Habari zilizopatikana jijini zinaeleza kuwa Mtawala ameachishwa kazi na si kwamba amecha kazi kama ilivyoelezwa na shirikisho hilo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mtawala, alisema kuwa ni 'siasa' za mpira wa Tanzania ndiyo zimemuondoa katika nafasi hiyo aliyokuwa akiishikilia kwa muda wa miezi nane.
Alisema: "Sitakaa kimya, nitahakikisha haki zangu zinapatikana."Kwa kifupi siasa ndiyo zimeniondoa, ila najua haki zangu nitapata kwa sababu nilikuwa na mkataba wa miaka miwili, nitatengeneza fedha ambazo sikufikiria kuzipata kwa wakati huu (alitaja kiwango)."
Mtawala ambaye aliamua kuachia ngazi nafasi ya ukatibu mkuu wa Simba na kujiunga na TFF miezi nane iliyopita, alisema Tanzania ina safari ndefu katika kusaka maendeleo ya soka kwa sababu 'vijana' wenye elimu na wanaosimamia kanuni na taratibu wanaonekana kikwazo kufanya kazi katika taasisi zinazojishughulisha na mchezo huo.
Taarifa zaidi zinadai kwamba Mtawala ameachishwa kazi akidaiwa kuvujisha siri kutoka ndani ya shirikisho hilo.
Inadaiwa kwamba TFF ilifikia maamuzi hayo ikiamini kwamba Mtawala ndiye aliyewaambia Simba wamsajili Okwi, baada ya Yanga awali kutopeleka jina lake kwenye orodha ya wachezaji itakaowatumia katika msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Pia anadaiwa ndiye 'aliyevujisha' barua za Yanga za kumuacha Okwi na kumshtaki kwa madai ya kuikacha timu hiyo na kusababisha ipoteze ubingwa wa Bara msimu uliopita.
"Kwa muda sasa Mtawala alionekana kutofautiana na uongozi wa shirikisho hilo na ndicho chanzo kikubwa cha kumfanya aondoke, ni kama walikuwa wanasubiri kupata sababu au chanzo cha kumuondoa," alisema kiongozi mmoja wa soka hapa nchini.
Sababu nyingine inayodaiwa kumfanya Mtawala ambaye kitaaluma ni mwasheria, asiaminike na viongozi wa TFF ni kudaiwa kutoa siri wakati wa mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Simba uliofanyika Juni 29, mwaka huu.
Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, alithibitisha kuachia ngazi kwa Mtawala lakini akasema ni kwa sababu mbalimbali ikiwamo kutaka kwenda kuegemea zaidi katika taaluma yake ya uanasheria.
Mtawala alipewa barua rasmi ya kumaliza ajira yake TFF juzi Agosti 31, mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment