Advertisements

Thursday, September 4, 2014

HIKI NI KIPINDI CHA NEEMA KWA MAKAMPUNI YA UTALII

Sasa ni wakati wa neema ya watalii katika nchi yetu kwenye mbuga za Serengeti na Ngorongoro kwani ni kipindi cha Magration wanyama uhama kwa mafungu kuelekea upande mwingine. Makampuni ya utalii ufanya biashara mzuri kwani watalii wengi uingia hilinkushuudia uhamajiwa wanya hao aina ya nyumbu na pia wanyama wengine ni rahisi kuonekana kwa sababu ujipatia riziki kwenye msafara huo wauhamaji wa nyumbu.
Wanyama wenye tabia ya kuhama ni nyumbu kama unavyoona kwenye picha hii, nyumbu usafiri masafa marefu na katika masafa hayo nyumbu wengine ufariki wakiwasafarini na wanyama wanaofuatilia kwa karibu msafara wa nyumbu wanapohama ni tai.

Ndege huyu mwenye macho makali hufuatilia msafara wa nyumbu kutoka angani.

Sababu kubwa ya ndege huyu kufuatilia msafara huu ni ile mizoga ya nyumbu wanaokufa kutokana na sababu mbalimbali wakati wa msafara.
Tai hula asilimia 70 ya mizoga ya nyumbu wanaokufa katika mikikimikiki ya safari hii ya kuhama kutoka Serengeti kuelekea Masai Mara na kurudi Serengeti.

Kwa maana hiyo, kupungua kwa idadi ya nyumbu katika misafara hii ya kuhama huathiri pia tai ambaye ni mmoja wa wanyama wanaonufaika na misafara hiyo.

Hii ni kwa sababu hata idadi ya mizoga nayo itapungua.

Orodha ya wanyama wanaonufaika na uhamaji wa nyumbu haiishii hapo. Wanyama wengine jamii ya swala kama vile Tomson gazelle nao pia hunufaika na uhamaji wa nyumbu wa Serengeti.

Kutokana na mfumo wa ikolojia wa mbuga hii, mara baada ya ardhi kutifuliwa na miguu ya mamilioni ya nyumbu hawa wanaohama, nyasi mpya huchipua.

Nyasi hizo zinakuwa ni chakula pendwa na kutosha kwa wanyama kama swala ambao nao uhama kutoka eneo moja na kuja kwenye maeneo haya yaliyoachwa na nyumbu.

Tomson gazelle wanafahamika sana kwa kupenda kula nyasi mpya zinazochipua hivyo nyumbu huacha nyuma mazingira ya kuwapatia swala hao chakula wakipendacho na cha kutosha.

Uhusiano na wanyama wengine

Nyumbu huchangamana na wanyama wengine ambao hula majani kama vile pundamilia na nyati.

Wote hupenda kuishi katika ukanda wazi wa nyasi na si kwenye miti mingi. Kuchangamana kwao kunayafanya makundi yao yazidi kuwa makubwa zaidi hivyo kuzidi kuwatisha maadui zao.

Lakini pia kwa kupenda kwao kuishi katika maeneo ya wazi, inakuwa rahisi kwao kuwabaini maadui pale wanapoanza kuwavizia.

Pia, nyumbu ana uwezo wa kubaini na kuzitambua sauti za tahadhari zinazotolewa na wanyama wengine wanapobaini hatari.

Hii inasaidia sana kwa yeye kuzidi kupata ulinzi kwani anazungukwa na wanyama wengi ambao kimsingi wanakuwa kama walinzi wanaoweza kumpa tahadhari hatari inaponyemelea.

Utafiti mmoja ulionyesha kuwa nyumbu hazitambui tu sauti za tahadhari za wanyama anaoishi nao karibu kama vile nyati na pundamilia, bali pia nyani.

Utafiti huo ulionyesha kuwa nyumbu alizitambua kwa haraka na wepesi zaidi sauti za tahadhari za nyani kuliko sauti za mabishano ya wanyama hao.

Nyumbu aliweza kuzitambua na kuzitofautisha sauti hizo licha ya sauti zenyewe kufanana kwa kiasi kikubwa, hasa kwa mnyama ambaye hatoki katika kundi hilo.

Sauti hizo za tahadhari zilitolewa na nyani hao baada ya kuwaona simba na sauti zao za mabishano zilirekodiwa wakati madume mawili ya nyani yakigombana.

Uzazi

Kutokana na tabia yao ya kuhamahama, nyumbu madume na majike hawawezi kuwa na uhusiano wa kudumu.

Lakini nao wana msimu wao wa kujamiiana. Huu ni wakati ambapo madume hujiwekea maeneo madogo ya himaya na kuanza kuwavutia majike.

Maeneo haya ya himaya yanakuwa na ukubwa wa kama meta za mraba 3,000 hivi, hivyo kufanya kuwe na maeneo ya himaya kama 300 hivi katika eneo la kilometa moja la mraba.

Wakati akifanya kazi ya kuwavutia majike kwenye eneo, dume la nyumbu pia linakuwa na jukumu la kulilinda na kulitetea eneo la himaya yake dhidi ya madume wengine.

Madume huwavutia majike kwenye himaya zao kwa kutumia aina maalumu ya sauti kama za kukoroma na mbinu nyingine.

Kwa kawaida, nyumbu hujamiiana katika kipindi cha mwisho wa msimu wa mvua.

Kipindi hiki ni kati ya Mei na Julai kila mwaka. Hiki ni kipindi ambacho wanyama hawa wanakuwa na nguvu nyingi.

Kwanza wanakuwa wamekaa katika eneo hilo kwa kama miezi kumi hivi na wakati huo nyasi huwa zinakuwa nyingi sana hivyo hawapati matatizo ya chakula.

Baada ya kujamiiana wakati huu, nyumbu hubeba mimba hadi kati ya Januari na Machi ambapo huzaa. Hunyonyesha ndama wake kwa muda wa miezi kati ya minane na tisa.

Lakini nyumbu ana uwezo wa kuzaa wakati wowote wa mwaka. Kundi dogo la majike na ndama wao huishi katika eneo la himaya ya dume ambaye amewazalisha majike hao.

Iwapo makundi ya nyumbu yanakutana na kuanza kuishi pamoja, idadi ya majike inakuwa kubwa zaidi ya madume, wataalamu wanaamini kuwa idadi ya madume ni ndogo kutokana na uwindaji haramu.

Kuzaliana

Kutokana na kuwa katika eneo dogo huko Afrika Kusini, nyumbu wa bluu na nyumbu mweusi wameweza kuzaa pamoja.

Lakini hali hii inatokea zaidi katika bustani za wanyama na hifadhi ambako wanyama hawa huwekwa pamoja kwa muda mrefu.

Matokeo ya kujamiiana baina ya jamii hizi mbili tofauti, ni kuzaliwa kwa aina nyingine ya nyumbu ambaye ana sifa za kipekee.

Nyumbu huyu mpya aliyezaliwa ana sifa zilizochanganyika za jamii hizi zote mbili. Lakini pia mzao huu una mpangilio wa meno wa kipekee tofauti na jamii hizi kuu mbili. Pia umbo la pembe zao pamoja na fuvu la kichwa ni tofauti na wenzao.

Uhifadhi

Nyumbu wanapatikana kwa idadi kubwa sana katika eneo la mashariki na kusini mwa Afrika. Huu ni ushahidi wa kufanikiwa kwa juhudi za kumlinda mnyama huyu kwani idadi yao imeendelea kubakia kuwa kubwa.

Hata hivyo, idadi ya nyumbu imeonekana kupungua kwa kasi katika baadhi ya maeneo.

Uhamaji, kama tulivyoona awali, unahitaji maeneo ya ardhi ambao ikolojia yake imeunganika. Lakini kutokana na mabadiliko ya tabia nchi ya miaka ya hivi karibuni, ni vigumu sana kuwa na maeneo kama haya.

Hatari kubwa zaidi kwa nyumbu inatokana na vikwazo vinavyomfanya ashindwe kutekeleza azima yake ya kuhama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine ambako kuna mazingira anayoyahitaji kwa ajili ya ustawi wa maisha yake.

Vikwazo hivi ni pamoja na uzio pamoja na barabara zinazojengwa kuzuia maeneo ambayo wakati mwingine hutumia kama njia zake.

No comments: