ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 8, 2014

KOCHA MAXIMO AREJESHA NIDHAMU YA USAJILI YANGA

Kocha Mkuu wa timu ya Yanga mbrazil Marcio Maximo akiteta jambo na mshambuliaji wa timu hiyo Jeryson Tegete kwenye mazoezi 
By KHATIMU NAHEKA (email the author) 

Katika kuhakikisha hilo, kocha huyo amesajili Wabrazili wawili kwa gharama ambayo haifiki hata nusu ya usajili wa Emmanuel Okwi anayezozana na viongozi akitaka kumaliziwa chake.
UJIO wa Kocha Mbrazili, Marcio Maximo, ndani ya Yanga umefuta usajili wa mamilioni uliokuwa ukifanywa kiholela na baadhi ya vigogo bila kufanya tathmini ya staa husika, lakini sasa usajili unafanyika kimahesabu.

Katika kuhakikisha hilo, kocha huyo amesajili Wabrazili wawili kwa gharama ambayo haifiki hata nusu ya usajili wa Emmanuel Okwi anayezozana na viongozi akitaka kumaliziwa chake.

Yanga kabla ya kuja kwa Maximo, ilitumia Dola 100,000(Sh165 milioni) kumsajili Okwi tu, lakini ikatumia Dola 35,000 (Sh57 milioni) kuwasajili Wabrazili wawili Andrey Coutinho na Genilson Santos ‘Jaja’.
Klabu hiyo bado inadaiwa na Okwi Dola 40,000 (Sh66 milioni) zilizobaki kwani makubaliano yalikuwa alipwe ada ya dola 100,000 kwa mkataba wa miaka miwili na nusu.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga iliyopigwa chini kwenye michuano ya Kagame kwa kupeleka kikosi laini, zinasema kwamba Coutinho amesajiliwa kwa dau la dola 15,000(Sh24.8) na analipwa mshahara wa Dola 2,700(Sh4.4milioni) kwa mwezi.

Jaja ambaye bado hajapata kibali cha kuichezea Yanga kutokana na usajili kutokamilika, alisajiliwa kwa Dola 20,000 (Sh33 milioni) na analipwa mshahara wa Dola 2,800 (Sh4.6 milioni).

“Kila mmoja wao amesaini mkataba wa miaka miwili tu, unaweza kuona hatukutumia kiasi kikubwa sana cha fedha na nina hakika watatusaidia,” alisema bosi mmoja mwenye ushawishi mkubwa ndani ya Yanga.

Tayari Coutinho ameanza kuonyesha uwezo katika nafasi ya winga wa kushoto huku Jaja akiendelea kupambana katika ushambuliaji wa kati.

Wachezaji hao wanakuwa raia wa kwanza wa Brazil kusajiliwa na Yanga na kucheza Ligi Kuu ya Bara katika miaka ya karibuni. Coastal Union iliwahi kusajili Mbrazili, Gabriel Barbosa, lakini akashindwa kuwika na akatemwa.

Okwi ambaye kiwango chake bado hakijawaridhisha Yanga, analipwa mshahara wa Dola 4000 (Sh6.6 milioni) ambao ni mshahara mkubwa zaidi Yanga na pengine kwa wachezaji wote wa Ligi Kuu Bara.

Maximo aibuka, kambi Pemba

Yanga imethibitisha rasmi kwamba sasa kikosi chao kitatua Pemba tayari kwa kambi, lakini Maximo ‘The Chosen One’ amesisitiza kutoipeleka Yanga kwenye Kagame haimaanishi anaogopa kufungwa.

Maximo alisema ameshtushwa na madai ya kwamba anahofia ushindani wa kupoteza mechi kutokana na uimara wa timu anazokwenda kupambana nazo. “Rais wa Cecafa, Tenga (Leodegar) kwangu mimi ni kiongozi bora tangu nimeanza kazi hii ambaye nimewahi kufanya naye kazi, nafikiri michuano hii haikuja wakati sahihi kulingana na timu yangu,” alisema.

“Tulikuwa na sababu nyingi lakini kuna nane zenye uzito ambazo zilitulazimu kutowajumuisha wachezaji wetu kushiriki mashindano hayo, nimeshakutana na mechi nyingi zenye ushindani mkubwa kamwe siwezi kuogopa mechi kama inavyoelezwa.

“Nimeshiriki michuano mikubwa duniani siwezi kuogopa mechi za Kagame, unawezaje kuwapeleka kwenye mashindano wachezaji ambao hujawahi kuwafundisha hata siku moja, mpira sio kupika wali ndani ya dakika 10 umeiva, watu wanatakiwa kuelewa hili.”

Maximo alisema sasa kikosi chake kitaondoka jijini Dar es Salaam Jumatatu kuelekea Kisiwani Pemba ambapo wataweka kambi ya siku kumi.

“Tutaondoka Jumatatu kuelekea Pemba tutakuwa na kambi ya siku 10, nimewaambia wachezaji wote hasa wale wa kigeni wafike klabuni Jumamosi na hata wale waliokuwa na majukumu ya kitaifa tutawapa siku tano za mapumziko kabla ya kuanza kazi,” alisema.
CREDIT:MWANASPOTI

No comments: