NINA furaha sana moyoni mwangu maana ninakwenda kuzungumza na wewe kuhusu mambo muhimu sana katika maisha yetu ya kimapenzi.
Rafiki zangu, nazungumza juu ya kauli ambazo zina ishara mbaya kwenye uhusiano. Wakati mwingine unaweza kumsikia mpenzi wako akikuambia maneno ya ajabu sana, lakini usielewe maana yake ni nini.
Ngoja nikuambie, kila kinachotoka kinywani mwa mpenzi wako kukuambia wewe kina maana yake. Lengo ni kujifunza; kufahamu maneno hayo na maana zake. Wiki iliyopita tulianza na maneno, huvutii na hupendezi. Sasa tuendelee.
UNATOA HARUFU...
Mwenzi ambaye hana mpango tena na wewe, ataanza kukuonea kinyaa. Maneno ya kejeli kwake si suala la kujiuliza mara mbili. Ni rahisi sana kukuambia unanuka!
“Ebwanae unanuka jasho sana, hebu kaoge kwanza,” anaweza kukuambia hivyo.
Katika hali ya kawaida kabisa hii ni dharau, ila inawezekana labda mpo katika hatua ya kuelekea kwenye mahaba, lakini ulipomsogezea kinywa chako, ukakutana na maneno haya: “Aaaah! Mh...unanuka mdomo bwana, sitaki!”
Hizi si kauli njema na bila shaka anajaribu kukuonesha jinsi ambavyo umepungua thamani kwake. Huwezi kunuka kwa mpenzi wako, siku zote huwa unanukia, lakini kama ameona dosari yoyote na yeye kama mwenzi wako wa karibu ana wajibu wa kuhakikisha anatumia lugha nzuri kukurekebisha, lakini kwa kuwa hana mapenzi na wewe, hana haja ya kuonesha mapenzi yake, anakubwatukia atakavyo!
KUHUSU NDOA
Wengi wanapokuwa katika uhusiano wanakuwa na ndoto zao, lakini ni aghalabu kukuta mtu yupo kwenye uhusiano wa kula raha tu! Mara nyingi ndoto kubwa huwa ni ndoa, ingawa ni vyema kupeana muda wa kuchunguzana kwa muda mrefu zaidi kabla ya kufikia azimio hilo muhimu maishani.
Lakini unapokuwa na mpenzi wako faragha, kwenye mazungumzo au katika matembezi ya jioni halafu ghafla akakuambia hana mpango wa kuoa au kukuoa, ni kama anakupa tiketi ya kukuacha.
Pima kauli hii, kama anazungumza kwa mzaha utagundua na kama yupo ‘serious’ pia utajua. Angalia macho yake na namna anavyoweka mkazo kwa kauli yake hiyo.
Lakini hata kama hatakuambia hana mpango wa kukuoa lakini kusema kwamba hana mpango wa kuoa kwa muda huu (huo) nayo ni alama kwamba hana ndoto ya kuendelea nawe tena na kama ataendelea, anapoteza muda tu.
HUWEZI MAHABA...
Hii ni mbaya zaidi maana inagusa eneo ambalo wengi hawapendi kuonekana hawawezi! Unaweza kuwa naye chumbani, ukijitahidi kadiri uwezavyo kuhakikisha anafurahia, lakini ghafla unashangaa anakuambia hujui mambo!
Tena wakati anakuambia, anatamka kwa kumaanisha huku akitaka uongeze ujuzi maana muda wote mliokuwa naye hapo, ni kama mlikuwa mnacheza!
“Jifunze ubunifu, kila siku huwa unaniacha kama nilivyokuja...nikueleze tu ukweli kwamba, hujawahi kukata kiu yangu hata siku moja!” Kwa kauli hii, hapo una mpenzi tena jamani?
Tafakari anachokuambia, kama kinaingia akilini au la. Kwa kawaida kama umekosea, anatakiwa kukushauri, siyo kukukashifu.
Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
GPL
Bwana Joseph, tafadhali jaribu kuweka picha za weusi na kadhalika pale unapotoa maoni yako. Nasikitika kila nisomapo makala yako naona picha za wazungu tuu! Ili ushauri wako uwe na maana kwetu wadau ni vyema kama utatuonyesha wapenzi weusi au waarabu au wahindi (kwani ndiyo demografu ya Tanzania).
ReplyDelete