ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 2, 2014

Polisi Stakishari watuhumiwa kuua raia

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Ernest Mangu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala limeingia katika kashfa mpya ya kudaiwa kumpiga hadi kufa mkazi wa Mtaa wa Karakata, Kata ya Kipawa, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, Liberati Damiani Matemu (59), baada ya kumshikilia kwa siku nane.

Kutokana na tukio hilo, familia ya Matemu imewasiliana na mwanasheria kwa ajili ya kuchukua hatua stahili iwapo polisi waliohusika na mauaji hayo hawatachukuliwa hatua.

Tukio hilo lilitokea wiki iliyopita, katika kituo cha polisi cha Stakishari, ambako marehemu (Matemu), alishikiliwa kwa siku nane bila dhamana.

Akisimulia tukio hilo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam waliofika nyumbani kwa marehemu, Wakili wa familia hiyo, Bagiliye Bahati, alisema Matemu alifariki alfajiri ya Jumamosi iliyopita, wakati akipata matibabu yaliyotokana na kipigo katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Fahamu Muhimbili (Moi).


Alisema Agosti 22, mwaka huu, Matemu akiwa kwenye biashara yake ya Meku Pub, iliyopo eneo la relini Karakata, alikuja mtu (jina limehifadhiwa kwa sasa) na kuanza kumshambulia, lakini alijihami kwa kutumia panga.

Alisema palitokea vurugu na baada ya muda, polisi walifika na kumkamata mmiliki wa baa hiyo, lakini ndugu walivyokenda kumdhamini walipigwa chenga licha ya kutimiza masharti ya dhamana.

“Mara chache walizoenda walimuona ndugu yao akiwa na afya njema, walimpa chakula na nguo za kubadilisha, lakini kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele walikatazwa kumuona na walivyopeleka chakula kilipokelewa na kuingizwa ndani,” alisema.

Mke wa marehemu, Naomi Liberati, alisema Ijumaa alielezwa hali ya mumewe ilikuwa mbaya na amepelekwa Hospitali ya Amana, na baada ya kufika walimkuta anapumua kwa mashine, huku akiwa uchi.

Alisema taarifa ya polisi ya PF3 yenye namba STKI RB/ 11246/14 iliandikwa kuwa alijeruhiwa na walipouliza kwa polisi aliyekuwa anamlinda, alidai kuwa walimuokota baada ya kupigwa na wananchi wenye hasira kali.

“Hadi sasa ile ni maiti yao, walimchukua ndugu yetu akiwa mzima wa afya. Tunataka wamrudishe akiwa na afya yake njema…haiwezekani mtu yupo mikononi mwao kwa siku nane bila kumpeleka mahakamani halafu tunamkuta hospitali akiwa mahututi, huku analindwa. Iweje kibaka alindwe?” alihoji.

Liberari alisema walimuuliza daktari aliyempokea, alisema marehemu alikuwa amejeruhiwa na damu imevimbia kichwani na walipomtazama alikuwa na majeraha sehemu nyingi, ikiwamo mkononi, ambako alikuwa kama amefungwa kwa kamba.

Wakili Bahati alisema Mei 23, mwaka huu, mteja (jina linahifadhiwa), alifika kwenye baa hiyo na kunywa vinywaji, ambavyo alikataa kulipa na Matemu alidai fedha yake kwa kumzuia asiingie ndani ya gari, lakini alimburuza na kumgonga.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema lina utata, hivyo amemwagiza Mkuu wa Upelelezi, kwenda kituoni humo kuchunguza zaidi.

 
CHANZO: NIPASHE

No comments: