tunachokosea sisi, tunatanguliza hasira na kauli zisizofaa, ndiyo maana moto unazidi kuwaka.

Kwa mfano, umekuta mipira ya kiume katika mfuko wa suruali ya mpenzi wako. Ni dhahiri kwamba hiyo si kwa ajili yako. Kama ni matumizi atatumia na mwanamke mwingine. Ingawa hiyo ni dalili iliyo wazi kabisa kuwa mwenzako ni mchepukaji, lakini haikufanyi kuwa na hasira na kuondoa staha katika kumkabili.

Kwanza mshukuru Mungu kwamba angalau mwenzako anajali. Hawezi kukuletea maradhi kutoka huko kwenye michepuko yake. Lakini pia, ukimuendea taratibu, aibu ya kibinadamu itamshika, hata kama hatasema, lakini atajutia.

Kauli ya ukali kwa jambo kama hili, unaweza kumpa nafasi ya kukugeuzia kibao. Nikuambie kitu, siku zote watu wakosefu hutafuta udhaifu wa anayemhusu katika kukabiliana naye. Kama unafoka, anaweza kuondoka nyumbani akijidai unampigia kelele na pengine akaenda kufanya kweli kabisa, ili kukukomoa!

Ikitokea hivyo, utakuwa umekosa kujua sababu ya yeye kuja na kondom nyumbani, ungekwenda taratibu, ungemnyima nafasi ya kuongopa, badala yake angekuomba msamaha. Kumbuka, KAULI NI SILAHA YAKO NAMBARI ONE! GPL

No comments: