ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 15, 2014

TANZANIA MWENYEJI WA MASHINDANO YA 8 YA MAJESHI YA AFRIKA MASHARIKI.

Mkuu wa Bregedi ya Nyuki ambae ni Makamo Mwenyekiti wa michezo ya Majeshi Bregedia Jenerali Sharif Sheikh Othman akizungumza na waandishi wa habari kuhusu michezo ya nane ya Majeshi ya Jumuia ya Afrika Mashariki. Mkuta huo umefanyika huko Bregedi ya Nyuki Migombani Zanzibar.
Waandishi wa Habari kutoka vyombo tofauti wakimsikiliza Bregedia Jenerali Sharif Sheikh Othman (hayupo pichani) katika Mkutano wake na wandishi leo. 
Mkurugenzi wa ufundi wa mashindano hayo upande (JWTZ) Luteni Kanali Joseph Bakari akitoa ufafanuzi wa Michezo hiyo. 
Na Miza Othman Makame Maelezo- Zanzibar .
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohammed Shein anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika ufunguzi wa Michezo ya nane ya Majeshi ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki itafanyika Zanzibar kuanzia tarehe 18 mwezi huu.

Akitoa Taarifa ya Mkuu wa Majeshi ya Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Makao Mkuu ya Brigedi Migombani kwa waandishi wa Habari, Mkuu wa Brigedi hiyo Brigedia Jenerali Sharif Sheikh Othman amesema lengo la michezo hiyo ni kujenga mashirikiano kati ya Majeshi na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema katika Michezo hiyo kutakuwa hakuna mshindi wala aliyeshindwa na wote watakuwa washindi, lengo ni kujenga uweledi na nidhamu ndani ya majeshi yetu.

“Hii ni fursa ya wanajeshi wetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kukutana pamoja kama tunavyofanya katika mazoezi ya pamoja ya kijeshi”, alisema Brigedia Jenerali Sharif Sheikh Othman.

Amezitaja Nchi za Jumuiya hiyo zitakazoshiriki Michezo hiyo kuwa ni wenyeji Tanzania, Burundi, Rwanda, Kenya na Uganda. Amesema Michezo itakayochezwa na wanajeshi hao ni Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete, Mpira wa Mikono, Mpira wa Kikapu na Mbio za nyika na ameelezea viwanja vitakavyofanyika kwa ajili ya michezo hiyo Polisi ziwani ,Vyuo vya Mfunzo Kilimani, JKU Saateni, Pamoja na Viwanja vya Zimamoto na Uokozi.

Brigedia Jenerali Sharif Sheikh ambaye pia ni Makamo Mwenyekiti wa Michezo hiyo, amewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi katika kuona vipaji vitakavyoonyeshwa na wanajeshi kutoka Nchi hizo .

Akitoa ufafanuzi wa Michezo hiyo Leftinenti Kanali Joseph Bakari amesema pamoja na micheo hiyo kutakuwa na Burudani ya Ngoma za Utamaduni kutoka Vikosi vya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Amesema jumla ya wanamichezo 505 wakiwemo Viongozi kutoka Nchi hizo watashiriki michezo hiyo itakayodumu kwa muda ya wiki mbili.

No comments: