Mwenyekiti wa CUF Ibrahim Lipumba akizungumza na waandishi wa gazeti hili. Picha na Edwin Mjwahuzi
Dar es Salaam. Wakati mchakato wa Katiba mpya unaendelea mjini Dodoma na suala la theluthi mbili likisumbua vichwa vya wengi, mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameeleza kuwa kura za wajumbe 14 kutoka Zanzibar ndizo zitauokoa au kuukwamisha mchakato huo.
Profesa Lipumba alikuwa kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam kuhusu mustakabali wa mchakato wa Katiba baada ya kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia kuhudhuria vikao.
Kundi hilo lilisusia vikao Aprili 16 kwa madai kuwa Bunge lilipoteza mwelekeo kwa kuacha kujadili Rasimu ya Katiba, hasa katika suala la muundo wa serikali ya Muungano na kwamba chama tawala, CCM kiliingiza suala la serikali mbili ambalo halimo kwenye rasimu hiyo badala ya serikali tatu.
Kutokana na uamuzi wa Ukawa, ambayo inaundwa na wajumbe kutoka CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na baadhi wa kundi la 201 kutoka taasisi mbalimbali za kijamii, kuna shaka kwamba mchakato huo huenda usifanikiwe kutokana na ukweli kuwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inataka uamuzi upitishwe na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Bara na idadi kama hiyo kutoka Zanzibar.
Kutokana na utashi huo wa kisheria, Profesa Lipumba alisema wana uhakika kuwa Katiba haitapita kwa kuwa wanao wajumbe 14 kutoka kundi la 201 ambao ndiyo tegemeo lao.
“Sisi tunao wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar wa vyama vyetu ambao hawakwenda hata kwenye vikao. Tukiwajumlisha, tunahitaji watu 14 kutokana na wale wajumbe 77 (wa Zanzibar) wa Kundi la 201 na kule tuna uhakika wa watu kama 21,” alisema.
“Wapo baadhi waliokwenda kuhudhuria vikao, lakini tunajua misimamo yao. Tunajua kuna mbinu zinafanyika kuwarubuni, lakini tunawafuatilia kwa karibu.”
Alisema kuwa Ukawa wana uhakika pia wa kuungwa mkono na wabunge na wawakilishi wa CCM kutoka Zanzibar katika kutetea mamlaka ya Zanzibar.
“Kama mnafuatilia mazungumzo ya Baraza la Wawakilishi, katika malalamiko ya suala la Muungano, mazungumzo ya CUF na CCM yalikuwa yanafanana na hata ule waraka uliopelekwa bungeni kutoka CCM Zanzibar ambao sasa wanaukana, unataka mamlaka tatu. Maana yake nini? Mamlaka ni Serikali,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Hata kura zitakapopigwa, CCM hawawezi kupata theluthi mbili za upande wa Zanzibar. Suala la Katiba ni suala la maridhiano.”
Aitetea Tume ya Jaji Warioba
Huku akitetea uamuzi wa Ukawa kutoka nje ya Bunge la Katiba, Profesa Lipumba ametaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na rasimu iheshimiwe kwa kuwa imefanya kazi kubwa.
“Pamoja na kwamba kila kundi lilikuwa na mambo yake katika Katiba, yale mambo ya msingi yaliyoletwa na Jaji (mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Joseph)Warioba na Tume yake tuyasimamie na yaongoze mchakato wa Katiba. Ukiisoma rasimu ile kwa kweli utaona Tume hiyo imefanya kazi kubwa,” alisema Profesa Lipumba.
Amewataja makamishna wa iliyokuwa Tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba akisema kuwa utaalamu wao ndiyo umezingatia umuhimu wa muundo wa serikali tatu.
“Kati ya wataalamu waliobobea katika Katiba ni pamoja na marehemu Dk Sengondo Mvungi na Profesa Palamagamba Kabudi. Siyo Profesa Issa Shivji (namheshimu sana huyo, kwani ameandika mengi kuhusu Zanzibar kwamba imebanwa sana),” alisema.
“Lakini, utaalamu wa Profesa Shivji ni sheria za kazi. Ni msomi mwenye uelewa mpana… lakini wanafunzi wake ni wataalamu wa masuala ya Katiba ambao ni Dk Mvungi na Profesa Kabudi ndiyo wameona hivyo.
“Hawa ni wazalendo. Huwezi ukahoji uzalendo wa Jaji Warioba, Jaji Augustino Ramadhani, Joseph Butiku, Dk Salim Ahmed Salim na wengineo.”
Utata Bunge la Katiba, NEC
Lipumba amesisitiza kuwa hata Bunge hilo likiendelea na vikao vyake, bado Katiba ya wananchi haitapatikana kwani haitakuwa na maridhiano ya kisiasa.
“Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakar Bakari hayumo katika Bunge Maalumu, unajadili vipi Katiba? Huwezi kupata Katiba bila maridhiano ya kisiasa ya Wazanzibari, hakuna maridhiano ya kisiasa. Kwa hiyo, tunataka mchakato usitishwe,” alisema.
Kwa upande mwingine, Profesa Lipumba alisema kuna mikanganyiko mingi katika Bunge hilo pia kukiwa na utata wa kufanyika kwa kura ya maoni kutokana na maandalizi hafifu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
“Tume ya Uchaguzi ilivyo sasa, hata Daftari la Wapigakura wanasema hawana, wameshafuta vitambulisho vya kupigia kura. Wanasema wataliandaa ifikapo Septemba wakati hadi tufikie kwenye Uchaguzi Mkuu 2015 tuna mwaka mmoja,” alisema.
Aliongeza: “Halafu wanachanganya mambo, leo utasikia mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samuel Sitta anakutana na jamii ya wafugaji. Kwamba wafugaji hawamo kwenye rasimu?
“Tunafahamu Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeeleza katika ripoti zao kwamba mambo hayo yote walikuwa nayo, lakini hawakuyaweka kwa kuwa hii ni Katiba ya Muungano.
“Mambo ya ardhi, serikali za mitaa hayakuwekwa. Sasa, utaletaje mambo ya Tanzania Bara yaamuliwe na Wazanzibari wakati wana Katiba yao? Hata ile mantiki iko wazi tu,” alisema Profesa Lipumba.
Rais Kikwete msahaulifu
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kusimamia ahadi zake, hali inayochangia kupwaya kwa utawala wake.
Akifafanua hoja yake, mwanasiasa hiyo alisema, “Katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka 2011 ambapo pia alianzisha mchakato wa Katiba, alisema kutakuwa na kituo cha kufua umeme cha megawati 300, kutakuwa na Kinyerezi (I) ya megawati 200, megawati nyingine 200 za makaa ya mawe na uzalishaji wa umeme kwa upepo.
“Hadi sasa imeshapita miezi 36, hakuna hata kimoja alichomaliza kukitekeleza, kituo cha kufua umeme cha Kinyerezi (I) kinaendelea kujengwa.”
“Kwa jumla, Kikwete ameshapoteza dira ya maendeleo kwa kipindi cha miaka tisa alichokaa madarakani, hivyo sioni cha kumshauri. Alisema tangu Kikwete aingie madarakani, hakuwa na ajenda maalumu ya maendeleo, ndiyo maana nchi imeendelea kuwa maskini.
“Kwa sasa, Rais Kikwete amebakiza muda wa mwaka mmoja, hakuna la kutegemea. Kwanza, hakuwa na mtazamo au dira ya kufanikisha mambo, kwa hiyo kwa mwaka huu mmoja huwezi kutegemea kuwa ataleta mabadiliko makubwa,” alisema Profesa Lipumba.
Profesa Lipumba, akirejea utawala wa kiongozi wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, alisema kuwa utawala wa Kikwete umeshindwa kuwa na nidhamu ya fedha kiasi cha kuzorotesha uchumi.
“Ili uweze kusimamia maendeleo ya nchi yetu, ni lazima uwe na matumizi mazuri ya fedha za umma na uwe na Serikali inayosimamia vizuri matumizi na malengo yaliyowekwa,” alisema msomi huyo wa nyanja ya uchumi.
“Rais Mkapa alikuwa na nidhamu ya utendaji wa Serikali kibajeti, kwa sababu alikuwa akitumia bajeti ya fedha taslimu. Ilitumika kuleta nidhamu kwa kuwa fedha zilizokuwapo, ndizo zilizotumiwa.
“Tatizo kubwa ambalo limejitokeza katika kipindi hiki… Bajeti kwa ujumla wake, ule mgawanyo wa kila wizara haukuwa na mwongozo mzuri wa nini Serikali itatekeleza. Tatizo hilo lilikuwa ni muhimu kwa awamu ya mwanzo kuleta nidhamu katika matumizi ya ujumla yalingane na mapato, lakini hilo jambo limeendelea mpaka leo.”
Kuondokana na umaskini
Ili kuondokana na umaskini nchini, Profesa Lipumba alishauri Serikali kukubali kuwekeza katika huduma za jamii, zikiwamo elimu na afya huku rasilimali nyingine zikifuata.
“Ukizungumzia mambo ya afya katika hotuba, si jambo utakalopigiwa makofi, lakini ndilo jambo linalosababisha umaskini, yaani watoto na kinamama kukosa lishe bora.
“Kwa takwimu za sasa, asilimia 42 ya watoto wa Tanzania wana utapiamlo, wamedumaa. Kwenye ‘Big Result Now’ (Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa), sekta ya afya haimo, nimebaki nastaajabu,” alisema.
Huku akitaja utajiri wa dhahabu kama mojawapo ya rasilimali zilizopo nchini, alisema Serikali haiko wazi katika mapato yake, badala yake imejikita zaidi katika kodi ya bidhaa ndogo ndogo.
“Tumejaliwa kuwa na rasilimali za asili. Tuna dhahabu, lakini ukisikiliza hotuba ya bajeti kila mwaka huwezi kusikia wakizungumzia tumepata kiasi gani katika sekta ya madini. Tunarudi kule kwenye sigara na bia na konyagi,” alisema.
“Tumegundua gesi, lakini hatuna mikakati inayoeleweka,” alisema.
. Kuna gesi imegunduliwa katika maji mafupi ndiyo hiyo ya Msimbati, Mnazi Bay na Songosongo iliyoko kusini mwa Tanzania ambayo ilitakiwa itumike kuzalisha megawati 300 za kuingiza gridi ya Taifa, lakini haikufanyika.”
“Sasa kuna gesi ya kina kirefu... lakini ukiangalia mkataba wa mfano ulioko kwenye tovuti ya TPDC, unasema Serikali itakuwa inapata asilimia 80 hadi 90. Lakini, mkataba halisi uliotolewa na (kampuni ya utafiti na uchimbaji mafuta) Statoil, unaonyesha kuwa Serikali itapata chini ya asilimia 50, hatuna uwazi katika mapato ya gesi,” alisema.
Aliongeza kuwa licha ya Kampuni za China kujenga bomba la gesi, bado hata mikataba yake haiko wazi hata kwa wabunge ili waweze kuhoji.
Aliitaka Serikali kuweka mikakati endelevu ya kufaidika na gesi ikiwa pamoja na kuihakiki ili kuhakikisha kuwa ina faida kwa Watanzania.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake