ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 2, 2014

‘Tuliacha milango wazi kumsubiri Merry’

Mtoto Merry na wazazi wake wakiwa na nyuso za furaha baada ya kupatikana. PICHA|RAPHAEL LUBAVA

Dar es Salaam. Tukio la mtoto Merryn Reppyson (4)  kutekwa kwa siku nane ni kama hadithi katika filamu ambayo inaweza kuchukua siyo chini ya saa tatu  kuhadithia. Ni hadithi ya kustaajabisha mithili ya sinema, lakini si ya kusadikika; ni ya kweli. Mtoto huyo aliibwa na swahiba mkubwa wa baba yake nyumbani kwao Changanyikeni na kwenda kufichwa Tandale kwa Mtogole.
Akielezea mlolongo mzima hadi kupatikana kwa mtoto wake, Baba mzazi wa Merryn,  Reppyson Ishabakaki anasema ‘Kupaza Sauti’ ndiko kulikosaidia mtoto wake akapatikana kwa vile angekaa kimya na vyombo vya habari visingeshikia bango, basi mwanae asingepatikana.
Tukio la kutekwa kwa mtoto wakel ilizizima nchi nzima kwa kuwa alijikuta akipigiwa simu na watu kutoka mikoa mbalimbali wakiwemo watu wakubwa ambao hakuwategemea.
“Siku ambayo mtoto alipotea nilikuwa kazini na nilichelewa kurudi, majira ya saa 12:30 jioni mke wangu alinipigia simu kuniambia kuwa mtoto hayupo nyumbani, nilishangaa sana, nikamuhoji hayupo nyumbani kaenda wapi wakati huwa hatoki nje akaniambia haijulikani: “Nikarudi nyumbani nilifika hapa kama saa 2:00 hivi usiku, nikakuta watu wengi nyumbani kwangu, kila mtu anaongea lake nikaenda kutoa taarifa kituo cha Polisi Chuo Kikuu. Nikawapa na picha ya mtoto. Hapo sasa majirani kila mtu akawa anahisi lake. Kuna msichana akasema alimuona ameongozana na kaka mmoja na kwa jinsi alivyokuwa amemuelezea wote, tukahisi ni kijana mmoja anakaa maeneo ya Makongo.
“Basi tukatoka kundi kubwa la watu kama 50 hivi tukaenda Makongo hadi nyumbani kwa huyo kijana. Mama yake akatuambia huyo mnayemulizia mbona amefungwa siku nyingi hayupo. Tukamwambia tuonyeshe picha yake akagoma, basi tukarudi tena mpaka hapa Changanyikeni tukaenda kumgongea mjumbe wetu tukamueleza, tukaondoka nae tena kurudi Makongo, ila safari hii mjumbe akasema si vema kwenda nyumbani kwa mtu bila ya mjumbe wake kujua. Basi mjumbe wetu akaenda kwa mjumbe wa Makongo akamgongea na muda ulikuwa umeshaenda hapo inakimbilia saa 5:00 usiku, ndio mjumbe wa Makongo akatuongoza mpaka kwenye hiyo nyumba.
Anasema walipofika waligonga kwa takriban nusu saa, lakini mlango haukufunguliwa na ndipo waliposhauriana kuvunja nyumba kwa sababu walihisi huyo mama alikuwa anamficha kijana wake.
“Tulivyosema masuala ya kuvunja nyumba, ndipo yule mama akafungua mlango,” anasema na kuongeza kuwa  baada ya majibizano sana, akakubali kuonyesha picha ya kijana wake. Lakini yule msichana aliyedai kumuona mtu aliyeongozana na mtoto, akasema sio mwenyewe baada ya kuiangalia picha.
“Ilibidi kumwomba msamaha yule mama na kumwambia kuwa shida yetu ilikuwa ni picha tu tuone kama ni yeye aliyeiba mtoto,” alisema.
Baada ya hapo walirudi nyumbani na usiku huo mama wa mtoto alituma taarifa kwenye mitandao ya kijamii na mdogo wa baba wa mtoto, Ben akatuma picha kwenye blog ya Michuzi pamoja na picha akatoa tangazo la mtoto kuibiwa.
“Hapakukalika wala kulika. Tulikesha hapa nje. Asubuhi ikabidi tugawane na mke wangu yeye aliyeenda  kanisani kwa mtumishi pale Malapa na mimi nikaenda kwa mtumishi wa Tegeta kwenye maombi,” anasema.
“Nilienda kuomba mwanangu apatikane akiwa salama. Nilipotoka pale nikaenda katika vituo vya televisheni  TBC.  Wakati  naingia ITV, kijana ninayemfahamu aitwaye Amir  Juma (aliyeiba mtoto) akanipigia simu. Lakini wakati huo simfahamu kama ni yeye kwa kuwa alibadilisha simu na sauti ilikuwa nzito sana, akawa ananiamuru nimsikilize,” anasema.
“Nilishachanganyikiwa hata nikawa simuelewi nikamwambia kama ni mambo ya kazi wapigie watu wengine mimi nina matatizo, na kwamba tatizo langu ni mtoto wangu ameibiwa. Akaniambia ‘mtoto wako ninaye mimi”, nikamuliza ‘yupo wapi’, akasema Goba.
“Nikampuuza nikaingia ITV. Nilimpuuza kwa vile toka tangazo litoke usiku ule na kwenye mitandao ya kijamii watu mbalimbali walikuwa wananipigia wanasema mara mtu yupo Geita anajifanya mtoto anaye yeye hivyo nitume pesa,  yaani ni utapeli juu ya utapeli sasa na yeye nikamchukulia ni walewale. Wakati tunatoka ITV tupo getini, akanipigia tena simu akaniambia nitume Sh300,000 ili nimpate mtoto wangu. Nikamwambia ‘kama kweli unae nipe niongee naye, basi akanipa mtoto nikasikia sauti ya mtoto wangu ananiambia ‘baba njoo unichukue’, nikamuliza upo wapi? akaniambia nipo huku mbali kwa bibi.
“Kwa kweli niliumia sana rohoni, kisha yule mwizi akamnyang’anya simu akaniambia tuma hizo hela upesi, na dakika 16 zijazo simu yangu itazima chaji nitawasha saa 5:00. Sasa hiyo saa tano aliyoandika nikashindwa kujua alimanisha ni saa 5:00 au saa 11:00. Basi nikarudi nyumbani, sikuthubutu kumwambia mke wangu kama mtoto nimeongea naye na mwizi ametaka hela na nimemtumia. Niliogopa kwa vile alinitisha nisithubutu kumwambia mtu wala kufanya chochote la sivyo angemuua mtoto. Niliona nikimwambia mama yake basi taarifa zitavuja maana hataweza kunyamaza atatangaza.
“Tukaongozana na  mke wangu na majirani wengine na ndugu waliokuwa hapa hadi kwa Mchungaji Bendera pale Sinza. Kufika kwa Bendera nikamuona mtumishi mmoja mkenya ninafahamiana naye muda mrefu tangu nikiwa naishi Arusha. Anaitwa GG. Tukasali pale. Mke wangu hapo yupo hoi hafai, basi tulipomaliza kusali namwambia Mama Merry twende nyumbani mama Merry akawa hataki anang’ang’ania tu kanisani kwa ajili ya maombi tu. Ikabidi nimvute pembeni nimueleze ukweli kwamba mtoto hajafa. Nikamuonyesha ile meseji (ujumbe) ya mwizi aliyokuwa ananisisitiza nimtumie Sh300,000 na nikamwambia akae kimya asimwambie mtu kwa sababu ikivuja, mtoto wetu atauawa.
“Sasa mtindo wa mwizi ukawa ni huo leo anakwambia utume Sh200,000 kesho atakwambia tuma Sh100,000 mara Sh300,000 tena anaamrisha anakwambia usipotuma tunamkorogea mtoto wako maji machafu tunampa aumwe tumbo afie mbali. Nikisikia hivyo inabidi nitume, mara ya mwisho sasa akapiga simu siku hiyo asubuhi analazimisha anataka kuongea na Mama Merry, mi nikamwambia hicho unachotaka kumwambia niambie mimi. Akakataa basi nikampa simu mama Merry akaweka sauti kubwa (loud speaker) akamwambia tumewateka watoto wawili. Shida yetu ni Sh8 milioni. Mwenzenu kashatoa Sh5 milioni sasa bado Sh3 milioni mnatakiwa mzitoe kabla ya saa 8:00. Nilichanganyikiwa ikabidi niende tena polisi nikatoa taarifa.
“Ikabidi nitoke nikahangaikie hela. Lakini  hadi saa 8:30 alikuwa hajapiga. Nilipofanikisha nikarudi nyumbani nikampigia simu akaniuliza saa hizi saa ngapi nikamwambia saa 8:30, akaniambia ‘umechelewa’. Nikamwambia sasa wewe si ulisema utanipigia, baada ya majibizano makali akaniambia nimtumie yote kwenye simu. Kwa sababu kwenye simu huwezi weka hela yote kwa wakati mmoja, inabidi uweke kidogo kidogo,  nikamwambia naomba nikupe hizi hela kwa mkono kisha unikabidhi mtoto wangu, akakataa. Nikamwambia basi muuwe, mke wangu aliposikia natoa kauli hiyo  alilia sana.
Mtekaji anakamatwa
“Kutokana na kupotea kwa mtoto wangu, nilijikuta nawapigia simu watu wote ambao nina namba zao. Amir (mwizi) ni miongoni mwa watu niliowapigia tena na pole akanipa akaniambia yupo Zanzibar, ila atajitahidi kuweka matangazo ya picha ya mtoto wake pale bandarini ili wageni wanaoingia na kutoka waangaliwe na yeye atajitaidi kuulizia huko Zanzibar. Sasa huyu Amir ana namba tatu ambazo mimi nazifahamu, lakini namba aliyokuwa anaitumia kututisha na kumtumia hela ni namba nyingine ambayo aliisajili kwa jina jingine kabisa. Sijui Mohamed, sijui nani. Polisi walichukua namba yangu, ya mke wangu na ile ya mwizi tuliyokuwa tunawasiliana naye. Hapo mimi kila siku mguu polisi, mguu kanisani kwenye maombi. Mpaka mtoto wetu amepatikana tumefanya maombi  makanisa zaidi ya 10.
“Siku  ya tarehe 19 nikaitwa polisi aliyekuwa anafuatilia akaniambia ‘wewe mbona unatuchezea’, nikamuliza ‘kivipi’, akaniambia mwizi wa mtoto wako mbona jana uliongea nae kwa namba hii na yupo Mkata. Mimi kucheki hivi ni namba ni ya Amir nikamwambia ‘haiwezekani’. Wakaniambia ndio hivyo, nikawambia mbona niliongea naye kumueleza tatizo la kutekwa mtoto wangu, akaniambia yupo Zanzibar. Wakaniambia hayupo Zanzibar yupo Mkata, basi nikampigia simu Amir kwa namba  ninazozifahamu nikamuliza ndugu yangu vipi huko ujafanikiwa akasema bado.
“Akaniambia lakini usijali mtoto anaweza kupatikana kwa vile hata yeye mtoto wake aliwahi kupotea Zanzibar lakini alipatikana, ila yeye hakutekwa ingawa mwanzo walidhani hivyo kumbe aliondoka bila kuaga na ndugu yetu akaja kurudi. Nikamwambia njoo basi unisaidie tumtafute wote akasema yeye yupo mbali na amefunga hivyo hawezi kuja Dar. Nilipomwambia Mama Merry mwizi wa mtoto ni Amir alishangaa sana hakuamini kama ni yeye anaweza kufanya unyama huo. Nikamsihi mke wangu asitume meseji popote atulie.
“Wahusika waliokuwa wananishugulikia suala langu wakaifuatilia tena ile namba jioni ikaonekana ipo Mkata, wakati  tunajiandaa na safari ya kwenda Mkata, akaniamuru tena nimtumie Sh100,000 nikamtumia, nikajaza gari mafuta tukaenda Mkata. Tulipofika Mkata tukazunguka Gesti zote za pale hamna kitu. Kesho yake asubuhi, Julai 20 tukaitafuta tena  ile namba ikaonyesha imetoa hela kwa Mtogole, kumbe tulipishana nae, wakati sisi tunaenda Mkata yeye alikuwa amerudi Dar.
“Basi tukaenda mpaka kwenye Kijiji chao kinaitwa Mazingara tukamkamata mama yake mzazi na ndugu zake wote tuliowakuta tukawaweka ndani. Tukarudi Dar. Nikiwa njiani mke wa Amir akanipigia simu akaniambia ‘shemeji mama yake Amir amewekwa ndani’. Nikamwambia mimi sijui, mimi nipo Dar naendelea kumtafuta mwanangu sijui lolote. Tuliporudi hapa sasa tukaenda Tandale kwa Amir hatukumkuta mke wake, baada ya kufuatilia namba yake tukaja kumkamata Tabata Shule kwa mama yake mdogo. Alipobanwa akasema mumewe alimwambia jana yake asilale nyumbani, na akatuambia amesafiri siku hiyo amemuaga anaenda Korogwe. Tukamwambia salama yake apatikane mumewe bila hivyo hatatoka.

“Basi muda ambao tunamkamata mke wake tayari ni saa 9:00 usiku. Usiku ule ule tukaanza safari ya kwenda Korogwe na hapo tayari  askari niliokuwa nao walishaifuatilia namba wameona kweli yupo Korogwe.
“Mke wake akawa anaongea nae kwa simu anamuliza amefikia wapi na kama kweli alichukua mtoto kwa vile dada zake walikuja juu wakamwambia Amir akamtoe mama yake kama kweli hajahusika kwa sababu mama yao ni mzee sana na pia ana matatizo ya mguu.
“Amir akamjibu mke wake yeye hajachukua mtoto anashangaa anavyotafutwa. Tulifika  Korogwe asubuhi Julai 21 tukamuweka mke wake ndani ila tukawambia wasimnyang’anye simu ili mumewe asishtukie. Tukaenda mpaka katika nyumba ya kulala wageni aliyokuwepo, kweli tukamkuta akiwa ametoka kuoga ndipo alipokamatwa.
“Baada ya kipigo kikali na kubanwa sana ndipo alipokiri kumwiba mtoto kwa madai kuwa ofisi aliyokuwa anafanya kazi ameharibu na anadaiwa Sh1.2 milioni hivyo alitishwa na mwajiri wake alipe hizo hela, na akaona njia rahisi ya kupata hizo fedha ni kumwiba mwanangu ili mimi nitoe kwa kuwa ananifahamu na alijua udhaifu wangu.
“Polisi niliokuwa nao wakawapigia wenzao wa hapa Dar wakaelekezwa nyumba ambayo mwanangu aliwekwa huko kwa Mtogole na kweli kufika wakamkuta mtoto. Wakamchukua na kumpeleka Mnazi Mmoja, ndipo nikampigia mke wangu akamchukue mtoto alipoenda akakabidhiwa mtoto na sisi ndio tukaanza safari ya kurudi Dar.”
Alidanganya Merry ni mtoto wake
Katika maelezo yake, Amir alisema alimpeleka kwa Mtogole kwenye nyumba ambayo alikuwa akiishi zamani na kumdanganya yule mama mwenye nyumba yake kwamba kwa sasa anaishi na mwanamke mwingine ambaye ndio anamlea kwa sababu yeye hana kazi na mama mtoto wake amembwagia mtoto hivyo anaogopa akienda naye kwa mke wake atawatimua.
Ishabakaki  anasema Julai 14 kijana huyo alifika mpaka Changanyikeni lakini akawa hajui nyumba akaondoka.
“Kesho yake alikuja na mwenzake na walikaa pale chini ya mti (anaonyesha mti uliopo nje ya nyumba yake). Nasikia walikaa muda sana ndio akaingia kuomba kujisaidia akaonyeshwa choo cha nje, na hapo ndipo alipopata upenyo wa kumteka mtoto,” anasema.
“Amir ni rafiki yangu mkubwa. Awali alikuwa ni mfanyakazi wangu katika karakana yangu, lakini tangu Septemba mwaka jana nilimuachisha kazi. Lakini licha ya kuondoka bado aliendelea kuwa rafiki yangu na hajawahi kuwa adui yangu hata siku moja ndio maana nilishangaa  yeye kufanya kitendo hicho,” anafafanua Ishabakaki .
Akanusha uzushi
“Ndoa yangu ina miaka mitano na kabla sijaoa, tulishakaa na mke wangu kwenye uhusiano kwa muda mrefu na nikamjua vizuri tu. Bahati nzuri  pia Merry ni mtoto wangu wa kwanza. Nadhani kila mtu anajua raha ya mtoto wa kwanza kwenye ndoa. Isitoshe sisi tumehamia hapa Dar akiwa tayari ameshazaliwa. Tuna miaka minne tu hapa mjini, tungekuwa tumeshazaa watoto wengi, ningeweza kuhisi mke wangu kachakachua, lakini  hatuna watoto wengi huyu mdogo kazaliwa hapa hapa juzi juzi tu.
“Wanaosema mtoto alichukuliwa na baba yake wamefilisika kimawazo, mimi wala hayakuniumiza labda mke wangu yalimuumiza kuona labda nitamuhisi alitoka nje ya ndoa. Lakini wala hayanipasui kichwa sana sana yamefanya niimarishe ndoa yangu na nimpende zaidi mke wangu. Kwanza yule mwizi hana hadhi ya kutembea na mke wangu,” alijinasibu Ishabakaki.
Amsamehe mhalifu
Ishababaki anasema alishamsamehe Amir tangu siku ile mtoto wake alipopatikana.
“Sikumgusa hata kwa kofi. Maumivu niliyopata ningemuadhibu vipi roho yangu itulie? Nilimwangalia tu na kwenye gari langu nikambeba njiani ananiambia, “bosi naomba unisamehe... ni ibilisi tu aliniingia mimi sijui hata kwa nini nilifanya hivyo,” alisema akikumbuka tukio hilo na kwamba alimjibu kuwa vitu vingine “tunasingizia ibilisi ni vyetu wenyewe”.
“Njiani nikamnunulia na msosi tukala pale kwa kuwa asubuhi hamna mtu alikuwa amekula kitu. Nikaja naye hadi Dar ndio nikampeleka Oysterbay na kumkabidhisha kwa askari. Sasa nimemuachia Mungu na Serikali naamini haki itatendeka,” anasema.
Mama wa mtoto huyo, Helida Fundi anasimulia kuwa siku tisa za kupotea kwa mtoto wake zilikuwa nyingi sana kwa kuwa hawakuweza kula wala kulala.
“Hapa alipo Merry yupo kwenye dozi ya homa ya mapafu. Nakumbuka alivyoibwa alikuwa kwenye dozi ya malaria, yaani jana yake nilimtoa hospitali alikuwa na malaria tatu. Sasa wiki hii ingeisha hajaonekana, nadhani yangekuwa mambo mengine si ajabu mwanangu angekufa maana siku mbili hizi homa hii ilimbana sana,” anasema mama huyo.
“Nimepungua kilo sita kwa siku tatu, sasa sijui mpaka sasa  nitakuwa nimepungua kilo ngapi. Kila ilipofika usiku, nilikosa amani kabisa nahisi sasa mtoto wangu ndio anafanywa kitu kibaya au anauawa.
“Tulikuwa hatufungi mlango kumsubiri Merry. Tulikuwa tunasema tutafungaje mlango wakati mtoto yupo nje, tulikuwa tunahisi tunamfungia mtoto nje. Si baba yake wala mimi aliyelala. Kwa mara ya kwanza baada ya mtoto kupatikana, baba yake alilala usingizi mzito sana. Mimi bado sijakaa sawa sawa, afadhali siku mbili hizi za Sikukuu ya Idd kidogo naona kama akili inaanza kutulia lakini bado na bado nina uchovu sana,” anaongeza Helida.
Walifunga na kusali
“Toka mwanangu ameibwa kwa siku tisa mfululizo sikumbuki siku niliyokula, wala kulala usingizi, nilifunga na kusali. Nawashukuru wanajumuia wenzangu wa  Mtakatifu Monica, Kigango cha Changanyikeni kila siku jioni walikuja kukesha na kufanya maombi na mimi,” anasema.
Makundi mbalimbali walifunga
Kundi la Motherhood ambalo Helida ni mwanachama katika mtandao wa kijamii wa facebook, liliingia kwenye maombi maalumu kwa ajili ya kumuombea mtoto huyo sambamba na  lile la Tabora Girls ambalo nalo liliingia kwenye maombi  yaliyoambatana na kufunga kwa siku tatu mfululizo.
Mmoja wa wanachama wa kundi hilo ambaye pia ni mama wa ubatizo wa Merry, Sarah Luhaga anasema: “Tulifunga na kufanya maombi siku tatu, siku ya nne asubuhi tukafanya maombi ya shukrani na kutukuza ukuu wa Mungu, tukamwambia Mungu mapenzi yako yatimizwe, mtoto  arudi salama kwa wazazi wake au basi kama ni maiti ionekane. Siku hiyo hiyo jioni saa 11:00 tukaambiwa mtoto kapatikana. Tumeona ukuu wa Mungu. Wanawake ni jeshi kubwa,” anasema Sarah.
Jumapili  Julai  28 wazazi wa mtoto huyo walifanya misa ya shukrani nyumbani kwao Changanyikeni.
MWANANCHI

1 comment:

Anonymous said...

Ingekuwa ulaya hiyo ni movie tayari nyie na mtoto mngekuwa maharufu kwa hilo lkn msikate tamaha