Hao watoto hatujawaiba, tumewatoa kwao huko mikoani na biashara wanazofanya ni hizo ndogondogo wala siyo ngumu. Wengine hapa hawana baba wala mama wanazunguka tu mitaani. Wameona kuliko kuiba, ni bora waje wafanye kazi ili wapate pesa za kujikimu,” anasema Fatuma.
Pengine takwimu za Umoja wa Mataifa (UN) kwamba watoto wapatao milioni 250 wanatumikishwa katika ajira mbalimbali duniani kote, zikawa ndogo kulingana na hali halisi kwa kuwa kila kukicha, mapya huibuka.
Ajira hizi zinapaswa kupigwa vita kwa kuwa siyo tu zinawanyima haki za msingi watoto, bali zinachochea umaskini kwa familia na taifa kwa jumla.
Hassan Abdallah mkazi wa Tabata ni mmoja kati ya wanaoshiriki katika biashara hii haramu ya kuajiri watoto. Hivi sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kuajiri watoto 11 kwa kazi za kuuza vitumbua huku akiwahifadhi ndani ya chumba kimoja.
Kati ya waajiriwa hao, watoto walio chini ya umri wa miaka 18 wako wanane.
Katika makazi hayo, watoto walimwonyesha mwandishi wa habari hizi banda la mabati wanalotumia kwa malazi likiwa kando ya nyumba ya mwajiri wao.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kisukuru, Lukresia Msuya anasema kuwa Abdallah na mkewe Fatuma Shomari wamekuwa wakiwafuata watoto hao mikoani na kuwaleta jijini Dar es Salaam kuwatumikisha kuuza vitumbua mitaani.
“Tulipigiwa simu juzi na katibu wa CCM wa mtaa akisema kuwa kuna jambo la muhimu. Hapo ndipo aliponionyesha nyumba hii ambayo ina watoto wanaotumikishwa kuuza vitumbua. Tukawakusanya na kuwapelekapolisi,” anasema Msuya.
Amewataja watoto wanaoishi kwenye nyumba hiyo kuwa ni pamoja na Furaha Samuel, Steven Tudius, Amani Adison, Yusuf Simon, Richard Zakaria, Kackson Jackson Michael, Elia Wilson, Boniface Lawrence, Baraka Francis, Zamda Yumpunju, Jema Ramadhani na Haji Ramadhani.
Msuya amesema kuwa baada ya kupata taarifa hiyo, walikwenda kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kisukuru kisha kuhamishia shauri hilo Stakishari ambako Abdallah aliwekwa ndani.
“Nikiwa kama mzazi inaniuma kuona watoto hawa wadogo wenye umri kati ya 17 na 12 wakifanyishwa kazi kama hizi. Nawaomba wazazi wawakumbatie watoto kama vifaranga vya kuku. Mtoto wa miaka 12 umfanyishe kazi, halafu utamlipa nini kama siyo kumdhulumu?” alihoji.
Jinsi walivyokamatwa
Akieleza jinsi alivyogundua suala hilo, katibu wa CCM wa Mtaa wa Kisukuru, Thomas Matiku anasema kuwa alipewa taarifa na wananchi wakati akitoka Buguruni.
“Nilikuwa natokea Buguruni, nikakutana na vijana fulani, wakaniuliza, ‘wewe si unataka kugombea udiwani?’ utakuwaje diwani wakati watoto wetu wanatumikishwa kinyume na sheria na wewe unaangalia tu?’ Ndipo nilipowaomba wanionyeshe. Kumbe ni nyuma tu ya ofisi yangu,” anasema Matiku.
Anasema baada ya kupata taarifa hiyo, alimwita mwenyekiti wa Mtaa wa Kisukuru na ndipo walipomkamata mtuhumiwa huyo.
“Niliwaita watoto wawili ofisini kwangu na kuwauliza kinachoendelea. Walisema wako 11 wanalala chumba kimoja na kwamba kazi kubwa wanayofanya wakiamka saa 11:00 alfajiri ni kupika maandazi na vitumbua na kwenda kuuza maeneo ya Buguruni, Kariakoo na Ubungo,” anasema.
Akijibu tuhuma hizo shemeji yake Abdallah, Fatuma Shomari anasema wana lengo zuri la kuwasaidia watoto hao kujipatia kipato.
“Hao watoto hatujawaiba, tumewatoa kwao mikoani na biashara wanazofanya ni hizo ndogondogo wala siyo ngumu. Wengine hapa hawana baba wala mama wanazunguka tu mitaani. Hawa wameona badala ya kuiba, ni bora waje wafanye kazi ili wapate pesa za kujikimu,” anasema Fatuma.
Amekiri kuvunja Sheria ya Watoto lakini kwa lengo la kuwasaidia.
“Ni sawa tunavunja sheria, lakini kutokana na matatizo kwa wazazi wao, wanazurura tu. Sisi tumewaambia wakae hapa na familia zao zinajua. Wengine wameshindwa kwenda shule, wakasema ni heri kuliko kwenda barabarani kuombaomba na kuiba,” anasema.
Hata hivyo, Fatuma anakiri kwamba suala hilo lilishafikishwa Kituo cha Polisi cha Tabata na waliamriwa kuwarudisha watoto hao makwao.
“Ni kweli tulipewa siku tano na Polisi Tabata tuwarudishe hawa watoto, lakini ujue hawa ni watoto wanaohitaji maandalizi. Kabla siku tano hazijafika, tumekamatwa tena hapa,” anasema.
Naye mjumbe wa Shina Na.2 Mtaa wa Kisukuru, Halima Kombo amekiri kusikia tuhuma hizo, lakini hakuchukua hatua hadi lilipofikishwa ngazi za juu.
“Nilipata hizo taarifa na nimesikia majirani wakilalamika kuchafuliwa nyumba zao kwa moshi. Inasikitisha kwa sababu watoto hao wengi wanapaswa kuwa shuleni. Vijana hawa wanatakiwa kurudishwa makwao ili waendelee na shule,” anasema Kombo.
Anasema kuwa Abdallah na mkewe walihamia mtaa huo wiki mbili zilizopita wakitokea Tabata Kimanga ambako pia walikuwa wakiwatumikisha watoto kama hao.
Watoto nao wazungumza
Akizungumzia maisha yao, Steven Tudius alisema kuwa huamshwa alfajiri kisha hukabidhiwa mzigo wa vitumbua kwenda kuviuza.
“Nilikuwa nikiishi na bibi wilayani Kilosa ambako nilikuwa nikisoma Shule ya Msingi Chanzulu. Bibi akaniachisha shule baada ya tajiri yangu kuja kijijini akitafutawafanyakazi,” anasema Tudius.
Alisema: “Mimi huenda kuuza soko la nyama hapa Tabata. Tunalipwa Sh1,000 kwa siku na tunapewa chakula na kulala kwenyechumba kimoja.”
Naye Amani Adison mwenye umri wa miaka 22 anayeishi na kufanya kazi na watoto hao, anasema amelazimika kufanya kazi hiyo ili kuitunza familia yake.
Adison aliyetoka mkoani Dodoma alisema kuwa ameshafanya kazi za ndani wilayani Moshi Kilimanjaro, kisha akahamia Dar es Salaam ambako alifikia kwa mjomba wake eneo la Manzese mwaka 2013.
“Nilipofika kwa mjomba mwaka jana, akaniozesha mke. Wakati huo nilikuwa na pesa zangu kiasi cha Sh3 milioni. Mke wangu nimempeleka kwetu Dodoma, ndiyo nimekuja tena Dar es Salaam kutafuta fedha ili nimtunze mke na mama yangu,” alisema na kuongeza:
“Kwa sasa mama akiugua hana mtu wa kumsaidia zaidi yangu. Kuna dada zangu wawili wameolewa, lakini hawana uwezo, ndiyo maana mini nimekuja kutafuta maisha hapa.
“Nimeshafanya kazi za kuuza duka la mwarabu mmoja huko Tandika, ila Mwezi wa Ramadhani alituachisha ndiyo nimekuja hapa, leo hii ni siku ya tano.”
Alisema kuwa kwa mwezi anapata hadi Sh25,000 ambayo huigawa na kuituma nyumbani kwao Dodoma.
Naye Boniface Lawrence anasema mazingira ya kazi zao siyo mabaya kwa kuwa hakuna shida ya chakula.
“Kama Serikali inatusikia, basi itupatie ajira maana hapa Dar es Salaam usipokuwa na kazi utaitwa mtoto wa mbwa... ni kweli kipato chetu ni kidogo. Tunamwomba mwajiri wetu atuongezee mshahara ufike hata Sh50,000,” anasema Lawrence.
Wapelekwa Ustawi wa Jamii
Baada ya kufikishwa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari Ukonga, watoto hao wamekabidhiwa kwa maofisa Ustawi wa Jamii.
Ofisa wa Idara ya Ustawi wa Jamii, Manispaa ya Ilala, Lucia Chamwi amekiri kuwapokea watoto hao na kusema kuwa wanahifadhiwa kwa muda kabla ya kurudishwa kwao.
“Hata kama watoto walikuwa wakifurahia kufanyishwa kazi kwa kupata ujira, bado ni kinyume cha Sheria ya Haki ya Mtoto ya 2009, kwa kuwa wanakosa fursa ya masomo,” alisema ofisa huyo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki amekiri kuwa na taarifa hizo na kwamba mtuhumiwa amekamatwa na jalada lake limepelekwa kwa mwanasheria wa serikali.
Pia watoto hao wamekabidhiwa kwa Idara ya Ustawi wa Jamii.
Sheria ya Haki za Mtoto ya 2009. Sura ya 11 inazungumzia ajira yenye madhara kwa watoto:
“Mtu yeyote haruhusiwi kumwajiri mtoto katika shughuli yoyote inayoweza kuwa na madhara katika maendeleo ya afya, elimu, akili, mwili na maadili yake.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment
bila kutumia lugha ya matusi na kumharibia mtu siku
yake