Kigoma/Songea/Arusha. Watu watatu wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya mtu anayesadikiwa kuwa ni jambazi, kurusha bomu ndani ya basi dogo aina ya Toyota Hiace lililokuwa likitoka Kilelema kwenda Kasulu, Kigoma.
Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kilelema, Benedicto Mahuta alisema tukio hilo lilitokea saa 11:00 alfajiri kwenye Pori la Kasesema, lililopo kati ya kijiji hicho na Kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Migongo, Wilaya ya Buhigwe.
Mahuta alisema wakati gari hilo likipita eneo hilo, mtu mmoja alionekana amesimama katikati ya barabara huku ameshika bunduki, hali iliyomlazimu dereva kuongeza kasi.
Alisema hatua 15 baada ya kumpita, walimuona mtu mwingine akiwa amesimama pembeni mwa barabara na baada ya kumpita, abiria waliokuwa wameketi nyuma ya basi hilo walishtukia kitu kizito kikitupwa ndani.
Mmoja wa abiria aliamua kukirusha nje lakini kililipuka na kusababisha vifo vya watu wawili na mtoto mdogo.
Mmoja wa abiria walionusurika, Mwalimu wa Shule ya Msingi Kilelema, Augustino Mkubhaka alisema baada ya mlipuko huo, gari lilipelekwa katika kambi ya JWTZ kwa ukaguzi.
Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Buhigwe, Samwel Utonga alisema inasadikiwa kuwa watu waliorusha bomu hilo ni majambazi wanaotokea nchi jirani.
Dereva wa jaji EACJ auawa
Dereva wa mmoja wa majaji wa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Ibrahim Msagati amefariki dunia kwa kupigwa risasi iliyofyatuka kutoka kwenye bastola ya mlinzi wa jumuiya hiyo.
Tukio hilo lililoibua majonzi na simanzi miongoni mwa wafanyakazi wa EAC lilitokea jana saa saba mchana muda mfupi baada ya kikosi cha ulinzi cha Jumuiya kumtia mbaroni mtu mmoja aliyefika Makao Makuu ya EAC kwa tuhuma ambazo hazikujulikana mara moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema tukio hilo ni la bahati mbaya kwani risasi ilifyatuka kutoka kwenye silaha ya mmoja wa maofisa usalama wa EAC.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma wa EAC, Richard Otieno-Owora alimtaja ofisa usalama ambaye risasi ilifyatuka kutoka kwenye bastola yake kuwa ni Jackson Oula.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, mmoja wa wafanyakazi wa Sekretarieti ya EAC alisema risasi hiyo ilifyatuka wakati ofisa huyo akijaribu kutoa simu maalumu ya kiusalama waliyotumia kunasa mawasiliano ya mtu waliyemtia mbaroni ili kuwapa ushahidi polisi waliokuwa wakichukua maelezo yao.
“Wakati akitoa simu mfukoni, risasi aliyoiweka chemba wakati wa kumtia mbaroni mtuhumiwa ilifyatuka na kutoboa kiti alichokalia mfanyakazi mwenzetu na kumpiga mgongoni na kusababisha kifo chake,” alisema.
Dereva huyo aliajiriwa hivi karibuni na alikuwa akiendesha gari inayotumiwa na Jaji Mfawidhi wa EACJ, Jean-Bosco Butasi.
Amchoma kisu mpenziwe
Mkazi wa Mandepwende, Ally Hassan (29) amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma baada ya kumchoma kisu shingoni mpenzi wake aliyetambulika kwa jina la Zamda Rashid (19) na kisha kujichoma kisu tumboni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema tukio hilo lilitokea jana saa tano usiku katika Kijiji cha Mandepwende baada ya kutokea ugomvi baina yao wakiwa nyumbani kwa mwanamume huyo.
Alidai kuwa katika ugomvi huo, Ally alimchoma kisu cha shingo na alipoona ameanguka chini akiwa ametapakaa damu alidhani ameua, hivyo naye aliamua kujichoma kisu cha tumbo ili kujiua lakini alipoteza tu fahamu baada ya kupoteza damu nyingi.
“Baada ya kujichoma kisu, wasamaria waliwahi na kumwahisha katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma ambako yeye pamoja na mpenzi wake wamelazwa na wanaendelea na matibabu.”
Mihayo alisema polisi wanaendelea kuchunguza tukio hilo na upelelezi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.
Imeandikwa na Diana Rubanguka (Kigoma); Peter Saramba na Mussa Juma (Arusha) na Joyce Joliga (Songea). wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment