ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 23, 2014

Kesi yafunguliwa Bunge la Katiba, Kesi ya kuhoji uhalali wake yafunguliwa

“Ni jambo ambalo ameomba mwenyewe kuhamia huko na ameruhusiwa maana hilo ni jambo la kawaida kama ambavyo wajumbe wengine kama kina Freeman Mbowe waliwahi kuomba, siyo jambo geni.” Hamad Rashid Mohamed

Dar es Salaam/Dodoma. Bunge la Katiba linaloendelea mjini Dodoma kwa sasa liko katika hatihati ya kuendelea baada ya kufunguliwa kesi ya kuhoji madaraka yake.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana na Mwandishi wa Habari Saidi Kubenea, kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo iliyopewa usajili wa namba  28 ya mwaka 2014, Kubenea anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya Mamlaka ya Bunge la Katiba. Kubenea amefungua kesi hiyo akiomba mahakama itoe tafsiri hiyo, chini ya  vifungu vya 25 (1) na 25 (2) vya Sheria ya Marekebisho ya Katiba namba Namba 83 ya mwaka  2011.
Sambamba na kesi hiyo ya kuomba tafsiri ya mamlaka ya Bunge  hilo, pia Kubenea amewasilisha maombi mahakamani hapo akiiomba mahakama itoe zuio la muda la kusimamisha Bunge hilo ili kusubiri uamuzi wa maombi ya tafsiri hiyo.
Maombi hayo ya kusimamisha Bunge hilo kwa muda yaliyopewa usajili wa namba 29 ya mwaka 2014, pamoja na maombi ya msingi ya tafsiri ya mamlaka ya Bunge yote yalifunguliwa mahakamani hapo jana chini ya Hati ya Dharura.
Katika kesi hiyo ya msingi anaiomba Mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya masharti ya vifungu hivyo vya sheria hiyo na pia itamke kama Bunge hilo lina mamlaka ya kubadilisha maudhui ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa hati ya madai, Kubenea anadai kuwa msingi wa kesi hiyo unatokana na uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Desemba Mosi, 2011, lililopitisha  Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Anasema sheria hiyo ilikuwa na lengo la kuratibu mchakato wa kutungwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anaendelea kusema kuwa kutokana na sheria hiyo,  Rais aliunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na mambo mengine vilevile kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mapendekezo ya Katiba Mpya na kwamba kwa msingi huo Tume hiyo iliandaa Rasimu ya Katiba.
Anadai kuwa baada ya Tume hiyo kuundwa iliendelea kukusanya maoni ya wananchi yaliyotolewa katika mikutano ya hadhara na katika miundo tofauti ikiwamo mabaraza ya Katiba yaliyoanzishwa kila wilaya kwa lengo hilo.
Hati hiyo inaendelea kueleza kuwa kwa mujibu wa takwimu halisi za tume hiyo,  jumla ya watu 333,537 walitoa maoni yao katika nyanja tofauti, tofauti za mapendekezo ya Katiba, ambayo ndiyo Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyatumia kuandaa Rasimu ya Katiba Mpya.
Inaendelea kueleza hati hiyo kuwa baada ya Rais kukabidhiwa rasimu ya mwisho Desemba 8, 2013, kwa mujibu wa vifungu vingine vya sheria hiyo, aliunda Bunge la Katiba kwa lengo la kujadili Rasimu ya Katiba na hatimaye kupata Katiba Mpya.
Hata hivyo, kwa mujibu wa hati hiyo baada ya Bunge la Katiba kuundwa, mjadala uliibuka ndani na nje  ya  misingi ya kisheria kuhusu mamlaka yake, kama Bunge linaweza kwenda kinyume na Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na tume hiyo.
Inaendelea hati hiyo kubainisha kuwa mjadala huu pia uliibuka ndani ya Bunge la Katiba lenyewe kuhusiana na mamlaka yake katika utekelezaji wa majukumu yake kama lina mipaka au la kwa mujibu wa vifungu hivyo 25 (1) na 25 (2) vya sheria hiyo.
Katika kusisitiza mjadala kuhusu mamlaka ya bunge hilo, hati hiyo inatoa mfano wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) katika mkutano wake wa mwaka, ambacho kilisema kuwa vifungu hivyo havilipi bunge hilo mamlaka ya kubadili rasimu hiyo.
Hati hiyo inaongeza kuwa wakati TLS wakitoa msimamo huo, kuna wataalamu wengine wa sheria wanadai kuwa  Bunge hilo linaweza kubadilisha na kuongeza ibara kadri itakavyoona inafaa bila kujali rasimu hiyo.
Kwa mujibu wa hati hiyo, mvutano huo ndani ya Bunge hilo ulisababisha baadhi ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka nje na kususia vikao, wakidai kuwa  rasimu hiyo haiwezi kubadilishwa. Msimamo huo wa wajumbe wa Ukawa, kwa mujibu wa hati hiyo ni  tofauti na wajumbe wengine waliobaki wanaodai kuwa Bunge hilo lina mamlaka ya kubadili vifungu vya rasimu.
Kwa mujibu wa hati hiyo, utungaji wa Katiba ni jambo la kitaifa ambalo si tu kwamba linabeba matumaini ya Watanzania bali pia linabeba mustakabali na ustawi wa nchi.
Hivyo, hati hiyo inaeleza kuwa tafsiri sahihi ya mamlaka ya Bunge la Katiba dhidi ya Rasimu ya Katiba ni jambo  muhimu sana katika kuongoza mchakato huo ili kuhakikisha kuwa unakwenda kwa mujibu wa sheria zinazohusika.
Katika hati ya maombi, Kubenea anaomba mahakama itoe amri ya kusimamisha kwa muda vikao vya Bunge la Katiba vinavyoendelea Dodoma, kusubiri uamuzi wa  Mahakama kuhusu mamlaka yake.
Katika hati ya kiapo chake aliyoiambatanisha na kesi na maombi hayo, Kubenea anadai kuwa hata baada ya Wajumbe wa Ukawa kutoka nje, wajumbe waliobaki wanaendelea kujadili rasimu hiyo.
Hati hiyo ya kiapo inaeleza kuwa kufunguliwa kwa kesi hiyo sambamba na maombi hayo ya kusimamisha kwa muda Bunge la Katiba si tu kunalenga kupata tafsiri ya Kimahakama kuhusu mamlaka ya Bunge la Katiba.
Rafu Kamati za Bunge Maalumu
Wakati kesi hiyo ikifunguliwa, kumekuwa na taarifa ndani ya kamati za Bunge zinazoendelea kuchambua rasimu hiyo zinazoeleza kuchezwa rafu ili kuwezesha upatikanaji wa akidi kwa ajili ya hatua ya kupiga kura kupitisha ibara za rasimu hiyo katika baadhi ya kamati.
Hivi sasa kamati nyingi ziko katika hatua ya kupiga kura ili kupitisha ibara za Rasimu ya Katiba, kazi ambayo inahitaji theluthi mbili ya wajumbe kutoka pande za muungano kwa mujibu wa kanuni za Bunge Maalumu.
Ili kutimiza matakwa hayo, gazeti hili limebaini kuwa rafu zimeanza kuchezwa hasa katika kamati ambazo zimeshindwa kutimiza sharti hilo. Moja ya rafu hizo ni ile ya mjumbe wa Kamati namba tano, Maida Hamad Abdallah kuhamishiwa kinyemela katika Kamati namba 8, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuwezesha upatikanaji wa akidi katika kamati aliyohamia.
 Habari zinasema mjumbe huyo kutoka Zanzibar alishiriki kupiga kura juzi mchana na wajumbe wa kamati hiyo walielezwa kuwa amepelekwa ili kuziba nafasi ya Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum ambaye hawezi kushiriki vikao hivyo kutokana na kwamba ni mgonjwa.
 Hata hivyo, suala hilo lilizua mvutano kiasi baada ya baadhi ya wajumbe kuhoji uhalali wa uhamisho huo ambao ni kinyume cha kanuni za Bunge Maalumu, hasa ikizingatiwa kwamba alipigia kura mambo ambayo hakushiriki kuyajadili na kuyafanyia uamuzi.
Mwenyekiti wa Kamati namba tano, Hamad Rashid Mohamed alithibitisha Abdallah kuhamia kamati namba nane inayoongozwa na Naibu Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai kwa maelezo kwamba aliomba mwenyewe.
“Ni jambo ambalo ameomba mwenyewe kuhamia huko na ameruhusiwa maana hilo ni jambo la kawaida kama ambavyo wajumbe wengine kama kina Mbowe (Freeman) waliwahi kuomba, siyo jambo geni,” alisema Rashid.
 Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu, Yahya Khamis Hamad alisema hakuwa na taarifa za uhamisho huo. Alipoulizwa kuhusu iwapo Kanuni zinaruhusu alisema suala la kupanga ujumbe wa kamati liko chini ya mamlaka ya mwenyekiti wa Bunge hilo.
 “Kwa kweli sifahamu na wala sina taarifa hiyo, hilo suala la kanuni pengine hebu zisome ili ufahamu zinasemaje kuhusu mjumbe kuhama kutoka kwenye kamati moja kwenda kamati nyingine,” alisema Hamad.
 Wajumbe wa Bunge Maalumu waliokwisharipoti wanakaribia 450, idadi ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya akidi inayotakiwa, lakini hali ni tofauti kwenye kamati kutokana na sababu mbalimbali, utoro ikiwa mojawapo.
 Kutokana na mwenendo huo na wajumbe wengi kutoingia kwenye vikao licha ya kuripoti, kuna wasiwasi iwapo akidi itapatikana wakati wa kupitisha rasimu hiyo wakati Bunge Maalumu litakapoanza kukutana kwa umoja Septemba 2 mwaka huu.
Matakwa ya kanuni
Kanuni ya 55 (1) ya Kanuni za Bunge Maalumu Toleo la 2014 inasema: “Kamati zinaundwa na mwenyekiti kwa namna ambayo itawezesha kila mjumbe kuteuliwa kuwa mjumbe wa kamati mojawapo.”
Fasili ya pili ya kanuni inasema wakati wa kufanya uteuzi wa wajumbe hao, mwenyekiti atazingatia kwa kadri inavyowezekana idadi ya wajumbe inalingana kwa kila kamati na uwiano kutoka pande zote za muungano.
Kadhalika kanuni hiyo inasema katika uteuzi wake mwenyekiti atazingatia idadi ya kila aina ya wajumbe ilivyo katika Bunge Maalumu, jinsia, wajumbe wenye mahitaji maalumu na uwepo wa wajumbe wenye utaalamu wa sheria.
Kanuni hiyo iko kimya kuhusu uhamishaji wa wajumbe na fasili yake ya nne inasema: “Ujumbe katika kamati utadumu kwa kipindi chote cha maisha ya Bunge Maalum.”
Waraka wa uchambuzi wa mgawanyo wa wajumbe katika kamati unaonyesha kuwa Kamati namba tano alikotoka Maida ina wajumbe 52 na kati yao 34 wanatoka Tanzania Bara na 18 Zanzibar wakati kamati alikohamia pia ina wajumbe 52; 35 kutoka Tanzania Bara na 17 kutoka Zanzibar.
Kwa maana hiyo hata kama uhamisho wa Maida ungekuwa na lengo la kuimarisha uwiano kwa maana ya pande za muungano, ni dhahiri kwamba unaathiri kwa maana ya idadi wajumbe kutoka Zanzibar katika kamati namba tano.
Gazeti hili lilimtafuta Ndugai kwa lengo la kupata maelezo jinsi alivyompokea mjumbe huyo, lakini kutwa nzima ya jana simu yake ilikuwa ikiita bila majibu. Kadhalika Maida naye alitafutwa lakini simu yake ilikuwa imezimwa wakati wote. Maida hakuwamo kwenye kamati yake ya awali namba nne ilipokutana jana mchana baada ya kuwa wamepumzika asubuhi kupitia sura za nyongeza.
Kupitisha uamuzi

Kanuni hizo pia zinaelekeza kwamba wakati wa kupitisha uamuzi lazima wajumbe wawe wamefikia theluthi mbili kwa pande zote za muungano, jambo ambalo limekuwa gumu kutokana na mahudhurio hafifu kwenye kamati husika.
Mwananchi

No comments: