ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 15, 2014

Wakuu wa wilaya wazozama hadharani

Rais Jakaya Kikwete

Ziara ya Rais Jakaya Kikwete iliyopangwa kufanyika mwezi ujao mkoani Mbeya imezua mtafaruku kufuatia Mkuu wa Wilaya ya Momba, Abiud Saideya na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Dk. Michael Kadeghe kuzozana hadharani na kutaka kuzipiga kutokana na mzozo uliotokana na maandalizi ya ziara hiyo.

Tukio hilo limetokea juzi asubuhi mjini Mbozi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Momba kufika nyumbani kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi kwa lengo la kutaka kufanya ukaguzi sehemu ambako atafikia Rais.

Inaelezwa kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa serikali, Rais akifanya ziara katika mkoa au wilaya hulazimika kulala ikulu ndogo ambayo inakuwa ni nyumba ya Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya husika.

Mtafaruku huo ulifuatia agizo la ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya kwamba kwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Momba hana sehemu ambako Rais anaweza kufikia kwa ajili ya malazi hivyo asaidiane katika maandalizi na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, ambake ipo ikulu ndogo.

Taarifa ambazo NIPASHE imezipata kutoka kwa chanzo cha uhakika zimeeleza kuwa kutokana na agizo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Momba, mapema asubuhi alikwenda nyumbani kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi kwa lengo la kwenda kufanya ukaguzi sehemu ambako angefikia Rais.


Mkuu wa Wilaya ya Momba, Saideya baada ya kufika tu Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Kadeghe alianza kuhoji ni kwanini mwenzake (DC Momba) anakwenda kufanya ukaguzi wa kushtukiza bila kumpa taarifa.


Taarifa zinaeleza kuwa wakuu hao wa wilaya inadaiwa walianza kuzozana na kutoleana lugha zisizo na staha hali ambayo kama isingekuwa baadhi ya maofisa wa serikali waliokuwepo eneo la tukio kuingilia kati, viongozi hao wakuu wangeweza kushikana mashati.

“Ilikuwa hali mbaya. Mabosi wetu (wakuu wa wilaya) walipoanza kurushiana maneno machafu, ikabidi tufanye jitihada za kuwasuluhisha wasiweze kupigana,”kilisema chanzo chetu.


Taarifa zinaeleza kuwa wakati wa mabishano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Momba alimweleza mwenzake Mkuu wa Wilaya ya Mbozi kwamba yeye ana uzoefu na mambo ya uongozi kwani wakati akifundisha Chuo Kikuu, yeye alikuwa tayari ana cheo hicho cha ukuu wa wilaya.


Taarifa zaidi zinaeleza kuwa wakuu hao wa wilaya kwa muda mrefu wamekuwa hawana mahusiano mazuri licha ya kwamba wilaya zao ni jirani.

Tangu Rais agawe wilaya mpya, Mkuu wa Wilaya ya Momba ambayo iligawanywa kutoka Wilaya ya Mbozi, amekuwa akitekeleza majukumu yake kwa kutumia ofisi za wilaya ya Mbozi, ambazo zipo katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi.

Mkuu wa Wilaya ya Momba, Saideya, akizungumza na NIPASHE kwa simu kutoka Mbeya, alithibitisha kwenda nyumbani kwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi kufanya mazungumzo kwa ajili ya ziara ya Rais anayotarajia kuifanya katika mkoa wa Mbeya hususani wilaya hizo.

“Nani ambaye amekwambia hayo wakati hukuwepo eneo la tukio? Nikeleze tu, mimi kweli nilikwenda pale nyumbani kwa DC Mbozi... tumeongea (na), tumekubaliana vitu gani vinahitajika kufanyika na kwamba tunasubiri kikao kingine na tumeteua watu wa kusimamia suala hilo,”alisema.

Saideya ambaye wakati akizungumza alikuwa akisitasita, alisema suala la kwamba ametupiana maneno machafu na mwenzake (DC wa Mbozi) halina maana isipokuwa wamekubaliana masuala ya msingi kwa ajili ya ziara ya Rais.

“Kimsingi, maandalizi yanaendelea vizuri na kama kuna masuala hayo mengine unaweza kuwasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya sababu yeye ndiye msemaji wa suala la ziara ya Rais,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Kadeghe, alipotafutwa alikiri kukutana na Mkuu wa Wilaya ya Momba kwa ajili ya kupanga mipango ya ziara ya Rais anayotarajia kuifanya mwezi ujao mkoani Mbeya.

“Wewe ni mwandishi wa habari... unajua protokali za nchi. Ni kweli tulikuwa naye Ikulu ndogo, lakini mambo ya ikulu hayazungumzwi mahali popote. Hivyo siwezi nikazungumza kilichokuwa kimetokea hapo,” alisema DC huyo na kukata simu.
SOURCE: NIPASHE

No comments: