ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 2, 2014

Yanga kupeleka timu B Kagame

Kocha mkuu wa Yanga, Marcio Maximo na msaidizi wake Leonardo Neiva wakiwa katika moja ya vipindi vya mazoezi vya timu hiyo, katika picha hii ya Maktaba.

Yanga ambayo ilitishia kujitoa, sasa itapeleka timu B na makocha wasaidizi katika michuano ya Kombe la Kagame la klabu bingwa ya Afrika Mashariki na Kati nchini Rwanda baadaye wiki hii, imeelezwa jijini.

Akizungumza katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari jijini jana, kocha mkuu wa Yanga, Marcio Maximo, alisema hatakuwepo kwenye Kombe la Kagame jijini Kigali.

Maximo aliyekuwa akizungumza baada ya mazoezi jijini Dar es Salaam, alisema yeye na kocha msaidizi mzawa, Salvatory Edward watabaki na kikosi kimoja cha Yanga Pemba kwa maandalizi ya ligi kuu ya Bara na Kombe la Shirikisho la klabu za Afrika la mwakani.

Kocha huyo ambaye anaingia mwezi wa pili wa mkataba wa miaka miwili wa kuifundisha Yanga, alisema kikosi cha Yanga kitakachokwenda Kigali kwa michuano hiyo inayoanza Ijumaa kitakuwa chini ya makocha wasaidizi Leonardo Neiva na Shadrack Nsajigwa.

"Kutakuwa na kikosi kitakachokwenda Kagame ambacho kitakuwa na mchanganyiko na vijana," alisema Maximo kabla ya kutoa ishara ya wazi zaidi kwamba Yanga itapeleka timu B Rwanda:

"Kikosi kingine kitakachokuwa na nyota wote wa kimataifa pamoja na wachezaji ambao wapo kwenye kikosi cha Taifa Stars tutakwenda kuweka kambi Pemba kujiandaa na ligi kuu," alisema Maximo ambaye aliwahi kuwa kocha wa timu ya taifa kwa miaka minne.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwapa nafasi ya kupata uzoefu wachezaji vijana pamoja na kuendelea na programu yake ya mazoezi kujiandaa na ligi kuu.

"Naamini wachezaji nitakaowatangaza kwenda Kigali watakwenda kushindana kwa kuwa wachezaji wote wa Yanga wana uwezo mkubwa wa kushindana na timu yoyote katika ukanda huu wa Afrika mashariki na Kati," alisema zaidi Maximo.

Alisema kuwa kikosi kitakachoenda Kigali kitaondoka nchini siku yoyote kabla ya Jumatano.

Wachezaji wa Yanga waliopo Taifa Stars ni Deogratius Munisi 'Dida', Nadir Haroub 'Canavaro', Kelvin Yondan, Simon Msuva na Mrisho Ngasa wakati wachezaji wa kimataifa wa klabu hiyo ni Hamis Kiiza, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Mbuyi Twite na Wabrazili wawili Genilson Santos 'Jaja' na Andrew Coutinho.

Yanga ilitishia kujitoa kwenye Kombe la Kagame wiki iliyopita kwa madai ya kutopatiwa taarifa rasmi na waandaaji wa michuano hiyo ya kila mwaka, shirikisho la soka la Afrika Mashariki na Kati, Cecafa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: