Tuesday, August 12, 2014

Mauaji

  Sungusungu wadaiwa kuwaua raia kwa kipigo
  Mmoja wamchoma akiwa mfu, mwingine hai
Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa

Mauaji ya kutisha ya watu wawili, yanadaiwa kufanywa na kundi la askari wa jadi maarufu kama Sungusungu wilayani Manyoni Mkoa wa Singida baada ya kuwatoa nyumbani kwao usiku, kuwapeleka kichakani ambako waliwashambulia kwa kipigo, kisha kumchoma mmoja akiwa mfu na mwingine akiwa bado hajakata roho.

Waliouawa katika tukio hilo lilitokea kwa nyakati tofauti usiku wa kuamkia ijumaa iliyopita katika kijiji cha Damwelu kata ya Ipande tarafa ya Itigi wilayani hapa mkoa wa Singida ni Lameck Joshua (31), mkazi wa kijiji hicho na Doto Kindai (20), wa mkoa wa Mbeya.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho, , Agustine Raphael, kundi la watu hao wanaokadiriwa kufikia 40 waliojitambulisha kuwa ni sungusungu, walifika nyumbani kwa Joshua na kugonga mlango kwa lengo la kutaka awafungulie.

Raphael alisema inasemekana Joshua hawafungulia, ndipo walipomtishia kuwa watamwagia nyumba yake petroli kisha kuilipua kwa njiti ya kibiriti.

"Baada ya tishio hilo Joshua alifungua mlango na kutoka nje na kukamatwa huku akizibwa macho kwa kufungwa usoni kwa kitambaa na baada ya hapo alipelekwa kwenye kichaka ambako alipigwa vibaya hadi kufa na mwili wake kuchomwa moto, " alisema.

Alisema baada ya kufanya mauaji hayo ya kinyama, sungusungu hao walikwenda nyumbani kwa Mapalala ambako nao walimkamata Kindai na kwenda naye kwenye kichaka hicho na kumshambulia kwa kipigo, kisha kummaliza kwa kumchoma moto.

" Taarifa zilizozagaa lijijini kwetu ni kwamba watu hao wameuawa kikatili kwa madai kwamba ni wezi wa mifugo.. hata hivyo serikali ya kijiji chetu haina taarifa kabisa juu ya watu hao kujihusisha na vitendo vya wizi wa mifugo." alisema na kuongeza kuwa:" Wameuawa kinyama, miili yao imeteketea na kubaini nyama kidogo na mifupa."

Katika hatua nyingine; Munge wa Manyoni Magharibi (CCM), John Paulo Lwanji amesema kuwa amepokea taarifa ya mauaji hayo ya kinyama kwa masikitiko makubwa.

Lwanji alisema kuwa analaani vikali wauaji hao kujichukulia sheria mkononi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Aliwataka wakazi wa jimbo hilo kujiepusha na vitendo vya kujichukulia sheria mkononi kwa sabababu vitawasababishia matatizo na usumbufu.
Alitoa wito kwao kuwa endapo watamhisi mtu au watu wanaojihusisha na vitendo hivyo viovu wasisite kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kwa upande wake Kamanda wa polisi Mkoa wa Singida, Geofrey Kamwela, alipotakiwa kuzungumzia mauaji hayo, aliomba muda zaidi ili aweze kujiweka vizuri na kutolea ufafanuzi.

Watuhumiwa watano wauawa Katika tukio jingine; watu wanne, wakiwamo raia watatu wa Kenya wameuawa kwa tuhuma za ujambazi katika kijiji cha Mriba tarafa ya Ingwe.

Kamanda wa Polisi Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa aliwataja waliouawa kuwa ni raia hao wa Kenya kutoka vijiji vya Ntimaro na Girabose wilaya ya Kurya East, Mwita Rugena (30), Rogona Nyamahoyi na Machera Marwa na Sagire Gachanga (25) wa kijiji cha Itiryo tarafa ya Ingwe wilayani Tarime Mkoa wa Mara.

Mambosasa alisema kuwa mauaji hayo yalitokea Agosti 8 mwaka huu baada ya watuhumiwa hao waliokuwa na silaha kukutwa na wananchi wakitaka kupora fedha na simu za wateja katika duka la Shadrack Mahenye kijiji hapo Agosti 3, mwaka huu na kuwajeruhi kwa risasi watu watatu.

Alisema baada ya taarifa hizo, polisi wakwenda katika eneo la tukio na kuwakuta watuhumiwa hao wameuawa kwa kushambuliwa kwa kipigo n a wananchi.

"Miili ya watu hao imehifadhiwa hospitali ya wilaya ya Tarime ikisubiri kuchukuliwa na ndugu zao. Kwa sasa tunawahoji watu nane kuhusiana na mauaji hayo,” alisema Kamanda huyo na kuwataja kuwa ni wakazi wa Kijiji cha Mriba.

Baba adaiwa kuuawa mwanawe
Wakati huo huo; Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamsaka Mkazi wa kijiji cha Kanji tarafa ya Kirua Vunjo wilaya ya Moshi Vijijini , aliyejulikana kwa jina moja la Maurice kwa tuhuma za kumuua mwanawe mwenye umri wa miaka minne, Nicholaus Maurice (4).

“Siku mbili kabla tulimisikia baba yake akitamka kwa jazba wakati akimuadhibu mwanawe kwa kuchelewa kupeleka kijiko ili ale chakula na mke wake," alidai mmoja wa watu kwenye familia hiyo na kuongeza kuwa:

" Nitakuuwa ili niishi na mke wangu vema na usinipotezee malengo bora ufe, sikuhitaji tena," Alisema kuna uwezekana wa baba huyo kuwa wakati akimuadhibu mtoto huyo alimnyonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo Agosti 10, mwaka huu saa 5 asubuhi.
Boaz alisema mtoto huyo alikutwa amefariki dunia baada ya kupigwa na baba yake mzazi huku mkono wake wa kushoto na makalio vikiwa vimevimba.

Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, mtuhumiwa huyo alitokomea kusikojulikana na kwamba polisi wanamsaka kwa udi na uvumba ili akamatwe na kufikishwa mahakamani.

Mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa hospitali ya Kilema ukisubiri kufanyiwa uchunguzi kisha kukabiliwa kwa ndugu kwa maziko.
“Inauma sana kuona mzazi unamchapa mtoto wako tena wa kumzaa paka umauti unamkuta, huu ni unyama. Tutahakikisha tunamsaka mzazi huyo popote pale alipo ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yake” alisisitiza Kamanda Boaz.

Vilevile alisema Agosti 9, mwaka huu majira ya saa 6:15 usiku, Nastori Christian (60), alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitali ya Huruma iliyopo Rombo- mkuu, wilayani Rombo baada kudaiwa kupigwa kichwani kwa fimbo na mtoto wake, Christofa Nestori(25).

Kamanda Boaz alisema chanzo cha mtoto huyo kuamua kumchapa baba yake huyo hakijajulikana, hivyo wanamshikilia kwa mahoajiano zaidi. Imeandikwa na Jumbe Ismailly, Singida, Samson Chacha, Tarime na Mary Mosha, Moshi.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment

bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake