ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 15, 2014

KUNA KITU ZAIDI YA NENO NAKUPENDA-3


MARAFIKI tunaendelea kujifunza zaidi kuhusu maisha ya uhusiano na mapenzi. Leo tunafikia tamati ya mada hii iliyoanza wiki mbili zilizopita.
Tumeshajifunza mengi, kama mtakumbuka wiki iliyopita tulianza kuona nini cha kufanya kwa kuanza na kuchunguza tatizo. Hebu sasa twende kwenye vipengele vilivyosalia.

Badilika...
Inawezekana wewe ndiye uliyekosea, yamkini pia ni mwenzi wako ndiye mwenye makosa, vyovyote ilivyo, kikubwa cha kuzingatia hapo ni kwamba, tayari mpo kwenye matatizo ambayo wewe umeshayagundua na upo tayari kuyasahihisha.

Badilika kifikra. Kama ulikuwa una majibu mabaya, anza kumjibu vizuri. Hata kama yeye ndiye mwenye makosa, haijalishi maana hapa sasa unatafuta amani ya nyumba yenu. Mtazame kwa picha tofauti, ondoa fikra za upungufu wa msisimko kwake.

Matayarisho ya akili yatakusaidia wakati ukielekea kwenye kutafuta suluhu ya kudumu ya tatizo lako/lenu.

Matendo yazungumze!
Kichwa chako kikishakuwa fiti, sasa unatakiwa kuanza mashambulizi ya kurejesha msisimko ndani kwa kuonyesha vitendo.

Kuna wanawake ambao hujisahau baada ya kuingia kwenye ndoa na kupata mtoto/watoto. Kutwa, kucha utakuta wapo makini na watoto wao. Wameshasahau kuwa wana waume ambao ndiyo sababu ya watoto hao.

Hilo ni tatizo. Utakuta mwanamke anajiachia hivyo, hajali kama ana mume. Anabaki mchafu, mumewe akirudi anamkuta yupo hovyohovyo, tena muda mwingi akiwa na mwanawe, hataki ukaribu na mume wake, huo msisimko utatokea wapi?

Hili lipo hata kwa upande wa baadhi ya wanaume. Kwa kuwa ameshaoa kila kitu kinaisha. Hapangilii nguo vizuri, haendi saluni nk. Hilo ni tatizo. Kama alikupenda ukiwa mtanashati ni kazi yako kuhakikisha unadumisha utanashati wako.

Hata mnapokuwa mmelala chumbani, lala mkao wa kuonyesha ‘upo tayari kwa lolote’, maana kuna wengine, akilala ni kama anakuambia wazi kuwa, ‘sina mpango na kitu chochote’. Kwa wanandoa siyo sahihi.

Maliza tatizo
Baada ya yote hayo, sasa unatakiwa kuanzisha mazungumzo. Usikubali kukaa na matatizo muda mrefu, mazungumzo ni jambo la msingi zaidi.Kikubwa ni kutumia kauli nzuri, epuka maudhi kwa mwenzi wako ili mwisho wa siku muweze kumaliza tatizo bila kutofautiana zaidi. Nalisema hili, maana kuna wengine, wanataka kumaliza tatizo lakini ndani ya mazungumzo wanaruhusu kutokuelewana.

Boresha Kukaa kwa amani na upendo ni jambo zuri, kwa sababu mtakuwa mmeshajifunza kwa yaliyopita, ni wakati wenu sasa kuboresha uhusiano wenu. Hakikisha yale uliyoyafanyia kazi hapo juu unayaendeleza kila siku katika maisha yenu ya uhusiano.

Isiishie pale tu ulipokuwa ukihitaji kutafuta suluhu, badala yake sasa, hakikisha kila siku unazidisha ubunifu ili mwezi wako akuone mpya. Kauli nzuri, matendo mazuri, kuheshimiana, kusikilizana ni kati ya mambo muhimu ambayo yamesisitizwa mara nyingi sana na wataalam mbalimbali wa mambo ya uhusiano na ndoa.

Hata viongozi wa dini, wakati wakifungisha ndoa wamekuwa mstari wa mbele kuwafundisha wanandoa kuwa na mambo niliyoelekeza hapo juu.

NINI ZAIDI YA NENO; NAKUPENDA?
Onyesha kuna zaidi ya upendo kwa mwenzako kwa kumheshimu, kumpenda kwa dhati, kumsaidia anapokuwa na matatizo, kuunganisha familia na mengine yanayozidisha upendo.
Kusema tu nakupenda, hakuna maana umeingia moyoni mwa mwenzako. Wako wengi tu hukutana klabu usiku, wanaambiana wanapendana, usiku wanalala pamoja halafu asubuhi kila mtu anachukua hamsini zake.

Kuna kitu zaidi ya neno, nakupenda. Dhihirisha basi kwa matendo. Kusema tu I love you, wakati matendo yako yanatafsiri unamdharau mpenzi wako hakuna maana yoyote na mwisho wake kila siku utabaki ukilia mapenzi yanakutesa!

Kazi ni kwako rafiki yangu.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers.
Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa

No comments: