Kifo cha Gotrum Mapunda aliyefariki kwa radi mkoani Ruvuma akiwa ameketi chini ya mwembe na wenzake kimezua utata kikihusishwa na imani za kishirikina.
Marehemu Mapunda wa kijiji cha kijiji cha Lilahi alifariki katika Kituo cha Afya Muhukulu ambako aliwahishwa kwa ajili ya matibabu.
Jambo la ajabu katika tukio hilo ni kuwa hakuna hata mmoja katika wenzake aliyokaa nao aliyeathirika hata kwa jeraha dogo.
Kutokana na mazingira hayo, baadhi ya ndugu, jamaa na rafiki, akiwemo mtoto wa marehemu, wametia shaka kuwa sio radi iliyomuua.
Mmoja wa mashuhuda ambaye pia ni shemeji wa marehemu, Said Kasasu, alisema marehemu alifika eneo ilipotokea ajali na walikaa pamoja na wenzake kupiga soga lakini jua lilipoongezeka walihamia chini ya mwembe.
Alisema saa nane akiwa ameenda kumhudumia mteja dukani, akasikia kitu kama kimepasuka na alipoka nje alimwona baba yake mzazi na wengine waliokuwa pamoja na Mapunda wamekimbilia eneo lilipo duka lake.
Kasasu alisema upande ulipo mwembe alimuona Mapunda akiwa mahututi ameanguka chini amelala kifudifudi, amebadilika akionekana akiwa hajitambui.
Kasasu alisema walimuingiza ndani na kujaribu kumpepea lakini hakuzinduka ndipo walipoamua kumpeleka Kituo cha Afya, ambako dakika chache baada ya kumfikisha waliambiwa amefariki.
Mmoja wa watoto wa marehemu, Edson Mapunda alisema ushahidi aliyouona haumjamridhisha kuwa kilichomuua baba yake ni radi.
Edson alidai ingawa hakuwepo, mashuhuda walimwambia hawahusikia mlio wowote kabla marehemu kuanguka.“Nikijaribu kuangalia mazingira pale hayaoneshi kama kulipiga radi pale ingawa mi si mtaalamu wa hayo mambo kwa uelewa wangu mdogo hakuna viashiria hivyo,” alisema Edson.
Edson alisema eneo hilo ambalo kinachosemekana radi ilipiga, kulikuwa na miti na mizizi lakini hakuna kilichodhurika.
“Lakini pia mwili kwa uelewa wangu mdogo hauna viashiria hivyo kwa sababu mimi naamini radi ni kama umeme kwa hiyo huwa unamuunguza mtu kabisa,”mtoto huyo wa marehemu alifafanua.
Hata hivyo, kauli ya Ofisa Muuguzi Msaidizi Kituo hicho cha Afya Muhukulu, Samson Ngakama aliyethibitisha kifo hicho, inapingana na maelezo hayo.
Ngakama alisema walimpokea mgonjwa huyo majira ya saa tisa akiwa katika hali ya koma na akafariki muda mfupi baadae huku mwili ukionesha dalili zote za mtu aliyepigwa na radi.
“Radi ilipiga sehemu ya mgongo lakini iiliunguza upande wa kifua, upande wa chini wa tumbo inaweza kupunguza nguo ambayo aliweza kuivaa ni shati ilipungua upande wa nyuma lakini pia upande wa mbele,” alisema Dkt Ngakama.
Naye Diwani wa kata ya Muhukulu Saimon Kapinga amewaasa wananchi waache imani potofu.
“Niwaambie tu wananchi hiki ni kifuku. Na radi kifuku sio kitu cha ajabu. Kwangu mimi naamini safari yake ya maisha hapa duniani nadhani ilikuwa imefikia mwisho. Mungu anapanga yoyote namna gani ataondoka katika dunia hii,” alisema.
No comments:
Post a Comment