Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiongea na Wawekezaji wa Kampuni ya Chinalco ya nchini China waliokuja nchini kwa lengo la kujadiliana na Viongozi Waandamizi wa Wizara kuhusu fursa za uwekezaji hususan katika sekta ya madini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema Wizara yake imejipanga kuhakikisha inajengwa mitambo ya uchakataji madini (Mineral Processing Plants) hapa nchini ili kuondokana na utaratibu wa kusafirisha madini ghafi nje ya nchi na badala yake zisafirishwe bidhaa zitokanazo na madini husika ili kuongeza thamani na hivyo kukuza pato la nchi.
Aliyasema hayo alipokutana na kuzungumza na Wawekezaji wa Kampuni ya Chinalco ya nchini China waliokuja nchini kwa lengo la kujadiliana na Viongozi Waandamizi wa Wizara kuhusu fursa za uwekezaji hususan katika sekta ya madini.
“Tunahitaji kuwa na mitambo ya uchakataji madini hapa nchini hivyo nawashauri katika uwekezaji wenu mfikirie suala la kujenga mtambo husika kwani hatutaki kusafirisha madini ghafi nje ya nchi,” alisisitiza Profesa Muhongo.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Muhongo aliwashauri wawekezaji hao ambao walioambatana na Balozi wa China nchini, Mhe. Lu Youqing kuhusu fursa muhimu za uwekezaji katika sekta ya madini hapa nchini kuwa ni uwekezaji katika madini yaliyo katika kundi adimu (Rare Earth Elements), madini ya Shaba (Copper) pamoja na madini ya Dhahabu.
Aliwashauri wawekezaji hao kukutana na Wataalamu kutoka Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ambalo limepewa dhamana ya kusimamia maeneo yote ya uwekezaji katika sekta ya madini kwa niaba ya Serikali, ili kujadiliana kuhusu uwezekano wa kuingia ubia katika uwekezaji husika ikiwa ni pamoja na kupata maelezo ya kina kuhusiana na uwekezaji katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi aliwaeleza wawekezaji hao kuwa Tanzania inajulikana vizuri kwa kuwa na mazingira mazuri ya kijiolojia yanayofaa kwa uwekezaji hususan kwa madini kama dhahabu, vito, shaba, nickel na cobalt na kwamba aina ya miamba inayopatikana nchini inaruhusu madini ya aina nyingi kupatikana akitolea mfano Tanzanite ambayo inapatikana Tanzania pekee.
Aidha, aliongeza kuwa Tanzania inayo sera nzuri ya madini, utawala bora, hali nzuri ya kisiasa (political stability) pamoja na miundombinu bora, ambazo ni miongoni mwa sababu za msingi zinazovutia uwekezaji nchini.
Naye Kamishna wa Madini, Mhandisi Paul Masanja aliwakaribisha wawekezaji wa Kampuni ya Chinalco kuja kuwekeza nchini na aliahidi kuwapa msaada utakaohitajika ili kufanikisha azma yao hiyo ikiwa ni pamoja na kuwapa leseni ya kutafuta au kuchimba madini kwa wakati.
Awali, Mwenyekiti wa Kampuni ya Chinalco, Bw. Xiong Weiping akiinadi Kampuni yake kwa Viongozi wa Wizara alieleza kuwa, Kampuni hiyo ni mali ya Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China na inasimamiwa na Serikali Kuu na kwamba inajihusisha na masuala ya maendeleo ya rasilimali za madini, uchakataji wa madini ghafi na masuala ya kiufundi (technical & engineering services).
Alisema mkakati wa kampuni hiyo ni kuendelea kupanua shughuli za uzalishaji wa madini ya Aluminum, Shaba, Rare Earth Element na uongezaji thamani madini.
Ziara ya Kampuni hiyo nchini imekuja kufuatia ziara zilizofanywa awali nchini China kwa nyakati tofauti na Mhe. Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana katika Makao Makuu ya kampuni hiyo mapema mwaka jana na kuuomba uongozi wa kampuni hiyo kupanua mipaka ya biashara hadi Tanzania.
No comments:
Post a Comment