Advertisements

Monday, September 29, 2014

BUNGE MAALUM LA KATIBA:Maamuzi magumu leo

  Kura kupigwa hadi Alhamisi
  Sheria ya mpito kupitishwa Ijumaa
Hatimaye Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba (BMK) leo wanaanza kufanya maamuzi magumu kwa kupiga kura yenye lengo la kupitisha rasimu ya Katiba inayopendekezwa huku kukiwa na taarifa kuwa huenda masuala kadhaa likiwamo theluthi mbili yakaikwamisha.

Hatua ya upigaji kura itakayohitimishwa Alhamisi wiki hii na Ijumaa kutunga sheria ya kipindi cha mpito kabla ya katiba kuanza kutumika, inafikiwa baada ya Bunge hilo kutumia zaidi ya siku 130 mjini Dodoma wakitunga Katiba mpya.

Bunge hilo kwa mara ya kwanza lilianza Februari 18, mwaka huu hadi Aprili 25 baada ya kuahirishwa kupisha Bunge la Bajeti na kuanza awamu ya pili Agosti 5, mwaka huu na kuendelea hadi litakapomaliza muda wake Oktoba 4, mwaka huu.

Kwa muda wote huo wajumbe walikuwa wakijadili, kurekebisha na kuboresha Rasimu iliyowasilishwa ndani ya Bunge hilo na Tume ya Mabadiliko Katiba, ili kupata Rasimu inayopendekezwa ambayo ndiyo itapigiwa kura ya maoni na Watanzania.

Akiahilisha shughuli za Bunge hilo Ijumaa iliyopita, Makamu Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa kabla ya kuanza kwa zoezi la kupiga kura, wajumbe wataanza kwa kuhakiki maudhui yaliyomo ndani ya Rasimu hiyo ili kujiridhisha kama michango ya maoni waliyoyatoa katika majadiliano ya mwisho yamezingatiwa na Kamati ya Uandishi.


“Ndugu wajumbe, siku ya Jumatatu tutakapokutana hapa tutakuwa na zoezi kuipigia kura Rasimu yetu tunayoipendekeza, lakini kabla ya kuanza kupiga kura tutatumia muda mfupi ambapo Kamati ya Uandishi itatupitisha kwa haraka kuhakiki mambo yale tuliyopendekeza katika hatua hii ya mwisho kama yamezingatiwa,” alisema Suluhu.

Kauli hiyo ya Makamu Mwenyekiti wa BMK ilikuja baada ya baadhi ya wajumbe kuhoji kuwa watapigaje kura kabla ya kujiridhisha kuwa yale waliyoyapendekeza katika hatua hiyo ya mwisho yameingizwa kwenye Rasimu.

Hata hivyo dalili zinaonyesha kuwa Rasimu hiyo ipo hatarini kukwama kutokana na baadhi ya wajumbe wenye imani ya kiislamu hasa wale wanaotokea Zanzibar kutoa masharti mawili mazito ambayo kama hayatatekelezwa wamedai kuwa kamwe hawatapiga kura ya kuipitisha.

Wajumbe hao wamedhamiria kukwamisha Rasimu hiyo ikiwa suala la Mahakama ya Kadhi halitaingizwa kwenye Rasimu na pia kama Zanzibar haitaruhusiwa kwa mujibu wa katiba kukopa nje ya nchi bila ya kushauriana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Msimamo huo ulitolewa juzi na wajumbe hao kwa nyakati na namna tofauti, ndani na nje ya ukumbi wa bunge.

Sheikh Masoud Jongo, baada ya kuruhusiwa kuchangia mjadala bungeni alisema; “Tulileta mapendekezo yetu, mpaka sasa tunaona kimya tunachotaka kujua ni yataingizwa au hayaingizwi? Kama hayaingizwi tuna msimamo wetu ambao pengine ubora wa Katiba inayopendekezwa ambayo na mimi naunga mkono kuwa hakika ni bora, utakomea hapahapa, asanteni sana,” alieleza Sheikh Jongo.

Akizungumza na vyombo vya habari kwenye viwanja vya bunge, Dk. Aley Nasoro, alisema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekuwa ikiahidi kuingiza mahakama hiyo kwenye Katiba ya Muungano nyakati za kampeni za uchaguzi, lakini inapopewa ridhaa kuingia madarakani, inapiga danadana utekelezaji wa ahadi hiyo.

Alisema kwa mara ya mwisho iliahidi kutumia mchakato wa mabadiliko ya Katiba kuingiza mahakama hiyo ambayo ni matakwa muhimu kwao, lakini mpaka juzi wakati wakihitimisha mapitio ya Rasimu ya mwisho ya Katiba Mpya inayopendekezwa, halikuwa miongoni mwa mapendekezo.

“Nasema yote yatakayojadiliwa, Katiba iwe nzuri itakavyokuwa bila kitu hicho kwa imani yangu ya Kiislamu sitaafiki chochote kilichomo kwa msingi huo Rasimu hii haifai, sina ridhaa nayo,” alieleza Dk Alley.

Msimamo huo unaiweka Rasimu ya Katiba inayopendekezwa katika hatari ya kutopitishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012 ambayo inaelekeza kuwa ili mabadiliko yoyote ya katiba yawe halali na kukubalika ni lazima yapate theruthi mbili ya kura za ndiyo kutoka upande wa Tanzania Bara na pia upande wa Zanzibar.

Uchunguzi wa NIPASHE unaonyesha kuwa inawezekana hilo likawa ni jaribu la mwisho kwa BMK ambalo kwa muda wote ambao limekutana mjini Dodoma limekabiliwa na misukosuko mingi.

Kabla ya kufikia hatua hiyo ya kupiga kura ambayo ni ya mwisho kabisa kuelekea kuvunjwa kwa BMK, Bunge hilo lilipitia kwenye changamoto za aina mbalimbali tangu wakati wa kuandaa kanuni za kuliendesha.

Baadhi ya mambo magumu ambayo Bunge hilo limepitia ni pamoja na kuamua aina ya kura zitakazopigwa na wajumbe wakati wa kufanya maamuzi kati ya kura ya siri au kura ya wazi.

Baada ya mvutano mkali wa kikanuni hatimaye Bunge hilo lilikubaliana kutumika kwa kura ya wazi na kura ya siri kwa pamoja kulingana na utashi au uamuzi wa mjumbe.

Suala gumu zaidi lililolikabili BMK ni kufanya uamuzi wa aina ya muundo wa Muungoano wa Tanganyika na Zanzibar, ambao baadhi ya wajumbe walikubaliana na mapendekezo ya Rasimu ya Jaji Warioba iliyopendekeza muundo wa Serikali tatu, huku wajumbe wengine hasa wanaotokana na CCM wakitaka muundo wa Serikali mbili uendelee.

Mvutano huo ndiyo uliopelekea Bunge hilo kumeguka, baada ya wajumbe wa ‘Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi’ (Ukawa) linalohusisha wabunge kutoka vyama vikubwa vya upinzani vya NCCR Mageuzi, CUF na Chadema kuamua kutoka nje na kususia kabisa vikao vya Bunge hilo.

Kuondoka kwa wajumbe wa Ukawa kuliibua changamoto nyingine ya kutimia kwa akidi ya wajumbe wanaohitajika kwa mujibu wa kanuni, hasa pale linapokuja suala la kufanya maamuzi kwa kupiga kura kwa kuzingatia sheria inayohitaji kupata theruthi mbili ya kura za wajumbe wote kutoka pande zote za Muungano.

Bunge hilo wiki iliyopita lilifanya marekebisho ya kanuni zake kwa kuruhusu wajumbe walio nje ya Bunge hilo kwa ruhusa waweze kupiga kura kwa njia ya mtandao, hatua iliyoelezwa na baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo na makundi kadhaa ya jamii kuwa inalengo la kuchakachua kura.

Katika kuhakikisha kuwa Rasimu inayopendekezwa inapata theruthi mbili ya kura za wajumbe bila kujali kama wamo ndani ya ukumbi wa Bunge au la, Mwenyekiti wa Bunge hilo alilazimika kutumia ubabe kuhakikisha kanuni inayoruhusu wajumbe kupiga kura wakiwa nje ya BMK inaridhiwa na kupitishwa.

Hata hivyo pamoja na mbinu zote zilizotumika kuvuka mawimbi yote hayo, huenda zikagonga ukuta ikiwa suala la Mahakama ya Kadhi na lile la Zanzibar kupewa mamlaka ya kukopa bila ya kufanya mashauriano na Serikali ya Muungano hayataingizwa kwenye Rasimu ya Katiba, kutokana na msimamo wa baadhi ya wajumbe wenye imani ya dini ya kiislamu.

Kufuatia msimamo huo, tangu Ijumaa jioni Kamati ya Uongozi ya BMK ilikuwa na vikao mfululizo kuona namna inavyovuka kwenye hatua hiyo, huku baadhi ya masheikh kutoka Zanzibar wakiwa wamepiga kambi mjini Dodoma wakifuatilia suala hilo na kuhakikisha linaingizwa kwenye Rasimu.

Hata hivyo, uamuzi wa Bunge hilo kuondoa kufuta mapendekezo mengi ya Rasimu iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba umelalamikiwa na watu na makundi kadhaa ya kijamii wakisema kuwa ni kutoheshimu maoni yaliyotolewa na wananchi kwa Tume ya Jaji Warioba. Wajumbe wa tume pia wamelalamikia hatua hiyo.

Miongoni mwa mambo yaliyotupwa ni muundo wa Muungano wa serikali mbili uliopendekezwa na tume na Bunge hilo kupendekeza serikali tatu, mawaziri wasitokane na wabunge, ubunge kuwa na ukomo wa vipindi vitatu, wananchi kuwa na mamlaka ya mumwomdoa mbunge kama atashindwa kuwajibika, wateule waandamizi wa serikali wakiwamo mawaziri na mabaibu kuthibitishwa na Bunge baada ya uteuzi na elimu ya angalau kidato cha nne kwa wabunge.

Jaji Warioba mwenyewe Ijumaa iliyopita alishangazwa na Katiba inayopendekezwa kuyaondoa mambo hayo na kusema kuwa wanawasubiri wajumbe wa Bunge hilo wakutane nao mitaani kwa wananchi kabla ya kupigwa kwa kura ya maoni ya kupitisha au kutopitisha Katiba inayopendekezwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: