Advertisements

Tuesday, August 26, 2014

Tanzania yaomba kuandaa Afcon 2017

Tanzania imeomba kuandaa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2017, baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuiondoa Libya, iliyokuwa imepangwa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

CAF ilitangaza kuiondoa Libya kutokana na kukumbwa na machafuko ya kisiasa nchini humo yaliyosababisha kutokuwa na serikali imara.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa (TFF), Selestine Mwesigwa, alisema wametumia nafasi hiyo kuomba kuwa wenyeji wa Afcon 2017.

Mwesigwa alisema uamuzi huo ulifikiwa na kupitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF, iliyokutana juzi Dar es Salaam kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali.

Katibu huyo alisema tayari wamewasiliana na serikali na walitarajia kutuma maombi hayo jana CAF na kwamba wana imani kubwa ya kukubaliwa, kutokana na kuwa na sifa za kuandaa fainali hizo.

Alisema miundombinu walionayo inatosha wao kuandaa fainali hizo, hasa ikingizatiwa uwapo wa usalama wa kutosha hapa nchini.Endapo Tanzania itapata nafasi hiyo ya kuandaa michuano ya Afcon, itafuzu moja kwa moja kushiriki kinyang'anyiro hicho kwa sifa ya kuwa timu mwenyeji.

Hiyo itakuwa mara ya pili kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo katika historia yake kwani mara mwisho kucheza fainali hizo ilikuwa 1980 wakati huo ikinolewa na Joel Bendera ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, huku nahodha akiwa ni Rais Mstaafu wa TFF, Leodigar Tenga.

Katika hatua nyingine, Mwesigwa alisema katika kupinga upangaji wa matokeo kwenye mechi mbalimbali za mashindano, endapo akibainika mtu kufanya kitendo hicho atafungiwa maisha kutojihusisha na masuala ya soka.

Kadhalika Mwesigwa alisema Kamati ya Utendaji ya TFF, imemteua Boniface Wambura kuwa Mkurugenzi wa Mashindano wa shirikisho hilo, kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu.

Mwesigwa alisema nafasi aliyokuwa nayo ya Ofisa Habari na Mawasiliano ipo wazi na wametangaza ajira mpya kwa nafasi hiyo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: