ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 30, 2014

Kura za hapana,siri zarindima bungeni

  Kampeni kali zatawala kwa wajumbe
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, jana walianza kupiga kura kupitisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, huku ikifanyika kampeni kali kusaka theluthi mbili za wajumbe baada ya suala la Mahakama ya Kadhi kushindikana kuingizwa kwenye rasimu hiyo.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wajumbe watatu wanaowakilisha madherhebu ya dini na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, walipewa fursa ya kuzungumza na kutoa kauli za kuwashawishi wajumbe wakubali kuipitisha rasimu hiyo huku suala kubwa likiwa ni Mahakama ya Kadhi.

KAULI YA PINDA
Kabla ya hatua ya kupiga kura kuanza jana alasiri, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilazimika kutoa tamko la serikali kufuatia taarifa kwamba wajumbe hususan ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu, wamedhamiria kuipigia kura ya `Hapana' rasimu hiyo.

Msimamo wa kuipigia kura za `hapana' rasimu hiyo ulitolewa mwishoni mwa wiki na baadhi ya wajumbe kwa nyakati tofauti bungeni wakati wakihakiki Rasimu ya Tatu iliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, ambayo haijaingiza suala la Mahakama ya Kadhi kama ambavyo walitaka iwe.

Akitoa tamko hilo, Waziri Mkuu Pinda, alisema linafuatia kikao cha maridhiano cha pamoja kati yake na Kamati ya Uongozi wa BMK ambacho pia kiliwashirikisha pia viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo.

Alisema suala la Mahakama ya Kadhi ambalo lilianza tangu mwaka 2005, lilifikia hatua nzuri kwa waumini wa dini ya kiislamu kuanzisha mahakama hizo mikoa yote nchini, mwaka 2011/12.

Hata hivyo, alisema tatizo ambalo limejitokeza kwa sasa ni utekelezaji wa maamuzi yanayofikiwa kwenye mahakama hizo kwa upande wa serikali.
Alisema: “Taifa hili ukiondoa ubaguzi serikali na kama nchi tumejitahidi sana kama serikali, tumejitahidi sana kama nchi kutenganisha shughuli za imani za dini na shughuli za serikali.”

Alisema huo ndiyo msingi muhimu sana kwa sababu serikali haina dini.“Serikali hii haina dini…nchi hii haina dini, lakini kwa Mtanzania mmoja mmoja, lazima tuheshimu sana yale ambayo yeye anaamini kwa imani yake,” alisema. Alisema kazi ya serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha kila mmoja anapata fursa nzuri ya kuamini imani yake.

Alisema nguzo hii muhimu imesaidia sana kujenga umoja, amani, utulivu na mshikamano wa taifa hili kwa kipindi chote hicho na kwamba ni matarajio ya Katiba mpya nayo italeta mshikamano huo kwa miaka mingi ijayo.

“Nawaombeni sana wote katika jambo hili tusitetereke, tukatae hisia zozote ambazo zitatuletea uvunjifu wa amani,” alisema.Alisema baada ya kikao chao cha Jumamosi, viongozi hao wa dini waliitaka serikali kutoa ahadi ni lini sasa wataboresha sheria zake ili maamuzi yanayotolewa na mahakama hizo yasiendelee kupuuzwa yanapopelekwa serikalini.

Pinda alisema kwa kuzingatia umuhimu huo, serikali itaziangalia sheria zake mbili ambazo ni Sheria ya Mahakama ya Mahakimu, Sura yua 11 na Sheria ya Kiislamu, sura ya 375, na wataleta muswada bungeni ifikapo Januari mwakani.

Alisema kabla ya kuwasilisha muswada huo utawashirikisha wadau wengi na ukifikishwa bungeni wataangalia namna gani bora ya kutekeleza maamuzi yao. Anasema awali alikuwa mbumbumbu sana katika eneo hilo, lakini baada ya mazungumzo hayo ameelewa vizuri.

SHEIKH THABIT JONGO

Akizungumza baadaye Mjumbe wa BMK, ambaye anatoka kundi la 201 (dini), Sheikh Thabit Jongo, alisema wajumbe bungeni humo wanashukuru kwa tamko lililotolewa na serikali kupitia Waziri Mkuu.

“Wajumbe humu ndani wathamini kauli ile iliyotolewa na Waziri Mkuu…kitu nyeti na kinachoweza kuvuruga amani ni suala la imani ya dini mtu. Humu ndani suala la Mahakama ya Kadhi lilitaka kutuvuruga,” alisema.

Alisema wapo Waislamu ambao walikuwa hawaipendi mahakama hiyo na wapo Wakristo pia ambao hawataki mahakama hiyo.Lakini kutokana na tamko lililotolewa na Waziri Mkuu jana, anawaomba wale wote waliokuwa na mipango ya kuipigia kura ya hapana rasimu hiyo sasa mipango hiyo waifute.

Sheikh Thabit alisema maadui wa bunge hilo ni watatu ambao ni kwanza kundi la Umoja wa Katiba ya Tanzania (Ukawa) ambao wangependa bunge hilo livunjike.

Alimtaja adui wa pili kuwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, ambaye mara kwa mara amesikika akilipinga bunge hilo na hata kudai kuwa atakwenda mitaani.

Adui wa tatu kwa mujibu wa Sheikh Thabit, ilikuwa ni suala la Mahakama ya Kadhi, lakini kutokana na tamko la serikali jambo hilo litashughulikiwa ifikapo Januari mwakani kwa maana ya kurekebisha sheria ili utekelezaji wa maamuzi ya mahakama hizo yaweze kushughulikiwa na serikali.
Sheikh Hamid Jongo

Kwa upande wake, Sheikh Hamid Masoud Jongo, alisema kwa kuwa tamko hilo limetolewa na ofisi ya Waziri Mkuu kwa maana ya taasisi basi utekelezaji wake usiwe na kigugumizi tena kesho kutwa.

Alisema Waislamu hawana nia haswa ya kuvuruga mchakato huo, lakini akataka ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu iheshimiwe.

ASKOFU MTETEMELA

Naye Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Donald Mtetemala, alisema suala la Mahakama ya Kadhi kwa muda mrefu lilileta wasiwasi kutokana na hofu ya kusababisha mpasuko kwa jamii ya Watanzania.

Alisema upo mpasuko wa kisiasa, lakini mpasuko wa kidini ni mbaya sana, hivyo ndiyo maana suala hilo limechukua muda mrefu ili kulipatia ufumbuzi.

“Nimeona roho ya kuvumiliana, ukomavu katika tamko la Waziri Mkuu Pinda. Alisema rasimu hiyo ina suala la msingi kwamba serikali na nchi hii kwa ujumla haina dini.Aliwaomba waumini wa dini ya Kikristo kuelewa suala hilo kwa mapana yake.

CHENGE

Mapema Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi, Andrew Chenge, akiwasilisha marekebisho ya Rasimu ya Katiba inayopendekezwa alisema rasimu hiyo imefuta na kuandika upya Ibara ya 2(2) ambayo sasa itakuwa ikisomeka kuwa, “Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka ya kuigawa Jamhuri katika mikoa, wilaya na maeneo mengine:
Alisema: “Isipokuwa kwa upande wa Tanzania Bara, Rais atashauriana na Rais wa Zanzibar kabla ya kuigawa Tanzania Zanzibar katika mikoa, wilaya au maeneo mengine.”

Kabla ya marekebisho hayo, rasimu yake aliyoiwasilisha wiki iliyopita, ilisema kwamba Rais wa Jamhuri angekuwa na mamlaka ya kuigawa mikoa, wilaya Tanzania Zanzibar, lakini bila kushauriana na Rais wa Zanzibar.

Aidha, alitaja marekebisho mengine kuwa ni kuongeza Ibara mpya ya 44A inayozungumzia Haki za wakulima, wafugaji, wavuvi na wachimbaji madini.

Pia, alisema rasimu imeongeza Ibara mpya 48A kuhusu Haki ya afya na maji safi na salama na Ibara ya 55 imefanyiwa marekebisho na kuweka haki kwa wazee.Alisema Ibara nyingine iliyoongezwa ni ya 100A inayohusu Makamu wa Kwanza wa Rais kushindwa kumudu majukumu yake.

Kuhusu idadi ya mawaziri alisema rasimu imeweka ukomo kwamba sasa imeweka idadi ya mawaziri na manaibu wao wasizidi 40.

Alisema rasimu pia imeunda Tume ya Uratibu na Uhusiano ya Muungano ambayo itakuwa ikishughulika na usuluhishi wa migogoro kati ya pande mbili za Muungano kabla ya kufikisha migogoro hiyo Mahakama ya Juu.

Ibara nyingine mpya ni 208A ambaye inazungumzia Tume za Kisekta ambayo itakuwa na tume mbalimbali za huduma. Kadhalika, alisema rasimu imeongeza ibara nyingine mpya 242 kuhusu Udhibiti wa rushwa.

UPIGAJI WA KURA
Zoezi la upigaji kura lilianza kwa kusuasua baada ya baadhi ya wajumbe hasa wa kutokea upande wa Zanzibar, kuikataa kwa kupiga kura za wazi.

Hatua ya baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar kupiga kura ya hapana, ilitarajiwa kutokana na msimamo wao wa awali waliouonyesha baada ya suala la Mahakama ya Kadhi kutoingizwa kwenye Rasimu hiyo.

Wajumbe hao bila woga walipiga kura ya wazi na kutamka kuwa hawaungi mkono ibara zote za Rasimu hiyo.
Hata hivyo, wapo baadhi ya
CHANZO: NIPASHE

No comments: