ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, August 31, 2014

URAIS 2015:Nyuma ya pazia la Mizengo Pinda

Upole wake wahusishwa na utii kwa Rais JK
Hatua ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutangaza nia ya kuwania Urais wa Jamhuri ya Muungano katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeibua siri nzito kuhusu uwezo na utendaji wake.

NIPASHE Jumapili limefanya tathmini ya tangu kushika wadhifa huo Septemba, 2, 2008, baada ya kujiuzulu kwa mtangulizi wake, Edward Lowassa, ambaye pia anatajwa kutaka kuwania Urais.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanamuelezea Pinda kwa namna tofauti zinazohusisha uwezo na upungufu wake katika kuishika nafasi hiyo, ikiwa atateuliwa na CCM na kushinda uchaguzi huo.

Miongoni mwa maeneo yaliyobainishwa katika utafiti huo kwa wiki nzima, ni pale Pinda, anapotajwa kuwa ni mwanasiasa asiyekuwa na ‘rekodi chafu’ katika utumishi wake wa umma, ama mwenye kashfa zinazohusishwa na uhujumu uchumi wa nchi au matumizi mabaya ya rasilimali na ofisi za umma.

Mhadhiri wa Chuo cha Mtakatifu Augustine, Profesa Mwesiga Baregu, aliimbia NIPASHE hivi karibuni kuwa, inawezekana Pinda akawa muadilifu na asiyekuwa na kashfa za ufisadi, ameitumikia serikali yenye viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi kwa miaka mingi.


“Inawezekana akawa si fisadi, lakini amekuwa katika serikali iliyogubikwa na ufisadi hivyo kumuondolea sifa hiyo, bali angejiondoa ndani ya serikali na kisha kuingia tena, angeeleweka,” alisema Profesa Baregu.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT) tawi la Mwanza, Marwa Chacha Kisyeri, alisema Pinda anapaswa kupimwa kiutendaji ili kubaini mambo aliyoyashughulikia, kuyasimamia na kuyatekeleza.

Hata hivyo, Kisyeri, alimkosoa Pinda kwa kauli zake hususani alizowahi kuzitoa bungeni akiashiria kuwaruhusu kuwapiga watu wanaokaidi kutii sheria.

UPOLE UNAOHUSIHWA NA UTII KWA JK
Imebainika kuwa tangu alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Pinda alikuwa mtiifu kwa Rais Kikwete, hali ambayo hata hivyo inatajwa kuwa ilichangia kumfanya aonekane kuwa mpole na asiyekuwa na uwezo wa kufanya maamuzi.

Pamoja na hatua hiyo, inaelezwa kuwa utendaji kazi wa mtangulizi wake (Lowassa) hasa kufanya maamuzi ya papo kwa hapo, ulikosolewa katika misingi ya uwajibikaji wa pamoja, hivyo Pinda (kwa uzoefu wake serikalini), asingeshiriki mfumo huo.

Mtaalamu wa sayansi ya jamii, Furaha Dimitrious, anasema katika uhalisia wake, mazingira ya utendaji kazi ambayo mtangulizi wake, Lowassa, alifanya maamuzi magumu yakiwamo yasiyowahi kutekelezwa na Rais Kikwete, isingekuwa rahisi kwa Pinda kufanya hivyo.

“Kama Pinda, angetumia nguvu na uwezo wake vinavyojulikana kwa walio wengi, lazima angejikuta katika mgongano na bosi wake, kitu ambacho kiutawala si kizuri na bila shaka na yeye aliongozwa hivyo,” anasema.

“Kwa hiyo Pinda si mpole kama watu wanavyoweza kuamini hasa katika kusimamia maslahi ya walio wengi, lakini kwa mazingira yaliyokuwapo wakati akiichukua nafasi hiyo, ilimpasa kuwa hivyo alivyo,” kinaeleza chanzo kingine ambacho hata hivyo, hakitaki kutajwa gazetini.

Utii wa Pinda, umebainika pia katika kauli zake nyingi zikiwamo alizowahi kuzitoa bungeni, akiahidi kushughulikia jambo baada ya kuwasiliana na Rais Kikwete.

“Hata alipokuwa akijibu maswali bungeni na kuahidi kutoa maelezo baada ya kuonana na Rais Kikwete, ilikuwa ni katika mazingira hayo, kwamba alijiweka kando dhidi ya kuzua mgongano na Rais,” kinaeleza chanzo kingine.

UHUSIANO WAKE NA WASTAAFU
Vyanzo tofauti vya gazeti hili vimebaini kuwa Pinda, amekuwa kiongozi aliyeweka rekodi ya kuwa na mawasiliano na uhusiano mzuri na watu wa kada tofauti ndani na nje ya serikali wakiwamo viongozi wastaafu wa ngazi ya kitaifa.

Inaelezwa kuwa, viongozi wastaafu hususani katika ngazi ya Taifa, wanastahili kutambuliwa kwa michango yao hata pale inapobainika kuwapo upungufu wakati wa utawala wao, jambo ambalo Pinda anatajwa kulithamini.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Pinda, amechangia kufanikisha mahitaji mengi ya viongozi hao wakiwamo waliowahi kuwa mawaziri wakuu, hali inayomfanya kuwa na sifa ya kutokuwa na kinyongo na kujikweza.

“Hata anapopigiwa simu na kiongozi mstaafu lakini akawa kwenye kikao, Pinda hulazimika kuwasiliana na kiongozi mhusika, tena kwa kutanguliza kuomba msamaha kwa kutopokea simu kwa wakati,” kinaeleza chanzo kingine.

KUTOJIVUNIA UTUMISHI WAKE IKULU
Miongoni mwa watumishi wanaotajwa kufanya kazi kwa miaka mingi kwenye Ikulu ya jijini Dar es Salaam, ni Pinda, ambaye hata hivyo kutokana na kutopenda makuu, anaelezwa kutoitumia fursa kutangaza mara kwa mara hadharani.

Chanzo chetu kimesema, “kuna watu wamefanya kazi na Rais Kikwete kwa awamu moja lakini kila kukicha wanajitangaza hadi kupitia mitandao ya kijamii, lakini Pinda, akitambua unyeti wa taarifa za Ikulu, hajawahi kusikika akizungumzia utumishi wake huko.”

MBIO ZA URAIS NDANI YA CCM
Mbali na Pinda na Lowassa, wanasiasa wengine wanaotajwa kutaka ‘kumrithi’ Rais Jakaya Kikwete, atakayeondoka madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwakani ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.

Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Mwigulu Nchemba, wabunge William Ngeleja (Sengerema) na Emanuel Nchimbi (Songea Mjini).

Pia wamo wanawake, Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Asha Rose Migiro na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka.

Lakini kuibuka kwa Pinda na ambapo hakukutegemewa na walio wengi, kunaelezwa na wachambuzi wa mambo ya siasa na chaguzi za mataifa, kwamba kumebadili upepo wa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 na fikra za raia.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

1 comment:

Anonymous said...

Pinda is a game changer