ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 26, 2014

Wahamiaji haramu 4,000 kutoka Malawi kupewa vibali

Mathias Chikawe
Serikali imesema itawapa kibali cha kuishi nchini, wahamiaji haramu zaidi ya 4,000 kutoka Malawi, walioorodheshwa katika operesheni maalum ya kuwaondoa, iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Aidha, Serikali imesema itawarudisha nchini kwao wahamiaji wote watakaokosa sifa za kupata kibali cha kuendelea kuishi nchini.

Akizungumza na NIPASHE, Afisa Uhamiaji wa mkoa,Grace Hokororo, alisema, mpaka sasa kinachosubiriwa ni Serikali kutoa fedha za kufanya zoezi hilo.


“Baada ya zoezi la kuwaorodhesha kumalizika, maamuzi ya serikali dhidi yao ni kuwapatia vibali vya kuendelea kuishi nchini kwa kuzingatia vigezo vitakavyoainishwa na atakayekosa vigezo atatakiwa kurudi kwao, zoezi ambalo litaanza baada ya kupewa taarifa ya kuanza kutoka makao makuu ya uhamiaji,” alisema Hokororo.

Serikali ilianza zoezi la utekelezaji wa operesheni ya kuwasaka na kuwarejesha makwao raia wa kigeni wanaoishi nchini bila kufuata sheria za nchi na zaidi ya wahamiaji haramu 3,000 walirudishwa makwao.

Wakati huo huo, Ofisi ya Uhamiaji Mkoa wa Dar es Salam inawashikilia watuhumiwa 13 wa uhamiji haramu walioingia nchini bila ya kuwa na kazi ya kufanya.

Wanaoshikiliwa ni watu nane kutoka India, wanne kutoka Nepal na Meneja wa hoteli waliyofikia iliyoko Kijitonyama, Manispaa ya Kinondoni.

“Watuhumiwa hawa ambao wanne ni wanajeshi kutoka nchini Nepal, tuliwakuta katika nyumba hiyo, tangu Jumamosi iliyopita bila ya wakala wao huyo kuwapo, wakiwa wanahudumiwa katika hoteli hiyo, ” alisema Hokororo.

 
SOURCE: NIPASHE

No comments: